Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres atambua uamuzi wa ICJ kuhusu Gaza, sasa kuwasilisha notisi Baraza la Usalama

Msichana mwenye umri wa miaka 11 ameketi kwenye vifusi vya nyumba huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Msichana mwenye umri wa miaka 11 ameketi kwenye vifusi vya nyumba huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Guterres atambua uamuzi wa ICJ kuhusu Gaza, sasa kuwasilisha notisi Baraza la Usalama

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Muda mfupi baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ huko The Hague, Uholanzi kupitisha uamuzi wa kuitaka Israel pamoja na mambo mengine ichukue hatua zote chini ya uwezo wake wote ku kuepusha mauaji ya kimbari dhidi ya wapalestina huko Ukanda wa Gaza na kuhakikisha misaada ya kiutu inaingia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametambua uamuzi huo. 

Uamuzi huo wa ICJ ambacho ni chombo kikuu cha haki cha Umoja wa Mataifa, unafuatia shauri lililowasilishwa na Afrika Kusini la kutaka Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa ichukue hatua za awali kwa mujibu wa Mkataba wa kimataifa wa kuepusha mauaji ya kimbari wa mwaka 1948.  

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema “kinachofuatia sasa kwa mujibu wa Mkataba wa kuanzisha ICJ, Katibu Mkuu atawasilisha kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa notisi hiyo ya hatua za awali kama ilivyoagizwa na Mahakama.”  

Katibu Mkuu ametambua pia agizo la Mahakama la kuitaka Israel ihakikishe haraka iwezekanavyo jeshi lake halitekelezi vitendo vyovyote vinavyokiuka Mkataba wa Kimataifa kuhusu mauaji ya kimbari ambao Israel ni mwanachama.  
Kingine pia ni Israel kuhakikisha usambazaji wa huduma za msingi na huduma za kiutu zinatolwe ili kutatua mazingira na changamoto zinazokumba wakazi wa Gaza.   

“Ametambua pia msisitizo wa Mahakama ya kwamba pande zote kwenye mzozo huko Ukanda wa Gaza zinawajibika chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu,” na kwamba inataka kuachiliwa mara moja na bila masharti mateka wote waliotekwa nyara wakati wa shambulio lililofanywa na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas na wengine dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023.  

Katibu Mkuu amesema kwa mujibu wa Mkataba wa kuanzisha ICJ, maamuzi yake yoyote yana nguvu na hivyo “naamini pande zote zitazingatia ipasavyo Agizo hilo kutoka mwa Mahakama.”