Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia 25 wameuawa Oicha DRC wiki hii na wengine kadhaa kujeruhiwa:UN

Moja ya maeneo mengi ya wakimbizi wa ndani ambayo yamechipuka huko Kivu Kaskazini ambapo watu milioni 1.2 wamelazimika kukimbia makazi yao.
© UNHCR/Blaise Sanyila
Moja ya maeneo mengi ya wakimbizi wa ndani ambayo yamechipuka huko Kivu Kaskazini ambapo watu milioni 1.2 wamelazimika kukimbia makazi yao.

Raia 25 wameuawa Oicha DRC wiki hii na wengine kadhaa kujeruhiwa:UN

Amani na Usalama

Machafuko yanayoshika kasi katika jimbo la Kivu ya Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, yameendelea kukatili Maisha ya watu , kujeruhi na kuwalazimisha wengi kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini New York Marekani msemaji wa Umoja huo Stephane Dujarric amesema “Taarifa kutoka kwa ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu nchini DRC imeonya juu ya kuendelea kwa machafuko Kivu Kaskazini na siku ya Jumatatu shambulio jipya lililofanywa la kundi la wanamgambo wenye silaha kwenye mji wa Oicha  mjini Beni lilikatili Maisha ya raia 25, kujeruhi wengine kadhaa na kulazimisha watu 1,500 kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao.”

Taarifa yake imeongeza kuwa shughuli za kibinadamu katika mji huo hivi sasa zimesitishwa na wafanyikazi wa kibinadamu wameondolewa kwa muda.

Changamoto ya usambazaji wa chakula

Pia amesema vurugu hizo zinazoendelea Kivu Kaskazini zimetatiza usambazaji wa msaada muhimu wa chakula unaokusudiwa kuwafikia zaidi ya watu 25,000 waliokimbia makazi yao na watu wengine walio hatarini kote katika jimbo hilo la Kivu Kaskazini.

Tangu mapema mwezi huu wa Oktoba, ghasia hizo zimesababisha takriban wanaume, wanawake na watoto 200,000 kuhama makazi yao, hasa katika maeneo ya Masisi na Rutshuru.

Amemalizia taarifa yake kwa kusema kuwa “Tumekuwa tukiangazia mzozo unaoendelea katika eneo hili kwa muda. Licha ya mazingira tete, mashirika ya kibinadamu yanasalia kujitolea kuongeza hatua za msaada wa kibinadamu.”

Tangu tarehe 15 Oktoba, watu 140,000 waliokimbia makazi yao wamepokea msaada wa chakula katika eneo la Masisi.