Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi huko Beni ni ya kupanga hivyo lazima watekelezaji wawajibishwe- Lacroix

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akisalimia wakazi wa Beni wakati wa doria huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
UN Photo/Sylvain Liechti
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akisalimia wakazi wa Beni wakati wa doria huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Mashambulizi huko Beni ni ya kupanga hivyo lazima watekelezaji wawajibishwe- Lacroix

Amani na Usalama

Akiwa ziarani jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix amesema mashambulizi dhidi ya walinda amani na wafanyakazi wa kibinadmu nchini humo si vitu vya ghafla bali ni matukio ya kupangwa na yanafadhaliwa na hivyo hayapaswi kukwepa mkono wa sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Goma hii leo baada ya mkutano wake na Gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini Carly Nzanzu Kasivita, Lacroix amesema “kila mtu anahitaji kujifunza kutokana na matukio ya hivi karibuni nchini DRC na kwamba wawili hao wamekubaliana kuwa kuna mambo ambayo wanaweza kufanya vizuri zaidi. MONUSCO bila shaka itaangalia ni mambo yapi inaweza kufanya kwa vizuri na kwa kina zaidi.”

Bwana Lacroix amesema anaamini kuwa “kulikuwepo na ahadi kutoka kwa mamlaka kuhusu jinsi ya hatua za kiusalama kuwa bora zaidi na zaidi ya yote, uratibu bora kwa sababu tunahitaji na imesisitizwa kwa uthabiti, ili hatua hizo ziwe na ufanisi. Inahitaij pia ubia wa karibu, mipango ya pamoja na kazi ya pamoja kuanzia mwanzoni kabisa.”

Mkuu huo ulinzi wa amani amesema kuwa katika mazungumzo yao walisisitiza umuhimu wa kutokuwepo kwa ukwepaji sheria katika mashambulio kwenye kituo cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO na pia kwa wahudumu wa Ebola.

“Watekelezaji wote lazima watambuliwe na wawajibishwe kwa vitendo vyao,” amesema Lacroix.

Mashambulizi hayo yalilaaniwa vikali na Mwakilishi wa maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC na mkuu wa MONUSCO, Leila Zerrougui.