Madai mengine ya unyanyasaji wa kingono yaibuka MONUSCO DRC
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema ofisi ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC-(MONUSCO) imepokea madai mengine ya miendendo mibaya ikiwemo unyanyasaji wa kingono, ukiwahusisha walinda amani kutoka Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi habari mjini New York, Durarric amesema taarifa mpya zaonyesha kuna madai matatu ya unyanyasaji wa kingono yaliyohusisha watu kadhaa.
Sauti ya Stephane Dujarric
“Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, madai matatu ya unyanyasaji wa kingono ukiwahusisha watu wazima watatu, moja likiwa la kuwa baba na lingine kuhusu madai ya matunzo kwa mtoto. Inadaiwa matukio hayo yalifanyika sehemu za sake, Beni na Goma katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Shirika la UNFPA limekuwa likihusika ili kuhakikisha kuwa waathiriwa wanapata msaada wa haraka”..
Nalo dai la nne linahusu mvulana wa miaka 17 kupigwa na mlinda amani Mashariki mwa Kasai. Muathirika ameelekezwa kwa UNICEF ili kupata msaada na ulinzi na anachunguzwa na ofisi ya pamoja na haki za binadamu.
Stephane ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa tayari umeifahamisha serikali ya Afrika Kusini kuhusu madai hayo.
sauti ya Stephane Durarric
“Umoja wa Mataifa umeshaiarifu nchi ya watu husika na kuiomba iteue maafisa wakitaifa wa uchunguzuzi katika kipindi cha siku tano na kuwa uchunguzi wa Madai hayo ukamilishwe chini ya mda wa siku 90, na kwamba uchunguzi huo utafanyika kwa pamoja na timu kutoka ofisi ya huduma za masuala ya ndani.”
Dujarric amesisitiza kuwa mkakati wa Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha kuwa waathirika wanapata msaada na pia MONUSCO itachangia msaada kama vile kukusanya sampuli za viini nasaba-DNA na kusikitishwa na madai ya unyanyasaji wa kingono licha ya juhudi kwa nchi washirika za kuzuia na kushughulikia unyanyasaji wa kingono.