Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia 18 wamejeruhiwa na 4 mahutusi katika machafuko Kivu Kaskazini DRC:UN

Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
MONUSCO/Sylvain Liechti
Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Raia 18 wamejeruhiwa na 4 mahutusi katika machafuko Kivu Kaskazini DRC:UN

Amani na Usalama

Taarifa kutoka mpango wa Umoja wa Mastaifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC zinasema hali katika Mashariki mwa nchi hiyo bado ni ya wasiwasi mkubwa , huku kukiwa na ripoti za mapigano kati ya wanajeshi wa serikali FRDC na kundi la wapiganaji la M23 kusini na kusini-mashariki mwa eneo la Kitchanga, katika jimbo la Kivu Kaskazini. 

Mapigano pia yameripotiwa huko eneo la Kishishe kama kilomita 25 kaskazini Magharibi mwa Rutshuru ikiwa ni pamoja na matumizi ya silaha nzitonzito.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa hii leo mjini New York Marekani hii inafuatia mfululizo wa mashambulizi siku mbili mfululizo ya kundi la M23 kwenye maeneo ya jeshi la DRC magharibi mwa Rutshuru mashambulizi yaliyosababisha kaya takriban 4,300 kufungasha virago na kuyahama makazi yao.

Athari za mapigano hayo kwa raia

Kwa mujibu wa MONUSCO kufuatia mapigano hayo watu 450 wamesaka hifadhi kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa mjini Kitchanga, ambako wanapatiwa huduma muhimu kama mahema , chakula, maji na msaada wa huduma ya kwanza.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanashika doria kwenye kambi hiyo na maeneo jirani ili kuwalinda watu hao na vijiji dhidi ya makundi yenye silaha yasiweze kuwadhuru.

Jana MONUSCO iliripoti kuhusu mlipuko mkubwa kwenye mji wa Beni ambako takriban raia 18 wakiwemo wanawake 13 walijerujiwa na 4 miongoni mwao wako mahututi.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya huduma za kutegua mabomu UNMAS imetuma timu ya wataalam kwenye eneo hilo la mlipuko kufanya uchunguzi na kuelimisha raia juu ya jinsi ya kujikinga na vilipuzi vya aina hiyo.