Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zilizo katika bonde la mto Nile kunufaika na mradi wa tahadhari za mapema

Chini ya nusu ya Nchi Zilizoendelea na chini ya theluthi moja pekee ya Nchi Zinazoendelea za Visiwa Vidogo zina mfumo wa maonyo ya mapema.
© UNDRR/Amir Jina
Chini ya nusu ya Nchi Zilizoendelea na chini ya theluthi moja pekee ya Nchi Zinazoendelea za Visiwa Vidogo zina mfumo wa maonyo ya mapema.

Nchi zilizo katika bonde la mto Nile kunufaika na mradi wa tahadhari za mapema

Tabianchi na mazingira

Maji yakiwa mengi yanaweza kusababisha mafuriko kama yaliyotokea hivi karibuni huko nchini Libya na uwepo wa maji kidogo unaweza kusababisha ukame kama hali ilivyo kwa nchi nyingi za ukanda wa Jangwa la Sahara kwa sasa, na ndio maana wadau wa masuala ya hali ya hewa wametaka suala la maji kuwa kitovu wakati dunia inashughulikia mabadiliko ya tabianchi. 

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa WMO, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza hatari za majanga UNDRR, Shirikisho la chama cha Msalaba mwekundu na Mwezi mwekundu IFRC na Kituo cha Ufadhili wa Uchunguzi wa Utaratibu SOFF wadau hao wanatarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa mabadiliko ya tabianchi ambao umejikita katika kuzingatia zaidi suala la maji.

Mradi huo Kutoka kwenye satelaiti hadi viroba vya mchanga”: Kuweka maji katikati ya hatua za tabianchi unaofadhiliwa na Uholanzi kwa muda wa miaka mitano unagharimu dola milioni 64.75, u utatekelezwa katika nchi zinazounda bonde la mto Nile ambazo ni Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda kwakuwa nchi hizo zinaelezwa kuwa katika hatari kubwa ya kuathirika na mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huo unatarajiwa kushughulikia hatari zinazohusiana na hali ya hewa ambazo mara nyingi huangukia kati ya nyufa za sera nyingi za ngazi ya nchi zinazo husu maji, usafi wa mazingira na kujisafi (WASH).

Katibu Mkuu wa WMO Prof. Petteri Taalas amesema mradi huo “utatoa mchango unaoonekana kwenye mpango wa tahadhari za mapema kwa wote.”

Katika mradi huo ushirikiano wa mashirika hayo ukichanganywa na maarifa ya ndani katika nchi husika na teknolojia ya kimataifa inaamika utasaidia jamii kuelewa na kuchukua hatua kuhusu hatari zinazohusiana na maji zinazowakabili kabla hazijawa na majanga.

“Kupitia ushirikiano wetu, hatua hizo zinaweza kutoa taarifa na teknolojia ikijumuisha utabiri na uchunguzi bora zaidi“ amesema Katibu Mkuu wa IFRC Jagan Chapagain.