Kutochukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kunaweka rehani maisha ya watu: WMO
Kutochukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kunaweka rehani maisha ya watu: WMO
Ukosefu wa hatua za kutosha kuelekea utimizaji wa malengo ya mabadiliko ya tabianchi unapunguza kasi ya mapambano ya kimataifa dhidi ya umaskini, njaa na magonjwa hatari, kulingana na ripoti iliyotolewa leo na shirika la hali ya hewa la Umoja wa Mataifa WMO.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliunga mkono ujumbe huo, akionya kwamba hali ya joto inayovunja rekodi na hali mbaya ya hewa vinasababisha maafa kote ulimwenguni.
Juhudi nah atua za kimataifa hazijakidhi matakwa amesisitiza Bw. Guterres kama vile takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa malengo ya maendeleo endelevu SDGs ni asilimia 15 tu ya malengo yote 17 ndiyo yako kwenye mstari wakati huu ambapo malengo hayo ya Ajenda ya 2030 yako katikati wa muda wa kuyatimiza.
Kusuasua kwa malengo ya SDGs
Kulingana na WMO, sera za sasa zitasababisha ongezeko la joto duniani la angalau nyuzi joto 2.8 juu ya viwango vya kabla ya kuanza kwa maendeleo ya viwanda katika kipindi cha karne hii kiwango ambacho ni juu ya shabaha ya makubaliano ya Paris ya kuhakikisha joto linasalia katika nyuzi joto 1.5°C.
Majira ya joto ya mwaka huu ya kaskazini mwa nchi ya ulimwengu yamekuwa ya kupindukia katika rekodi, na kumfanya mkuu wa Umoja wa Mataifa wiki iliyopita kusisitiza wito wake wa "kuongeza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi".
Katika dibaji yake ya ripoti hiyo, Bw. Guterres amesisitiza kwamba hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi, na sayansi zinazohusiana na maji na hali ya hewa vinaweza kuongeza kasi ya hatuia katika SDGs katika kila nyanja".
Maisha yako katika mzani
Ripoti ya muungano katika Sayansi, ambayo inachanganya utaalamu kutoka kwa mashirika 18 ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine, inaonyesha jinsi sayansi ya mabadiliko ya tabianchi ilivyo bayana na tahadhari za mapema vinaweza kuokoa maisha na uwezo wa watu kuishi, kuendeleza uhakika wa chakula na maji, nishati safi na afya bora.
Baada ya mafuriko ya hivi karibuni nchini Libya ambayo yamegharimu maisha ya maelfu ya watu, katibu mkuu wa WMO Petteri Taalas amesisitiza kuwa ukosefu wa uwezo wa kutosha wa utabiri unaweza kuwa na matokeo mabaya kwa nchi wakati inakabiliwa na hali mbaya ya majanga ya hali ya hewa.
Ameangazia hali ya hatari inayoendelea nchini Sudan, ambapo migogoro imelemaza uwezo wa shirika la utabiri wa hali ya hatari ya hewa.
Mkuu wa huduma ya utabiri wa hali ya hewa nchini humo amemwambia kuwa wafanyakazi wake wengi walitoroka Khartoum na hawakuweza kuendesha shughuli zao kwa njia ya kawaida".
Ameonya kwamba kwa mantiki hiyo "Hawawezi tena kutabiri aina hii ya matukio ya hali ya hewa yenye athari kubwa tena".
Sayansi ya hali ya hewa ni muhimu kwa uhakika wa chakula
Matukio mabaya ya hali ya hewa ni sababu kuu ya kuenea kwa njaa duniani na ripoti hiyo mpya inataka kufahamisha hatua za haraka kuhusu suala hili kwani Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu watu milioni 670 wanaweza kuwa na uhaba wa chakula ifikapo mwaka 2030.
Waandishi wa ripoti hiyo wanachunguza uhusiano kati ya uzalishaji wa chakula kinachookoa maisha na lishe, na uwekezaji katika sayansi ya hali ya hewa na huduma ambazo huwawezesha wakulima kufanya maamuzi juu ya mazao na upandaji.
Tahadhali za mapema pia ni muhimu kwa "kusaidia kutambua maeneo yanayoweza kuharibika ya mazao ambayo yanaweza kuwa na uzalishaji duni wa mazao na kusababisha dharura".
Kutarajia milipuko hatari
Muungano katika Sayansi unajumuisha uchambuzi kutoka kwa jopo la serikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi (IPCC), ambalo lilionya kuwa mabadiliko ya hali ya hewa na matukio makubwa kama vile mawimbi ya joto yanaweza "kuongeza kwa kiasi kikubwa majanga ya afya na vifo vya mapema".
Matokeo ya ripoti hiyo yanaonyesha kuwa kuunganisha taarifa za magonjwa na hali ya hewa kunawezesha kutabiri na kujiandaa kwa milipuko ya magonjwa yanayotokana na athari za hali ya hewa, kama vile malaria na dengue.
Punguza hasara zitokanazo na majanga
Mifumo ya tahadhari za mapema pia inaweza kusaidia kupunguza umaskini kwa kuwapa watu nafasi ya kutarajia na kupunguza athari za kiuchumi zitokanazo na majanga.
Ripoti iliyoongozwa na WMO inaonyesha kuwa kati ya 1970 na 2021, kulikuwa na karibu majanga 12,000 yaliyoripotiwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi na maji yaliyokithiri, na kusababisha hasara ya dola trilioni 4.3 na mengi kati ya majanga hayo yalitokea katika nchi zinazoendelea.
Kila sehemu ni muhimu
WMO imesema imesikitishwa na ukweli kwamba hadi sasa, kumekuwa na hatua ndogo sana zilizopigwa katika kupunguza pengo kati ya ahadi ambazo nchi zilitoa kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kiwango cha upunguzaji wa hewa chafu kinachohitajika sana kufikia lengo la kupunguza ongezeko la joto la mkataba wa Paris.
Ili kupunguza ongezeko la joto duniani hadi kufikia nyuzijoto 1.5°C, uzalishaji wa gesi chafuzi duniani lazima upunguzwe kwa asilimia 45 ifikapo 2030, huku uzalishaji wa hewa ukaa (CO2) ukikoma kabisa ifikapo mwaka 2050.
Waandishi wa ripoti hiyo wameandika kwamba ingawa baadhi ya majanga ya mabadiliko ya hali ya hewa ya siku zijazo hayawezi kuepukika, "kila sehemu ya kiwango na tani ya hewa ukaa au CO2 ni muhimu kushughulikia kupunguza ongezeko la joto duniani na kufikia malengo ya SDGs".
Tahadhari za mapema kwa wote
WMO pia imesisitiza umuhimu wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa "Tahadhari za Mapema kwa Wote" unaolenga kuhakikisha kuwa "kila mtu duniani analindwa dhidi ya hali ya hatari ya tabianchi, maji, au matukio ya hali ya hewa kupitia mifumo ya tahadhari ya mapema ya kuokoa maisha ifikapo mwisho wa mwaka 2027".
Hivi sasa, ni nusu tu ya nchi duniani kote zinaripoti kuwa na mifumo ya kutosha ya tahadhari za hatari nyingi za hali ya hewa.
Ripoti hiyo ya muungano wa sayansi imetolewa kabla ya mkutano wa kilele wa SDG na wa malengo ya tabianchi utakaofanyika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki ijayo.
Mikutano hii "itaangazia jinsi ya kunusuru malengo ya SDGs ikiwa ni katikati ya utimizaji waajenda ya 2030 na kuongeza hamasa ya kukabiliana na mzozo wa mabadiliko ya tabianchi", mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa aliwaambia waandishi wa habari mjini New York Marekani jana Jumatano.