Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na wadau wasaka dola bilioni 1.2 kushughulikia mgogoro wa wakimbizi Afrika

Soko nchini Sudan Kusini
© UNICEF/Sebastian Rich
Soko nchini Sudan Kusini

UNHCR na wadau wasaka dola bilioni 1.2 kushughulikia mgogoro wa wakimbizi Afrika

Wahamiaji na Wakimbizi

UNHCR, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, pamoja na washirika wengine 102 wa kibinadamu na masuala ya maendeleo wanaomba dola za Marekani bilioni 1.2 ili kuwasilisha misaada ya kibinadamu inayohitajika na ulinzi kwa wakimbizi milioni 2.3 wa Sudan Kusini na jumuiya za wenyeji zinazopokea wakimbizi hao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ethiopia, Kenya, Sudan, na Uganda.

Baada ya takriban muongo mmoja wa vita na licha ya juhudi za kutekeleza makubaliano ya amani, Sudan Kusini inaendelea kukabiliwa na ghasia za hapa na pale, kutokuwepo na uhakika wa chakula na athari mbaya za mafuriko makubwa yaliyoikumba nchi hiyo hivi karibuni.

Shirika hilo la wakimbizi limesema pia janga la COVID-19 limedhoofisha rasilimali za watu, na kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kukidhi mahitaji yao kwa njia endelevu.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa UNHCR mjini Geneva Uswis nchi zinazotoa hifadhi kwa wakimbizi nazo zinakabiliwa na changamoto kama hizo kutokana na mabadiliko ya tabianchi na janga la COVID-19 lakini zimeendelea kuweka milango wazi kwa wakimbizi.

“Ufadhili unahitajika kwa haraka ili kusaidia nchi zinazowakaribisha kutoa chakula, malazi na upatikanaji wa huduma muhimu kama vile elimu na afya.” Limesema shirika la UNHCR.

Watoto wakichungulia nje kupitia dirishani nchini Sudan Kusini.
© UNMISS/Amanda Voisard
Watoto wakichungulia nje kupitia dirishani nchini Sudan Kusini.

Fedha zitakavyotunmika

UNHCR imesema kuwa Serikali katika nchi tano za hifadhi ya wakimbizi zitaungwa mkono katika juhudi zao za kuwaunganisha wakimbizi wa Sudan Kusini katika mifumo ya kitaifa ya utoaji wa huduma za kijamii.

Wakimbizi na jumuiya za wenyeji zitapokea usaidizi wa kuimarisha uthabiti wao kwa kutambua na kubadilisha fursa za kupata riziki.

“Hii ni muhimu sana hasa ukizingatia ufadhili duni wa muda mrefu kwa siku za nyuma ambao umeathiri utoaji wa chakula, ambao unaendelea kusababisha kupunguzwa kwa mgao wa mara kwa mara.”

Pia fedha zitasaidia katika kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia pamoja na kutoa msaada wa afya ya akili na kisaikolojia pia utaongezwa.

Hii inafuatia kuongezeka kwa wasiwasi kwa ripoti za msongo wa mawazo  mwaka jana, haswa miongoni mwa wakimbizi nchini Kenya na Uganda.

Pia imesalia kuwa shida ya watoto, na wakimbizi wawili kati ya watatu wa Sudan Kusini walio chini ya umri wa miaka 18.

UNHCR imessistiza kuwa ufadhili unahitajika kwa ulinzi wa mtoto ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usajili sahihi wa kuzaliwa na kuunganishwa na familia zao.

Watu walioathiriwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini wakiwa katika kambi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda raia mjini Malakal
IOM/Bannon
Watu walioathiriwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini wakiwa katika kambi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda raia mjini Malakal

Watoto wengi ambao waliathiriwa na kufungwa kwa shule wakati wa janga la COVID-19 wanahitaji msaada wa ziada.

Ili kulinda mazingira bora na kupunguza athari za mzozo wa mabadiliko ya tabianchi, UNHCR inaongeza matumizi ya nishati safi na kufanya uwekezaji mwingine unaojali mazingira.

Kwa mujibu wa UNHCR mgogoro wa wakimbizi wa Sudan Kusini unasalia kuwa mkubwa zaidi katika bara la Afrika.

Pia ni mmoja ya migogoro ilyofadhiliwa kidogo zaidi mnamo mwaka 2021 kwa asilimia 21 tu.

Mshikamano wa kimataifa na usaidizi kwa wakimbizi lazima uongezwe hadi Kenya, Uganda, Ethiopia, na Sudan, ambazo zimewakaribisha kwa ukarimu wakimbizi wa Sudan Kusini.