Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tume ya haki za binadamu imeanza ziara Sudan Kusini, Uganda, Kenya na Ethiopia

Pichani  ni nchini Sudan Kusini  ambako wafanyakazi wa ofisi ya haki za binadamu  akichunguza ukiukwaji wa haki za binadamu.
UN Photo/JC McIlwaine
Pichani ni nchini Sudan Kusini ambako wafanyakazi wa ofisi ya haki za binadamu akichunguza ukiukwaji wa haki za binadamu.

Tume ya haki za binadamu imeanza ziara Sudan Kusini, Uganda, Kenya na Ethiopia

Haki za binadamu

Wajumbe wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa  ajili ya Sudan Kusini leo wameanza ziara ya siku kumi katika nchi nne za Afrika ambazo ni Sudan Kusini, Uganda, Kenya na Ethiopia.

Ziara hiyo itakayomalizika 29 Agosti imeanzia leo Sudan Kusini ambako wajumbe wanazuru makambi ya wakimbizi na makazi ya wakimbizi wa ndani nchini humo ikiwemo makazi ya mpango wa Umoja wa Mataifa (UNMISS) ya ulizi wa raia kwa lengo la kukutana na wakazi , viongozi wa kijamii na mashirika ya asasi za kiraia yakiwemo ya wanawake.

Wajumbe watatu wa tume hiyo wanaoshiriki zira hiyo ni mwenyekiti Yasmin Sooka, wajumbe Andrew Clapham na Barney Afako wakiwa Sudan Kusini kwa siku sita hadi Agosti 24 wanatarajia kukutana pia na maafisa wa serikali ikiwemo mawaziri wajumbe wa asasi za kiraia, viongozi wa kidini, jumuiya ya wanadiplomasia, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa UNMISS akiwemo mkuu wa UNMISS David Shearer kujadili hali ya sasa ya haki za binadamu nchini Sudan Kusini. Kabla ya kuondoka Sudan Kusini tume hiyo itakuwa na mkutano na waandishi wa habari Ijumaa ya Agosti 23.

Kisha wajumbe hao watagawanyika kwa ajili ya kuzurua Uganda , Ethiopia na Kenya ambako watakutana na wakimbizi wa Sudan Kusini waliotawanywa hivi karibuni. Nchini Ethiopia wajumbe watafanya mkutano na viongozi wa Muungano wa afrika , IGAD, maafisa wa Umoja wa Mataifa na wajumbe wa jumuiya ya kimataifa.

Baada ya ziara yao katika nchi hizo zote nne wajumbe watawasilisha taarifa ya mdomo ya hali ya haki za binadamu kwa sasa nchini Sudan Kusini katika Baraza la Haki za binadamu Septemba 16 mwaka huu wa 2019, na ripoti ya kina ya maandishi itawasilishwa kwa baraza hilo Machi 2020.