Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 247 zasakwa kunusuru Madagascar, Malawi, Msumbiji na Zimbabwe

Takribani watu milioni 10 wameathiriwa na msururu wa majanga ya tabianchi kwenye ukanda wa Kusini mwa Afrika tangu mwezi Januari hadi Machi mwaka 2923.
©FAO/Fábio de Sousa
Takribani watu milioni 10 wameathiriwa na msururu wa majanga ya tabianchi kwenye ukanda wa Kusini mwa Afrika tangu mwezi Januari hadi Machi mwaka 2923.

Dola milioni 247 zasakwa kunusuru Madagascar, Malawi, Msumbiji na Zimbabwe

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo duniani, FAO hii leo limezindua wito wa dharura wa usaidizi kwa nchi za kusini mwa Afrika zlizokumbwa na msururu wa majanga ya tabianchi tangu mwanzo wa mwaka huu, majanga ambayo yamesambaratisha maisha ya mamilioni ya watu.

Taarifa iliyotolewa na FAO hii leo huko mjini Harare, nchini Zimbabwe imesema ombi hilo la dola milioni 247 ni kwa ajili ya kusaidia watu milioni 2.5 walio hatarini zaidi huko Malawi, Madagascar, Msumbiji na Zambia ambao wanakabiliwa na changamoto zitokanazo na madhara ya majanga mfululizo.

 

FAO inasema kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu wa 2023, kimbunga Freddy, kimbunga chenye nguvu zaidi kuwapi kurekodiwa na kimbunga Cheneso, kilipiga Malawi, Madagascar na Msumbiji. Na wakati huo huo, Zambia inakabiliwa na mvua kubwa haribifu ambazo zimesababisha mafuriko.

 

FAO inasema miundombinu muhimu ya kijamii na kiuchumi, vifaa vya uvuvi, mifumo mamia ya maelfu ya ekari za mazao vimeharibiwa.

 

“Mafuriko yamechochea ongezeko la mienendo ya mifugo kuhamahama kusaka malisho halikadhalika wanyamappri, hali inayoweza kuchochea mlipuko wa magonjwa ya wanyama,” imesema taarifa hiyo ikitanabaisha kuwa takribani watu milioni 10 wameathiriwa kwenye ukanda mzima wa kusini mwa Afrika.

 

Mratibu wa FAO Kanda ya Kusini mwa Afrika Patrice Talla amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema, “hali ya upatikanaji wa chakula na mbinu za wakazi wa kijijini kujipatia kipato vimevurugika. Hatua ya haraka ya usaidizi inahitajika ili kuwezesha watu kunyanyuka na kurejea katika uzalishaji wa kilimo.”

 

Fedha hizo zinazoombwa zitaelekezwa kwenye usaidizi wa kilimo, uvuvi, ufugaji, sambamba na kufanya tathmini na uchambuzi wa usaidizi unaoratibika ili kuleta matokeo ya haraka.

 

Kwa mujibu wa FAO, zaidi ya asiliia 70 ya wakazi wa vijijini katika nchi za kusini mwa Afrika wanategema kilimo ili kujipatia kipato.

Unaweza kupata ombi hilo kwa kina hapa.