Bado Malawi inahitaji msaada wa kibinadamu baada ya kimbunga Freddy
Bado Malawi inahitaji msaada wa kibinadamu baada ya kimbunga Freddy
Ikiwa ni mwezi mmoja tangu kimbunga Freddy kupiga wilaya 15 zilizopo kusini mwa nchi ya Malawi na kuathiri maisha ya watu na makazi, jamii hizo bado zinahitaji usaidizi wa kibinadamu ili ziweze kuendelea na maisha wakati huu wakikabiliana na athari za kimbunga hicho ikiwemo mmomonyoko wa udongo.
Taarifa iliyotolewa leo kutoka Lilongwe nchini Malawi na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA imesema tangu tarehe 12 Machi watu 230,000 wamefikiwa na kupatiwa misaada mbalimbali ikiwemo maji safi na kujisafi, chakula, huduma za afya, afya ya uzazi na huduma nyingine za dharura.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Malawi Rebecca Adda-Dontoh amesema kwa wiki kadhaa ameona magari yaliyobeba bidhaa za misaada na kushuhudia majirani wakisaidia wenzao na pia mashirika ya Umoja wa Mataifa yakitoa misaada.
“Katika kasaidia jamii zilizo athirika na mafuriko, utoaji wa misaada unaoongozwa na serikali, mashirika 60 ya Umoja wa Mataifa na mashiri amengine yasiyo ya kiserikali yamesaidia kutoa misaada ya kuokoa maisha waliathirika na kimbunga, hata hivyo bado misaada hiyo haitoshi bado mambo mengi yanatakiwa kufanyika.” Amesema Bi. Adda-Dontoh.
Ametaja usaidizi zaidi unahitaji kuanzia kwenye maji safi na kujisafi hususan kipindi hiki nchi hiyo ikikabiliana na mlipuko wa kipindupindu mpaka kwenye elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia.
“Tunahitaji kuhakikisha kuwa wanawake na watoto, wanalindwa dhidi ya udhalilishaji, unyonyaji na unyanyasaji, kutokana na hatari nyingi zinazotokana na mazingira ya sasa baada ya mafuriko.”
Mwakilishi huyo wa UN nchini Malawi amesema kwa muda wa mwezi mmoja wamepokea misaada kutoka kwa wafadhili wa kimataifa wenye thamani ya dola milioni 7.6 na kutoa ombi kwa wafadhili kuongeza mara mbili ufadhili huo ili waweze kutekeleza mambo mengi ambayo wataweza tu kuteleza iwapo watapata ufadhili.
Malawi ni moja ya nchi zilizoko kusini mwa bara la Afrika ambazo zimeathiriwa zaidi ya kimbunga Freddy ilihali nchi hiyo imechangia asilimia 0.04 kwenye uchafuzi wa tabaka la ozoni.
Kimbunga Freddy ambacho mpaka sasa kimesha sababisha vifo vya zaidi ya watu 1000 ni ukumbusho madhubuti wa athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye maisha ya wanadamu.