Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Msumbiji na Malawi hatarini kupata kipindupindu baada ya kimbunga Freddy: UNICEF

Vifaa vya kukabiliana na kipindupindu vimewasili katika kituo cha Dzenza Katikati ya Malawi
© UNICEF
Vifaa vya kukabiliana na kipindupindu vimewasili katika kituo cha Dzenza Katikati ya Malawi

Watoto Msumbiji na Malawi hatarini kupata kipindupindu baada ya kimbunga Freddy: UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF leo limeonya kwamba mamilioni ya watoto wako hatarini kutokana na uwezekano wa ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu nchini Malawi na Msumbiji baada ya kimbunga Freddy, ambacho kimekumba nchi zote mbili kwa mara ya pili katika muda wa chini ya mwezi mmoja.

Shirika hilo limeongeza kuwa uharibifu na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga hicho yameongeza hatari kubwa kwa watoto na familia katika nchi hizo, kudhoofishwa zaidi na mifumo duni ya maji, usafi, afya na vyoo.

Mkurugenzi wa UNICEF wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Mohamed M. Malick Fall amesema "Wakati wa kukabiliwa na mgogoro na machafuko, ni watoto ambao wanakuwa hatarini zaidi. Kimbunga Freddy kimeleta madhara makubwa. Familia nyingi nchini Malawi na Msumbiji zimeshuhudia Maisha yao yakisambaratishwa na kuwaacha vitu kidogo sana huku watoto na wasiojiwezwa wakiwekwa katika hatari kubwa. UNICEF inafanya kazi usiku kucha na mamlaka na washirika wengine ili kukidhi mahitaji ya haraka ya watoto na familia zao."

Mgonjwa anayeugua kipindupindu akitibiwa Tukombo kaskazini mwa Malawi.
© UNICEF
Mgonjwa anayeugua kipindupindu akitibiwa Tukombo kaskazini mwa Malawi.

Hasara iliyosababishwa na kingunga Freddy

Kote nchini Malawi na Msumbiji, mafuriko na uharibifu uliosababishwa na kimbunga umesababisha vifo, uharibifu wa miundombinu na huduma za kijamii na kulazimisha watu kuhama makwao, huku zikikwamisha upatikanaji wa huduma za afya na huduma nyingine za msingi, ambazo kwa hakika zitazidisha milipuko ya kipindupindu ambayo nchi hizo mbili zinakabiliwa nayo.

Hata kabla ya kimbunga hicho, UNICEF inasema Malawi na Msumbiji zilikuwa miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na mlipuko wa kipindupindu ambao mwaka huu pekee umesababisha zaidi ya wagonjwa 68,000 katika nchi 11 za ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Shirika hilo limeendelea kusema kwamba “Msumbiji imekuwa ikikabiliwa na mlipuko wa kipindupindu tangu mwezi Septemba 2022, na kuna wagonjwa waliothibitishwa katika wilaya 35 katika majimbo saba, na kuna uwezekano mkubwa pia yatakuwa yameathirika tena. Kufikia 18 Machi 2023, karibu wagonjwa10,000 walikuwa wameripotiwa, ikiwa ni ripoti ya wagonjwa mara tatu zaidi tangu mapema Februari.”

UNICEF inasema Msumbiji wakati huo huo inakabiliana na migogoro mingi ya kibinadamu inayoshindana, huku watu milioni 2 wakihitaji msaada wa kibinadamu katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, huku juhudi za nchi nzima za chanjo ya polio zinaendelea.

Kimbunga Freddy kimetua Msumbiji kwa mara ya pili na kusababisha mvua kubwa, upepo na mafuriko
© UNICEF/Alfredo Zuniga
Kimbunga Freddy kimetua Msumbiji kwa mara ya pili na kusababisha mvua kubwa, upepo na mafuriko

Kimbunga Freddy kimerejea mara mbili

Kwa mujibu wa UNICEF kimbunga Freddy kimepiga mara mbili nchini Msumbiji, kwanza mwishoni mwa Februari, katikati mwa jimbo la Inhambane la Msumbiji, na tena tarehe 12 Machi, kaskazini zaidi katika mkoa wa Zambezia.

Kikielekea bara, kimbunga hicho kilipiga sana kusini mwa Malawi, na kusababisha uharibifu mkubwa wa barabara, miundombinu, nyumba, biashara, na vituo vya afya, ikiwa ni pamoja na vitengo vya matibabu ya kipindupindu na shule katika maeneo yaliyoathirika.

Kipindupindu hicho tayari kimeua zaidi ya watu 1,660. Ukijumuisha janga hili na msimu unaoendelea wa kila mwaka wa muambo wakati mamilioni ya Wamalawi wanatarajiwa kuwa na uhaba wa chakula, watoto wanateseka zaidi kutokana na mgogoro huu.

Sayari ikiendelea kushika joto, Malawi ina uwezekano wa kukumbwa na hatari mbaya zaidi zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kama vile dhoruba kali na ukame.

Kwa mujibu wa shirika hilo la watoto duniani “Leo hii inakadiriwa kuwa watoto milioni 4.8 wako katika uhitaji wa kibinadamu. Hadi kufikia mwishoni mwa Machi, karibu robo milioni ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kuwa na utapiamlo, huku zaidi ya watoto 62,000 wakitarajiwa kuwa na utapiamlo mkali.”

Kwa vile mtoto aliye na utapiamlo mkali ana uwezekano wa kufa kutokana na kipindupindu mara 11 zaidi ya mtoto mwenye lishe bora, kipindupindu kinaweza kuwa hukumu ya kifo kwa maelfu ya watoto nchini Malawi.limeongeza shirika hilo.

Wagonjwa wa kipindupindu wameongezeka kwa kasi Afrika mwanzoni mwa mwaka 2023
© WHO
Wagonjwa wa kipindupindu wameongezeka kwa kasi Afrika mwanzoni mwa mwaka 2023

Jitihada zinazofanywa na UNICEF

Nchini Malawi na Msumbiji, UNICEF inalenga katika uhamasishaji wa vifaa muhimu vya msingi, kuhakikisha upatikanaji wa chakula na maji salama, kuchagiza masuala ya usafi na vifaa, mahema, vifaa vya matibabu, vyoo vya dharura, elimu na huduma nyingine muhimu na msaada wa kisaikolojia na ulinzi dhidi ya unyanyasaji unaoweza kutokea.

Kwa ushirikiano na waendeshaji wa ndege zisizo na rubani au drone UNICEF inaunga mkono ramani ya anga katika wilaya sita za Malawi ili kutathmini kiwango cha uharibifu na mafuriko katika maeneo ambayo ni magumu kufikiwa na pia kwa juhudi za utafutaji na uokoaji.

UNICEF inatoa wito wa dharura wa ufadhili wa dola milioni 155 ili kukabiliana na athari za mafuriko na kipindupindu kwa watoto na familia katika eneo hilo, na kutoa vifaa vya kuokoa maisha, huduma, na msaada wa kiufundi katika suala la maji, usafi wa mazingira na usafi, afya na huduma za VVU, elimu,  lishe, ulinzi wa mtoto na ulinzi wa kijamii na msaada wa mabadiliko ya tabia za kijamii zilizounganishwa katika sekta zote.

Ili kupunguza athari za mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi kwa watoto katika eneo hilo, UNICEF pia inalenga katika kujenga mifumo ambayo inaweza kushughulikia majanga yajayo.

Bwana Fall amesema “UNICEF inafanya kazi na wabia na jumuiya za mitaa kujenga mifumo thabiti zaidi katika ngazi ya wilaya na jamii ambayo inaweza kuhimili athari zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi. Mfano ni kazi yetu nchini Msumbiji kujenga shule zenye mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaweza kustahimili upepo wa kimbunga. Kimbunga Freddy kilikuwa dhoruba ya kihistoria, lakini, kwa bahati mbaya, kutokana na mabadiliko ya tabianchi, tunajua haitakuwa dhoruba ya mwisho ya kuvunja rekodi ambayo ukanda huu unaweza kukumbana nayo. Hata tunaporudi nyuma kutokana na athari za Freddy, lazima tufanye hivyo kwa majanga yajayo ili kujenga uthabiti katika siku zijazo.