Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tafadhali tushikamane na waathirika wa kimbunga Idai:Wataalam UN

Wavulana wawili wakicheza kwenye maji ya mafuriko kufuatia kimbunga idai kupiga kambi ya wakimbizi ya Tongogara kusini mashariki mwa Zimbabwe
UNHCR/Zinyange Auntony
Wavulana wawili wakicheza kwenye maji ya mafuriko kufuatia kimbunga idai kupiga kambi ya wakimbizi ya Tongogara kusini mashariki mwa Zimbabwe

Tafadhali tushikamane na waathirika wa kimbunga Idai:Wataalam UN

Tabianchi na mazingira

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, hii leo mjini Geneva Uswisi wametoa wito kwa mataifa, mashirika ya kimataifa na sekta binafsi kuonesha mshikamano na nchi za kusini mwa Afrika baada ya kimbinga Idai kuwaua mamia na pia maelfu kubakia bila makazi huku pia kimbunga hicho kikisababisha hasara ya mabilioni ya fedha.

 

Taarifa hiyo iliyochapishwa pia katika tovuti ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR inaeleza kuwa hadi sasa, Idai imesababaisha uharibifu nchini Msumbiji, Zimbabwe na Malawi na kuwaua zaidi ya watu 700 ikiwa bado mamia hawafahamiki waliko. Watu wengine zaidi ya  milioni 3 wameathirika kuanzia tarehe 9 hadi 21 Machi 2019.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa ni Obiora C. Okafor, mtaalamu huru wa haki za binadamu na mshikamano wa kimataifa, Bi Cecilia Jimenez-Damary mjumbe maalumu kuhusu haki za bindamu za wakimbizi wa ndani, Bwana Léo Heller mjumbe maalumu kuhusu haki za binadamu kuhusu maji safi ya kunywa na usafi, Bwana David R Boyd mjumbe maalumu wa haki za binadamu na mazingira, Bwana Saad Alfarargi, mjumbe maalumu katika haki ya maendeleo, Bwana Dainius Pῡras mjumbe maalumu katika haki ya afya ya mwili na akili, Bi Rosa Kornfeld-Matte mtaalamu huru katika kufurahia haki zote za binadamu kwa watu wenye umri mkubwa, Bwana Livingstone Sewanyana mtaalamu huru katika kuhamasisha utaratibu wa kidemkrasia na usawa wa kimataifa.

Watalaamu hao  wanakadiria kuwa kimbunga hicho ni cha gharama zaidi katika eneo la Kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi zikiwemo athari hasi katika kufurahia haki za binadamu.“Pepo kali na mafuruko yaliyotapakaa vimepasua barabara, kuvinja madaraja, nyumba, shule na maeneo ya huduma za afya na pia ardhi kwa ajili ya kilimo.” Wamesema wataalamu hao.

Aidha wamesema ingawa viwango vya maji ya mito viko katika hali sawa lakini mafuriko yanabakia kuwa mabaya na kiasi cha madhara yaliyosababishwa na mafuriko bado hakijafahamika kwa uhakika kwa kuwa bado operesheni za utafutaji na uokozi zinaendelea. Kutokana na uwepo wa maji kidogo ya kunywa, visa vya kipindupindu vimeripotiwa na kua hatari kubwa zaidi ya kutokea milipuko ya magonjwa yanayotokana na maji.

“Ukubwa wa janga hili unatuma ujumbe ulio wazi kuwa mengi zaidi yanatakiwa kufanywa katika jinsi ya kujipanga kukabiliana na majanga, kujiandaa kwa dharura, na pia masuala ya tabianchi. Ushahidi wa kisayansi unaonesha kuwa matukio ya namna hii yatakuwa ya mara kwa mara na mabaya zaidi katika siku za usoni.” wametahatharisha.

Na hapo ndipo wataalamu hao huru ambao hufanya kazi kwa kujitolea na kuchunguza mabo Fulani kuhusu nchi au sehemu iliyopangwa, wakatoa wito kwa mataifa, mashirika ya kimataifa, asasi za kijamii na watu binafsi na makampuni kuonesha mshikamano nan chi zilizoathirika, jamii, familia na pia kwa mtu mmoja mmoja.

“Nchi zilizoathirika zinahitaji msaada ili kuunga mkono jitihada kadhaa ambazo zimeshafanywa na mashirika ya kiraia yakiwemo mashirika ya misaada wakati wa majanga ili kuleta nafuu kwa wale ambao wameathirika na masaibu yaliyosababishwa na kimbunga hiki.” Wamesema wataalamu.