Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula ilizidi kuwa mbaya kote duniani mwaka jana: UN

Mwanamke katika mkoa wa Tanganyika nchini DRC akiwa na watoto wake ambao wanakabiliwa na utapiamlo.
© UNICEF/Olivia Acland
Mwanamke katika mkoa wa Tanganyika nchini DRC akiwa na watoto wake ambao wanakabiliwa na utapiamlo.

Hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula ilizidi kuwa mbaya kote duniani mwaka jana: UN

Amani na Usalama

Kutokana na migogoro, misukosuko ya kiuchumi na majanga ya mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa chakula uliongezeka duniani kote mwaka 2022, huku watu milioni 258 wakihitaji msaada wa dharura wa chakula ikilinganishwa na watu milioni 193 mwaka jana, imetahadharisha ripoti kuhusu mgogoro wa chakula mwaka 2023 iliyozinduliwa leo na mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa.

Hii ni idadi ya juu zaidi tangu kuanzishwa kwa ripoti hiyo miaka saba iliyopita. Mwaka 2021, watu milioni 193 katika nchi na wilaya 53 walikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, kulingana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ya mgogoro wa chakula, ikibainisha kuwa ongezeko hilo unaonyesha kwa kiasi kikubwa tathimini ya ongezeko la idadi ya watu.

Tatizo la kutokuwa na uhakika wa chakula linaongezeka "kwa mwaka wa nne mfululizo na mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa kali ambayo inatishia maisha yao moja kwa moja", wanasisitiza watendaji 17 wa mtandao huu, unaoleta pamoja shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), shirika la umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) , Muungano wa Ulaya, pamoja na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali, ambayo yanajitahidi kupambana na migogoro ya chakula kwa pamoja.

Wamesisitiza kuwa katika hali hii watu katika nchi 7 wako katika hatihati ya baa la njaa.

Kushindwa kusongesha SDGs

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika dibaji ya ripoti hiyo amesema "Zaidi ya robo ya watu bilioni hii leo wanakabiliwa na kiwango kikubwa cha njaa, na wengine wako katika ukingoni mwa njaa. Hili halikubaliki.”

Mwaka 2022, changamoto ya uhaba wa chakula iliongezeka hadi asilimia 22.7, ikilinganishwa na asilimia 21.3 mwaka 2021, lakini bado hali hiyo haikubaliki na ripoti inasisitiza kuwa mwelekeo ni wa kuzorota wa uhaba mkubwa wa chakula ulimwenguni kote.

"Toleo hili la saba la ripoti ya dunia ya mgogoro wa chakula ni shitaka kali la ubinadamu kutokuwa na uwezo wa kupiga hatua katika kumaliza njaa, ambalo ni lengo namba mbili la Maendeleo Endelevu la Umoja wa Mataifa,” ameongeza mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres.

Kulingana na ripoti hiyo, zaidi ya asilimia 40 ya watu wako katika kiwango cha daraja la 3 au zaidi la (IPC) na wanaishi katika nchi tano tu ambazo ni Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ethiopia, majimbo 21 ya Nigeria ikiwemo mji mkuu wa nchi hiyo na Yemen.

Wamama wakitembea katika eneo la mafuriko huko Rann, Borno nchini Nigeria.
© UNOCHA/Yasmina Guerda
Wamama wakitembea katika eneo la mafuriko huko Rann, Borno nchini Nigeria.

Hofu Afghanistan, Burkina Faso, Haiti, Nigeria, Sudan Kusini na Yemen

Watu katika nchi saba walikabiliwa upungufu na njaa , au viwango vya janga la njaa kali daraja la 5 katika wakati fulani wa mwaka  2022.

Zaidi ya nusu ya watu hawa walikuwa Somalia asilimia 57, wakati hali hizi mbaya pia zilitokea Afghanistan, Burkina Faso, Haiti kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo, Nigeria, Sudan Kusini na Yemen.

Takriban watu milioni 35 walikumbwa na njaa kali wiwango vya IPC daraja la 4 katika nchi 39, na zaidi ya nusu yao wako katika nchi nne tu za Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan na Yemen.

Aidha, katika majanga 30 kati ya 42 makubwa ya chakula yaliyochambuliwa katika ripoti hiyo, zaidi ya watoto milioni 35 walio chini ya umri wa miaka mitano walikumbwa na utapiamlo mkali au unyafuzi, ikiwa ni pamoja na watoto milioni 9.2 kutokana na kupungua kabisa kwa uzito ambayo ni aina ya utapiamlo hatari zaidi kwa maisha na jambo ambalo huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vifo vya watoto wachanga.

Vyanzo vikuu wa migogoro ya chakula

"Vita na machafuko vinasalia kuwa kichocheo kikuu cha migogoro ya chakula," limesema shirika la FAO katika muhtasari wa ripoti hiyo, likiongeza kuwa lakini mishtuko ya kiuchumi, inayohusishwa na janga la COVID-19 na athari za vita vya Ukraine, zilielemea zaidi katika baadhi ya nchi mwaka 2022.

Migogoro na ukosefu wa usalama ulikuwa kichocheo muhimu zaidi katika nchi au maeneo 19, ambapo watu milioni 117 walikuwa katika kiwango cha ukosefu wa chakula daraja la 3 au zaidi au sawa.

Makadirio haya ya chini yanaelezewa na ukweli kwamba mshtuko wa kiuchumi umepita migogoro kama kichocheo kikuu cha uhaba mkubwa wa chakula katika nchi tatu ambazo bado zimeathiriwa na migogoro ya muda mrefu ambazo ni Afghanistan, Sudan Kusini na Syria.

Matukio makubwa yanayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi, kama vile ukame wa kihistoria katika Pembe ya Afrika au mafuriko makubwa nchini Pakistani au ukame kusini mwa Afrika, pia ni sababu kuu za kukithiri kwa uhaba huu wa chakul kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Sababu hizo zilikuwa chachu kubwa  ya uhaba mkubwa wa chakula katika nchi 12 ambapo watu milioni 56.8 walikuwa katika kiwango cha IPC ch adaraja la 3 au zaidi au sawa, na zaidi ya mara mbili ya idadi ya watu milioni 23.5 katika nchi nane mwaka 2021.

Duniani kote ripoti imesema  hakuna dalili kwamba mambo haya yatapungua mwaka wa 2023.

Kulingana na Umoja wa Mataifa na washirika wake, mabadiliko ya tabianchi yanatarajiwa kuzidisha hali mbaya ya hewa, uchumi wa kimataifa na wa kitaifa unakabiliwa na matarajio mabaya, wakati migogoro na ukosefu wa usalama huenda vikaendelea.

Mama wa watoto watisa ambao wankabiliana na utapiamlo anapika chakula katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Aden,  nchini Yemen
© UNICEF/Saleh Bin Hayan YPN
Mama wa watoto watisa ambao wankabiliana na utapiamlo anapika chakula katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Aden, nchini Yemen

Wito wa UN

Dunia ikikabiliwa na utabiri huu unaotia wasiwasi, Umoja wa Mataifa umetoa wito wa mabadiliko ya dhana katika kupendelea kinga bora, matarajio bora na ulengaji bora ili kukabiliana na vyanzo vya migogoro ya chakula, badala ya kukabiliana na athari zake zinapotokea.

Kwa mtazamo wa maendeleo, ni muhimu sana kuongeza uwekezaji wa msingi ili kukabiliana na vyanzo vya migogoro ya chakula na utapiamlo kwa watoto.

Katibu Mkuu amehitimisha akisema "Mgogoro huu unahitaji mabadiliko ya kimsingi na ya kimfumo. Ripoti hii inaonyesha wazi kuwa maendeleo yanawezekana. Tuna takwimu na ujuzi wa kujenga ulimwengu unaostahimili, jumuishi zaidi na endelevu zaidi, ambao njaa haina nafasi ikiwa ni pamoja na kupitia mifumo imara ya chakula na uwekezaji mkubwa katika uhakika wa chakula na kuboresha lishe kwa kila mtu, popote anapoishi,"