Chonde chonde G-7 endelezeni nia ya kudumisha uhakika wa chakula duniani: WFP

Chonde chonde G-7 endelezeni nia ya kudumisha uhakika wa chakula duniani: WFP
Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limewataka viongozi wa kundi la nchi saba tajiri zaidi duniani G-7 zitakazokutana siku chache zijazo nchini Japan kuendelea kudumisha ahadi yao ya mwaka 2022 ya kuhakikisha uhakika wa chakula duniani ukizingatia kwamba mwaka huu migogoro mipya ya Sudan, Haiti na Sahelinawatumbukiza watu wengi zaidi katika janga la njaa.
Kwa mujibu wa WFP hivi sasa watu wapatao milioni 345 wanakabiliwa na kiwango cha juu cha kutokuwa na uhakika wa chakula ikiwa ni ongezeko la watu milioni 200 tangu mwanzo mwa mwaka 2020 na watu milioni 43 kati ya hao wako katika hatihati ya baa la njaa.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Cindy McCain. Amesema “Mwaka jana, uongozi wa G7 ulifanikiwa kufikia matokeo ya kuokoa maisha katika vita dhidi ya njaa. Mamilioni ya watu walipata msaada uliohitajika na nchi kama Somalia ziliondolewa kwenye ukingo wa njaa. Kwa bahati mbaya, mzozo wa chakula duniani haujaisha. Na hali kama vile Sudan na Haiti zinaongeza mafuta kwenye moto.”
Mzozo wa Sudan, Sahel na Haiti chachu ya njaa zaidi
Mapigano nchini Sudan yamesababisha mamia kwa maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kusababisha mamilioni ya watu kukabiliwa na njaa.
WFP inakadiria kuwa kati ya watu milioni 2 na 2.5 wa ziada watakuwa na uhaba wa chakula katika miezi ijayo kama matokeo ya moja kwa moja ya mapigano yanayoendelea, na kufikisha jumla ya watu milioni 19 nchini humo wanaokabiliwa na njaa.
Nchini Haiti WFP inasema , njaa inazidi kushika kasi huku ukosefu wa usalama, ghasia na matatizo ya kiuchumi vinazidi kuwafanya Wahaiti wasio na uhakika wa chakula kuingia kwenye mgogoro.
Rekodi kubwa ya watu milioni 4.9 nchini humo wanakadiriwa kukabiliwa na njaa kali, karibu asilimia 45 ya watu wote nchini humo.
Na vile vile, katika eneo la Sahel barani Afrika, milipuko mipya ya ghasia katika maeneo kama vile Burkina Faso inasababisha njaa miongoni mwa watu wanaokimbia pamoja na wale ambao maisha na uwezo wao wa kuishi vimeathirika na migogoro.
Wito wa WFP kwa nchi za G-7
WFP inatoa wito kwa nchi za G7, ambazo zote ziliongeza ufadhili mwaka 2022, kuendelea kufadhili msaada wa chakula kwa mamia ya mamilioni ya watu walioathiriwa na mgogoro wa chakula duniani na mamilioni ya watu wapya waliotumbukia kwenye njaa tangu mwaka jana.
Pia inataka uungwaji mkono wa kisiasa kwa hatua nyingine ambazo zitasaidia kupunguza mgogoro huo wa njaa.
Hatua hizo ni Pamoja na kufanya kazi kwa ajili ya kuendeleza Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, kuhakikisha ugavi wa kutosha wa mbolea na programu zinazosaidia kuongeza uzalishaji wa wakulima wadogo.
Maombi ya muda mrefu ya WFP yanahusu hitaji la kufanya idadi ya watu walio katika mazingira hatarishi kuwa imara zaidi.
Shirika hilo linazitaka nchi hizo kuangazia upya ulinzi wa kijamii kwa jamii zilizo hatarini na kuhakikisha kila mtoto anayehitaji anapokea mlo bora shuleni kila siku.
"Tunahitaji kuongeza usaidizi, haswa linapokuja suala la kufanya mifumo yetu ya chakula iwe thabiti," amesema Bi. McCain na kuongeza kuwa "Ikiwa tunaweza kuandaa jamii zilizo hatarini kushughulikia majanga ya mabadiliko ya tabianchi yajayo, hazitahitaji msaada wa dharura wakati ujao kutakapokuwa na ukame au mafuriko."
Niger iliathirika vibaya mwaka jana
WFP inasema mwaka 2022, Niger ilikabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa kutokuwa na uhakika wa chakula katika kipindi cha muongo mmoja.
Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni maeneo ambayo WFP ilikuwa na programu za kujenga mnepo.
Matokeo yake, idadi kubwa saw ana asilimia 80 ya vijiji vilivyo katika maeneo yaliyoathirika sana havikuhitaji msaada wa kibinadamu.
Katika mkutano wa kilele wa G7 nchini Ujerumani mwaka jana, viongozi waliapa "kufanya juhudi zote za ili kuongeza uhakika wa chakula na lishe duniani na kuwalinda walio hatarini zaidi.”
Pia walijitolea kuimarisha mnepo wa muda mrefu wa mifumo ya kilimo na chakula ili nchi maskini zisiwe hatarini zaidi katika siku zijazo.
Migogoro inasalia kuwa mojawapo ya vichocheo vikuu vya njaa duniani. Matukio nchini Sudan ni mfano wa hivi karibuni zaidi wa jinsi uhaba wa chakula unavyoongezeka wakati bunduki zinarindima.
WFP inazitaka nchi za G7 "kufanyia kazi suluhu za kisiasa kwa migogoro ya muda mrefu kwani migogoro ndio chanzo kikuu cha njaa."