Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu milioni 820 wanakabiliwa na njaa kote duniani - SOFI

Ripoti ya hali ya uhakika wa chakula na lishe duniani 2019.
Jarada la Ripoti
Ripoti ya hali ya uhakika wa chakula na lishe duniani 2019.

Zaidi ya watu milioni 820 wanakabiliwa na njaa kote duniani - SOFI

Ukuaji wa Kiuchumi

Baada ya karibu muongo mmoja wa hatua kubwa , hivi sasa idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa inaongezeka taratibu kwa miaka mitatu iliyopita huku mtu 1 kati ya 9 kote duniani anakabiliwa na njaa hivi leo imesema ripoti ya Umoja wa Mataifa inayotathimini “hali ya uhakika wa chakula na lishe 2019 " ikipatiwa jina kwa kifupi, SOFI.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na kutolewa leo na mashirika matano ya Umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo FAO, la kuhudumia Watoto UNICEF, la mpango wa chakula WFP, la afya WHO na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD inasema zaidi ya watu milioni 820 wako katika hali ya njaa na kwamba “ukweli huu unadhihirisha changamoto kubwa katika kufikia lengo namba moja la maendeleo endelevu la “kutokomeza njaa ifikapo mwaka 2030.

Ripotoi hiyo imezinduliwa kandoni mwa jukwaa la ngazi ya juu la kisisa (HPLF) linaloendelea jijini New York Marekani kwa ajili ya kutathimini hatua zilizopigwa nan chi wanachama katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu SDGs likiwemo lengo la kutokomeza njaa.

Hali ilivyo kikanda

Kwa mujibu wa ripoti ya SOFI njaa imeongezeka takriban asilimia 20 katika ukanda wa afrika eneo ambalo pia lina kiwango kikubwa cha watoto wasio na lishe bora ambapo utapiamlo unaathiri asilimia 11 ya watu wote.

Ripoti pia imesema ingawa kiwango cha njaa katika ukanda wa Amerika Kusini na Caribe kiko chini ya asilimia 7, taratibu kinaongezeka , na barani Asia lishe duni inaathiri asilimia 11 ya watu wote japokuwa Kusini mwa asia kulishuhudiwa hatua zilizopigwa katika miaka mitano iliyopita.

Wakuu wa mashirika hayo matano kwa pamoja wamesema “Hatua zetu kukabiliana na mwenendo huu wenye athari kubwa ni lazima ziwe  madhubuti sio tu kwa kiwango bali pia katika ushirikiano wa sekta mbalimbali”.

Hapa ni kwenye moja ya soko nchini Thailand, wadudu wakiuzwa kama kitoweo.
P.B. Durst
Hapa ni kwenye moja ya soko nchini Thailand, wadudu wakiuzwa kama kitoweo.

Wamesema njaa inaongezeka katika nchi nyingi ambako ukuaji wa uchumi unasuasua hususani katika nchi za kipato cha kati na zile ambazo zinategemea sana biashara ya kimataifa kama chanzo cha pato.

Ripoti hiyo ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa pia imebaini kwamba pengo la kipato linaongezeka katika nchi nyingi ambako njaa inaongezeka pia na kufanya hali kuwa mbaya zaidi kwa masikini, wasiojiweza au makundi yanayotengwa  kuweza kukabiliana na mdororo wa uchumi.

Viongozi hao wamesisitiza kuwa “ni lazima tuchagize mbinu za kuwasaidia masikini na mabadiliko ya mfumo jumuishi unaojikita katika maslahi ya wat una kuziweka jamii katika kitovu cha kupunguza hali tete ya kiuchumi na kujiweka tena katika msitari wa kutokomeza njaa, kutokuwepo uhakika wa chakula na aina zote za utapiamlo.”

Kutokuwepo uhakika wa chakula

Ripoti ya mwaka huu imemulika athari za kutokuwepo kwa uhakika wa chakula zaidi ya njaa na kwa mara ya kwanza imeweka  lengo dogo namba 2.1  kwa ajili ya kufuatilia lengo la njaa la SDGs  ambalo linaangalia hali ya wastani au mbaya zaidi ya kutokuwepo na uhakika wa chakula ambayo inaonyesha kwamba asilimia 17.2 ya watu wote duniani sawa na watu bilioni 1.3 walikosa fursa ya kupata chakula cha kutosha na chenye lishe bora, hata kama hawakabiliwi na njaa moja kwa moja wako katika hatari ya kukabiliwa na mifumo mbalimbali ya utapiamlo na afya duni..”

Uzito mdogo bado ni changamoto kubwa

Shirika la chakula duniani linasambaza mgao wa chakula kwa watu walio na mahitaji nchini Yemen.
WFP/Annabel Symington
Shirika la chakula duniani linasambaza mgao wa chakula kwa watu walio na mahitaji nchini Yemen.

Ikiwamulika watoto ripoti hiyo inasema tangu mwaka 2012 hakuna hatua zozote zilizopigwa katika kupunguza kiwango cha  wanaozaliwa na uzito mdogo. Pia kuhusu suala la watoto kudumaa ripoti imesema ingawa katika miaka sita iliyopita idadi ya watoto wanaoathirika imepungua kwa asilimia 10 kimataifa lakini kasi yake ni ndigo kuweza kufikia lengo mwaka 2030 la kupunguza kwa nusu idadi ya watoto wanaodumaa.

Zaidi ya hayo ripoti ya SOFi imetaja kuwa uzito wa kupindukia na utipwatipwavinaendelea kuongezeka katika kanda zote , hususan miongoni mwa watoto wa umri wa kuwepo shuleni na watu wazima.

 Kutokuwepo usawa katika kipato kunaongeza uwezekano wa kutokuwa na uhakika wa chakula- SOFI

Nini kifanyike

Ili kuhakikisha uhakika wa chakula na lishe ripoti hiyo ya 2019 inasisitiza umuhimu wa kuwa na será bora za kiuchumi na kijamii kukabiliana na athari za mzunguko wa matatizo ya kiuchumi kama yatajitokeza huku wakiepuka kupunguza huduma muhimu. Imesisitiza kuwa kutokuwepo kwa uwiano wa ufufuaji wa uchumi “kuna athiri juhudi za kukomesha njaa na utapiamlo, wakati njaa inaongezeka katika nchi nyingi ambako uchumi umeshuka hasa katika nchi za kipato cha kati.”

Ripoti imehitimisha kwa muongozo wa sera zipi za suluhu ya muda mfupi na muda mrefu lazima zichukuliwe ili kuhakikisha kuna uhakika wa chakula na lishe wakati wa mdororo wa kiuchumi . Mfano kujumuisha hofo za uhakika wa chakula na lishe katika juhudi za kupunguza umasikini na kujikita walio masikini na kuleta mabadiliko jumuishi.