Skip to main content

Kongamano la 11 la mijini duniani limeng’oa nanga Katowice, Poland:UNHABITAT

Washiriki katika kongamano la miji linalofanyika Katowice Poland
UN Habitat
Washiriki katika kongamano la miji linalofanyika Katowice Poland

Kongamano la 11 la mijini duniani limeng’oa nanga Katowice, Poland:UNHABITAT

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kikao cha kumi na moja cha Kongamano la kimataifa la miji endeleu kimefunguliwa rasmi leo Katowice, Poland kwa wito wa kuongeza juhudi maradufu ili kukabiliana na changamoto zinazoletwa mijini na janga la COVID-19, dharura ya mabadiliko ya tabianchi na migogoro.

Jukwaa la miji duniani, ambalo hufanyika kila mwaka likiandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa makazi UN-HABITAT, mwaka huu linafanyika katika wakati muhimu kwa maendeleo ya miji. Shirika hilo limesema huku kukiwa na miaka minane tu iliyosalia kuweza kufikia Lengo la 11 la maendeleo endelevu la kufanya miji na makazi ya watu kuwa jumuishi, salama, thabiti na endelevu, maeneo ya mijini na wakaazi kote ulimwenguni wanakabiliwa na shinikizo kubwa.

UN-HABITAT imeongeza kuwa idadi ya watu watakaokuwa wanaishi mijini inatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 56 mwaka 2021 hadi asilimia 68 ifikapo mwaka 2050 ikiwa ni ongezeko la watu bilioni 2.2 zaidi wengi wakiwa ni barani Afrika na Mashariki ya Kati.

Lazima tuongeze juhudi mara mbili

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo mkurugenzi mtendaji wa UN-HABITAT Maimunah Mohd Sharif amesema "Wakati hali ya sasa bila shaka ni gumu sana, lazima tudumishe umakini wetu na kuongeza juhudi zetu mara mbili katika maendeleo endelevu. Maudhui ya kikao cha mwaka huu (WUF11), kubadilisha miji yetu kwa mustakabali bora wa mjini, ni muafaka kabisa. Tunahitaji haraka masuluhu bunifu kwa maeneo ya mijini ili kukabiliana na majanga matatu ambayo ni COVID, mabadiliko ya tabianchi na migogoro, ambayo yana athari mbaya kwa miji, na kuwaacha watu na maeneo yao nyuma,"

Ufunguzi wa kongamano la miji Katowice Poland
UN Habitat
Ufunguzi wa kongamano la miji Katowice Poland

Ameongeza kuwa “Lakini mustakabali bora bado unawezekana. Tunajua jinsi ya kufika huko. Serikali na miji tayari ina ramani ya barabara ya kuelekea huko ambayo ni malengo ya maendeleo endelevu, ajenda mpya ya miji, na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi. Sasa tunahitaji hatua za kweli kutekeleza ahadi hizi, na miji lazima ijumuishe mkataba mpya wa kijamii wenye mapato ya msingi kwa wote, bima ya afya na nyumba za gharama nafuu."

Miji ni kitovu cha ajenda ya 2030

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa video kwenye kongamano hilo amesema miji ni kitovu cha takriban kila changamoto tunayokabiliana nayo na ni muhimu katika kujenga mustakabali unaojumuishi zaidi, endelevu na thabiti. “Miji imekuwa mstari wa mbele wakayti wa janga la COVID-19.

Tunapotarajia kujikwamua na janga hili, kukuza miundombinu na huduma za mijini zilizo jumuishi zaidi, zinazozingatia jinsia itakuwa muhimu ili kuwapa watu wote hasa vijana, wanawake na wasichana fursa ya kupata maisha bora ya baadaye.”

Guterres ameongeza kuwa ahadi ya ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu ya kutomwacha mtu yeyote nyuma inategemea vitendo katika ngazi ya ndani ya serikali na inategemea vitendo ndani ya miji. Miji inazalisha zaidi ya asilimia 80 ya Pato la Taifa la kimataifa - na asilimia 70 ya uzalishaji wa gesi chafuzi. Amesema miji “Lazima iwe viongozi wa hatua za mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha lengo la kusalia na juzi joto 1.5 linafikiwa. Miji zaidi na zaidi ulimwenguni inajitolea kuhakilisha hakuna uzalishaji hewa ukaa ifikapo mwaka 2050 au kabla. Kadiri tunavyotafsiri ahadi hizi kwa vitendo madhubuti, ndivyo tutakavyofikia ukuaji unaozingatia mazingira, afya bora na usawa zaidi.”

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema miji haiwezi kutimiza hayo peke yake. “Inahitaji usaidizi ulioratibiwa zaidi kutoka ngazi zote za serikali, ushirikiano imara na sekta binafsi na jumuiya ya kiraia, na nafasi kubwa ya fedha na sera kuleta suluhisho za kiwango kinachohitajika.”

Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa umejitolea kikamilifu kufanya kazi na miji ili kuunganisha wenyeji na ulimwengu na kufikia miji inayojali mazingira, yenye haki na yenye afya. Amehitimisha ujumbe wake akisema kwamba “Kwa ajenda mpya ya miji, muongo wa utekelezaji kwa malengo ya maendeleo endelevu na muungano wa maeneo ya ndani ya nchi wa mwaka 2030 tunayo ramani ya maendeleo. Hebu tutumie uwezo wa kuleta mabadiliko ya ukuaji wa miji na kujenga mustakabali endelevu zaidi, thabiti, na jumuishi kwa wote.”

Miji kama mji mkuu wa Korea Kusini Seoul ni watumiaji wakubwa wa nishati
Unsplash/Ethan Brooke
Miji kama mji mkuu wa Korea Kusini Seoul ni watumiaji wakubwa wa nishati

Kwa nini Katowice

Kongamano hilo lililoanza jana Juni 26 litaendelea hadi Juni 30 huko Katowice, Poland na limeandaliwa kwa pamoja na Serikali ya Poland na jiji la Katowice.

Katowice ilichaguliwa kwa kongamano hilo la kwanza la kufanyika Ulaya Mashariki kwa sehemu kubwa ni kwa sababu ya mafanikio yake ya kuondoka kuwa mji kitovu cha viwanda vya makaa ya mawe na chuma hadi kuwa jiji linalojikita na teknolojia, utamaduni na matukio. Kongamano hili ni kubwa zaidi la mijini duniani kufikia sasa.

Kwa mara ya kwanza, litakuwa tukio la mseto kamili, likifanyika ana kwa ana na mtandaoni ambapo karibu watu 23,000 wameshajisajili kuhuduria. Wengi, hata hivyo, watahudhuria ana kwa ana na wanaweza kuchagua kutoka kwenye jumla ya matukio 451 yanayotarajiwa kufanyika kuanzia mijadala , kwenye meza ndogo za duara hadi vikao maalum na mijadala.

Vikao vya ufunguzi na kufunga kongamano hilo vyote vinafanyika katika ukumbi wa Spodek Arena, mojawapo ya viwanja vikubwa zaidi vya ndani nchini nchini Poland. Huu utakuwa mkutano mkubwa wa kwanza wa kimataifa kuandaliwa tangu kuanza kwa janga la COVID-19.

Zaidi ya watu 16,000 wanaotarajiwa kushiriki ana kwa ana katika Kituo cha Kimataifa cha mikutano cha Katowice, kilichojengwa kwenye eneo la mgodi wa zamani wa makaa ya mawe.

Watakaohudhuria ni pamoja na zaidi ya mawaziri na manaibu waziri 50 wa serikali mbalimbali na zaidi ya maafisa 800 wa serikali na wawakilishi.

Pia kutakuwa na wasemaji zaidi ya 400 katika hafla kadhaa zinazojadili na kubuni sera na suluhisho bunifu kwa ajili ya changamoto za mijini. Siku tano za WUF11 zitahitimishwa kwa kutangazwa hatua za Katowice ambapo wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na wadau wa ajenda mpya ya miji ambayo ni ramani ya maendeleo ya miji iliyopitishwa mwaka 2016 huko Quito, wataeleza dhamira yao na mipango ya kusaidia ukuaji wa miji endelevu.