Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Baraza Kuu ataja vipaumbele vyake huku akisisitiza matumaini

Rais wa Baraza Kuu la UN Abdullah Shahid akihutubia Baraza Kuu kuhusu vipaumbele vyake kwa ng'we ya pili ya mkutano wa 76
UN/Eskinder Debebe
Rais wa Baraza Kuu la UN Abdullah Shahid akihutubia Baraza Kuu kuhusu vipaumbele vyake kwa ng'we ya pili ya mkutano wa 76

Rais wa Baraza Kuu ataja vipaumbele vyake huku akisisitiza matumaini

Masuala ya UM

Huku janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 likiendelea kusambaa maeneo mbalimbali duniani, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid leo wakati akitoa hotuba ya vipaumbele vyake, amesisitiza umuhimu wa mshikamano na matumaini.

 

Vipaumbele hivyo ni mambo ambayo atayapatia msisitizo wakati wa ng’we ya pili ya mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayoingia mwezi huu wa Januari baada ya mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Bwana Shahid amewaambia nchi wanachama kuwa “lazima tuthamini utu wetu wa pamoja wa kibinadamu na kujilinda dhidi ya vichocheo vya mizozo, iwapo dunia inataka kukabiliana na changamoto kama vile janga la Corona, kuenea kwa nyuklia, ugaidi na mizozo duniani.”

Amesihi jamii ya kimataifa iazimie tena katika misingi ya amani iliyowekwa bayana katika Chata ya Umoja wa Mataifa, na kufanya kazi kwa misingi ya kirafiki ili kushughulikia changamoto zinazokabili dunia.

Akitaja vipaumbele vyake vitano katika kipindi chake cha sasa cha urais wa matumaini, Bwana Shahid amesisitiza pia umuhimu wa matumaini, akisema “kulinda matumaini na kuachana na ukosefu wa matumaini akisema, “ukosefu wa matumaini ni mwelekeo wa kutokuchukua hatua.

Iwapo tutakubali kuchukua njia hiyo tutatwama kwenye kuridhika na hali ilivyo, na kuamini kuwa chochote tufanyacho hakina maana na hivyo tusubiri kisichoepukika.” 

Kundi la kwanza la vijana waliojiunga na Programu ya HOPE ya Rais wa Baraza Kuu la UN ya kukuza wanadiplomasia vijana
Office of the PGA/UNITAR
Kundi la kwanza la vijana waliojiunga na Programu ya HOPE ya Rais wa Baraza Kuu la UN ya kukuza wanadiplomasia vijana

Amesihi Jamii ya kimataifa kuazimia tena pia kwenye suala la uwiano wa chanjo kama njia pekee ya kujikwamua vyema kutoka katika janga la Corona, akitoa wito wa uzalishaji na usambazaji wa haraka wa chanjo na kuondoa vikwazo katika kuzisambaza.

Rais huyo wa Baraza Kuu ambaye azimio lake la mwaka mpya ni kampeni ya uwiano kwenye mgao wa chanjo, anaungwa mkono na mataifa 120 wanachama wa Umoja wa Mataifa na tarehe 25 mwezi ujao wa Februari atakuwa na mkutano wa ngazi ya juu wa kuhamaisha utoaji wa  chanjo duniani kote.

Bwana Shahid amesema kuwa jamii ambazo zimeathirika zaidi na Corona mara nyingi ni zile zilizoko kwenye nchi zinazoendelea, hazina bahari na zile za visiwa vidogo ambazo ni pamoja na taifa lake la Maldives.

Ametoa wito kwa mkakati wa kiuchumi ambao unaendana na vipaumbele vya sasa vya dunia vya kimazingira na ulinzi wa maliasili, akigusia pia kikao cha ngazi ya juu atakachoandaa cha kujikwamua kutoka coronavirus">COVID-19 kupitia utalii, mkutano uliopangwa kufanyika mwezi Mei.

Wakati akizungumzia kuhusu mahitaji ya sayari ya dunia, Rais Shahid ameonya hatari inaweza isiwe dhahiri hivi sasa lakini “tuko kwenye mwelekeo wa kutumbukia kwenye hatari.”

“Tuna wajibu wa kuchukua hatua. Maldivves ni moja ya nchi za visivwa vidogo ambavyo viko hatarini kuzama iwapo kiwango cha maji ya bahari kitaendelea kuongezeka,” amesema Bwana Shahid.

Rais huyo wa Baraza Kuu amezungumzia pia Tonga akisema mlipuko wa volcano na mawimbi ya tsunami yaliyofuatia tarehe 15 mwezi huu wa Januari ni mfano wa majanga ambayo nchi za visiwa vidogo hukumbana nayo kila wakati.

Ameisihi jamii ya kimataifa iungane na kuipatia Tonga msaada unaohitajika wakati huo huo akituma salamu za rambirambi na pole kwa wafiwa na majeruhi.

Katika hotuba yake pia amegusia masuala ya usawa wa jinsia na umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu.

Amepongeza pia programu yake aliyozindua ya vijana wanaofanya kazi sambamba na ofisi yake aliyoipatia jina HOPE ikimaanisha Kuchota fursa za kuendeleza na kuwezesha vijana.