Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Programu ya kuleta vijana kufanya kazi na Rais wa Baraza Kuu yazinduliwa

Pichani kati ni Paul Siniga, balozi kijana wa SDGs na mchechemuzi wa kampeni ya He4She akiwa kwenye picha na wanafunzi wa kike.
UN Tanzania
Pichani kati ni Paul Siniga, balozi kijana wa SDGs na mchechemuzi wa kampeni ya He4She akiwa kwenye picha na wanafunzi wa kike.

Programu ya kuleta vijana kufanya kazi na Rais wa Baraza Kuu yazinduliwa

Masuala ya UM

Hatimaye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid amezindua mpango wake wa mafunzo kwa vitendo ambao unalenga kujenga uwezo wa chombo hicho kwa kupatia fursa vijana wanadiplomasia kwa kiingereza Harnessing Opportunities for Promoting Empowerment, HOPE.

Uzinduzi umefanyika hii leo jijini New York, Marekani ambapo taarifa iliyotolewa na ofisi ya Bwana Shahid imetaka nchi wanachama kuteua vijana watakaoshiriki programu hiyo ambapo tarehe ya mwisho ya kupokea majina hayo ni tarehe 30 mwezi huu wa Novemba mwaka 2021.

Programu hiyo itachukuwa wanadiplomasia 8 vijana kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zisizo na uwakilishi wa kutosha kwenye chombo hicho, mathalani zile maskini, LDCs, zisizo na bandari, LLDCs, na zile za visiwa vidogo SIDS ambapo taarifa imemnukuu Rais Shahid akisema “programu hii inalenga kufungua milango ya kuwawezesha kutambua kile Umoja wa Mataifa unafanya na ni mradi muhimu wa Urais wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wenye lengo la kuleta matumaini, jambo ambalo ninalo moyoni mwangu.”

Je watachaguliwa vipi?

Taarifa imesema nchi wanachama zinakaribishwa kuteua kijana mmoja ambapo jopo la wataalamu litateua kwa kuzingatia eneo la kijiografia na jinsia na kwamba gharama zote zitalipwa na mfuko wa programu wa nchi wanachama.
Mwisho wa kupokea majina ni tarehe 30 mwezi Novemba na watakaoteuliwa wanatakiwa kuwepo New York Marekani mapema mwezi Januari mwaka 2022.

Bwana Shahid amesema ana imani kubwa katika kushirikisha vijana kwenye ngazi zote za kuchukua uamuzi na kwamba uwekezaji katika uhusiano wa kimataifa kwa siku za usoni “ni lazima kuwekeza kwa vijana na kuwasogeza karibu na kazi za Umoja wa Mataifa.”

Programu imeandaliwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mafunzo na Utafiti, UNITAR na vijana watakaoteuliwa watashikishwa katka ofisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa ikiwemo ya Rais wa Baraza Kuu.