Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa volcano ya Tonga: Takribani watu watatu wamefariki dunia, wengine hawajulikani waliko

Picha ya visiwa vya Tonga ambako vumbi zito lilianguko kutokana na mlipuko wa Volcano uliotokea katika bahari ya Pasifiki
New Zealand Defence Force
Picha ya visiwa vya Tonga ambako vumbi zito lilianguko kutokana na mlipuko wa Volcano uliotokea katika bahari ya Pasifiki

Mlipuko wa volcano ya Tonga: Takribani watu watatu wamefariki dunia, wengine hawajulikani waliko

Tabianchi na mazingira

Takriban watu watatu wamefariki dunia nchini Tonga kufuatia mlipuko mkubwa wa volkano na wimbi la Tsunami lililotokea mwishoni mwa wiki. Nyumba na majengo mengine kote kwenye visiwa yamepata uharibifu mkubwa.

Visiwa vilifunikwa na majivu, nyumba kadhaa ziliharibiwa

Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Tonga kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne, watu watatu waliofariki ni raia wa Uingereza mmoja na wawili wa Tonga.


Shirika la Afya Duniani la Umoja wa Mataifa, WHO, limeripoti kuwa watu wengi bado hawajulikani walipo, huku takriban watu 90 wakielekea katika maeneo salama katika vituo vya uokoaji katika kisiwa cha Eua, na wengine wengi kukimbilia katika makazi ya marafiki na familia.


Katika kisiwa kikuu cha Tongatapu, karibu nyumba 100 zimeharibiwa, na 50 zimeharibiwa kabisa, kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, ambayo iliwapa taarifa waandishi wa habari mjini Geneva siku ya Jumanne.

Picha ya visiwa vya Tonga ambako vumbi zito lilianguko kutokana na mlipuko wa Volcano uliotokea katika bahari ya Pasifiki
New Zealand Defence Force
Picha ya visiwa vya Tonga ambako vumbi zito lilianguko kutokana na mlipuko wa Volcano uliotokea katika bahari ya Pasifiki


OCHA imesema kuwa bado iko katika harakati za kukusanya taarifa kuhusu ukubwa wa uharibifu, na haijawezekana kuwasiliana na visiwa vyovyote vya Ha'apai et Vava'u.


Visiwa vya Mango na Fonoi, ambavyo ni sehemu ya mlolongo wa visiwa vidogovidogo vya Ha'apai, ni sababu ya wasiwasi, amesema Msemaji wa OCHA Jens Laerke, huku ndege za uchunguzi zikionesha uharibifu mkubwa wa majengo, na picha kutoka Kituo cha Satelaiti cha Umoja wa Mataifa, UNOSAT zinaonesha kuwa kwenye kisiwa kidogo cha Nomuka, mojawapo ya vilivyo karibu zaidi na volcano ya Hunga Tonga Hunga Ha'apai, visiwa 41 kati ya 104 vinavyoonekana vimeharibiwa, na karibu vyote vimefunikwa na majivu, ingawa Kituo kinabainisha kuwa tathmini hii inabakia kuthibitishwa na timu zilizo katika maeneo.


Msemaji wa WHO Christian Lindmeier, amewaambia waandishi wa habari Jumanne hii kwamba Tongatapu imefunikwa na vumbi na majivu ya volkano karibu sentimita mbili, jambo linaloibua wasiwasi wa hewa, maji na uchafuzi wa chakula.


Kuna habari njema, ameongeza akisema, “vituo vyote vya afya katika kisiwa kikuu vinafanya kazi kikamilifu, na shughuli za kusafisha tayari zimeanza.”


Mlipuko mkubwa zaidi katika miongo mitatu


Mlipuko huu  wa volkano ulikuwa mkubwa zaidi kurekodiwa katika miaka thelathini. Wingu kubwa lililopanda juu angali katika umbo la uyoga  lenye urefu wa kilomita 20 la moshi na majivu lilifuatwa na tsunami, na mlipuko huo ulisikika hadi Australia na New Zealand, na kusababisha maonyo ya tsunami kote katika ukanda wa bahari ya Pasifiki.


Mawimbi ya urefu wa mita 1.2 yalipiga mji mkuu wa Tonga, Nuku’alofa, ambao wakazi wake walikimbilia maeneo ya miinuko, na kuacha nyumba zilizofurika, huku mawe na majivu yakinyesha kutoka angani.

Mlipuko mkubwa wa volkano uliotokea Hunga Tonga-Hunga Ha'apai katika bahari ya Pacifiki karibu na Tonga tarehe 15 Januari 2022.
©UNICEF/NOAA
Mlipuko mkubwa wa volkano uliotokea Hunga Tonga-Hunga Ha'apai katika bahari ya Pacifiki karibu na Tonga tarehe 15 Januari 2022.

 

WHO inaripoti kwamba Serikali ya Tonga ilichukua hatua za haraka  na kupeleka meli ya kivita kwenye visiwa vya Ha’api, ikiwa na timu ya Msaada wa Dharura ya Tonga iliyofunzwa na WHO, tayari kuwasaidia waliojeruhiwa.


Serikali inawashauri wakazi wa Tonga kukaa ndani, kuvaa barakoa iwapo itabidi watoke nje, na kunywa maji ya chupa ili kuepusha hatari za kiafya zinazotokana na majivu yaliyoanguka.


Nchi majirani wa Tonga kama Australia na New Zealand, pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau, wamekuwa wakifuatilia kwa karibu hali ilivyo na inavyoendelea huku wakitoa misaada inayohitajika na tathimini ya ujumla ya hali ikisubiriwa.