Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shahid akabidhiwa ‘kijti’ cha UNGA76, kuitisha kikao maalum kuhusu uwiano wa chanjo

Volkan Bozkir, (kulia) Rais wa UNGA75akikabidha rungu la kuongozea mkutano kwa Abdulla shahid, Rais wa UNGA76
UN / Evan Schneider
Volkan Bozkir, (kulia) Rais wa UNGA75akikabidha rungu la kuongozea mkutano kwa Abdulla shahid, Rais wa UNGA76

Shahid akabidhiwa ‘kijti’ cha UNGA76, kuitisha kikao maalum kuhusu uwiano wa chanjo

Masuala ya UM

Abdulla Shahid amekula kiapo hii leo kuwa Rais wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuashiria kuanza kwa mkutano wa 76 wa Baraza hilo.

 

Akila kiapo kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani  Bwana Shahid amesema, “naapa kwa dhati kuwa nitakuwa mkweli katika kutekeleza majukumu yangu na kutekeleza kazi zangu za Urais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa uaminifu, utashi na uadilifu.”

Kisha Rais huyo alikabidhiwa rungu la kuongoza Baraza kutoka kwa mtangulizi wake Rais wa mkutano wa 75 Volkan Bozkir na ndipo mkutano wa 76 ukaanza rasmi.

Katika hotuba yake Bwana Shahid kutoka Maldives ameeleza bayana kuwa kipindi chake cha mwaka mmoja wa urais wa chombo hicho cha Umoja wa Mataifa chenye wanachama 193 kitakuwa cha matumaini ya kukwamuka kutoka janga la ugonjwa wa Corona au coronavirus">COVID-19, kujenga kwa uendelevu, kushughulikia mahitaji ya sayari dunia, kuheshimu haki za kila mtu na zaidi ya yote kuimarisha Umoja wa Mataifa.

“Kuhusu kukwamuka kutoka COVID-19, kupatia chanjo dunia nzima itakuwa ndio kipaumbele changu. Lazima tuzibe pengo la utoaji wa chanjo,” amesema Bwana Shahid.
Ameongeza kuwa ataitisha mjadala wa wazi wa ngazi ya juu kuhusu uwiano wa chanjo duniani ukihudhuriwa na wataalamu na viongozi w anchi wanachama.

Akizungumzia ujenzi endelevu wa kiuchumi baada ya janga la Corona, Rais huyo wa Baraza Kuu amesema atashirikiana na Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa pamoja na mfumo wa Umoja huo na taasisi za kifedha ili kusaidia kuhakikisha kuwa ukwamukaji wa kiuchumi na kijamii unazingatia mustakabali wa dunia, akimaanisha si haribifu kwa mazingira ya ardhi na baharí na vile vile unakuwa na mnepo zaidi.

Kufuatia kuapishwa kwa Bwana Shahid, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amempongeza kwa dhati akisema kuwa uzoefu wake katika diplomasia ikiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Maldives utakuwa na mchango mkubwa wakati wa kipindi chake cha uongozi.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kulia) akiwa na Abdulla Shahid, Rais wa UNGA76
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kulia) akiwa na Abdulla Shahid, Rais wa UNGA76

Guterres amesema, “Rais huyu wa Baraza Kuu kutoka Maldives atakuwa chachu mpya katika uzoefu wa nchi za visiwa vidogo na ninasubiri kwa hamu kufanya naye kazi kwa ushirikiano.”

Kuhusu changamoto na mgawanyiko ambao dunia inakabiliwa nao hivi sasa, Katibu Mkuu amesema “tunapaswa kuongeza kasi. Tunapaswa kuongeza kasi ya hatua zetu dhidi ya COVID-19, chanjo, tib ana vifaa kwa kila mtu si kwa wale tu ambao tayari wamepata vifaa kupita kiasi.”

Bwana Abdulla alichaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 7 mwezi Juni mwaka huu kuwa Rais wa mkutano wa 76, UNGA76 ambao utatamatishwa mwezi Septemba mwaka 2022.