Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya magonjwa na uharibifu, Rais mteule wa Baraza Kuu asema matumaini ndio msingi wa ushindi

Rais Mteule wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid akiwa ndani ya  ukumbi wa Baraza hilo
UN/Eskinder Debebe
Rais Mteule wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid akiwa ndani ya ukumbi wa Baraza hilo

Licha ya magonjwa na uharibifu, Rais mteule wa Baraza Kuu asema matumaini ndio msingi wa ushindi

Masuala ya UM

Mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75 unafungwa rasmi hii leo na kutoa fursa ya kufunguliwa kwa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76 unafungua pazia lake hii leo huku rais wake mteule Abdulla Shahid kutoka Maldives akisema tumaini ndio limesalia kuwa tegemeo kwa mabilioni ya watu duniani wakati huu wakihaha katikati ya janga la COVID-19, uharibifu wa mazingira, vita na majanga mengineyo.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, UN News jijini New York, Marekani kabla ya kuapishwa rasmi leo kupokea kijiti cha kuongoza Baraza hilo,  Bwana Shahid amesema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo ndio chombo chenye uwakilishi mpana zaidi katika Umoja huo limeundwa ili kuweka mwongozo wa muundo wa matumaini yao. 

Naahidi kwamba katu sitokaa katika jopo la mkutano lisilo na uwiano kijinsia- Abdula Shahidi, Rais Mteule UNGA76

Ametoa mfano wa jinsi tumaini liliinuka katikati ya janga la Corona na kwamba ni wakati wa kusimama kidete na kutoa matumaini kwa kuwa “tumeshuhudia utu katika ubora wa juu kabisa. Tumeona kujitoa kwa hali na mali kwa wahudumu walio mstari wa mbele. Tumeona madaktari, wauguzi na watu wa kawaida kabisa wakiweka maisha yao rehani ili kusaidia wengine. Hicho ni tumaini. Tumeona chanjo imetengenezwa katika kasi isiyo ya kawaida. Hilo ni tumaini.”

Akagusia pia hatua atakazochukua kukabili mabadiliko ya tabianchi “natarajia kuitisha kikao maalum ili kupatia nchi fura ya kukutana na kupitisha tamko la mwisho la kisiasa. Ndio tumeazimia kupunguza joto kwa nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi. Ndio! Tunajali ubinadamu. Nchini Maldives ambako ninatoka, kila siku tunaishi na tishio la mabadiliko ya tabianchi lakini katu hatukati tamaa. Ubinadamu utashinda tishio hilo na tutaishi.”

Bwana Shahid akaulizwa jinsi atatumia uongozi wake kusongesha usawa wa jinsia ambapo amesema,“naahidi kwamba katu sitokaa katika jopo la mkutano lisilo na uwiano kijinsia. Natarajia kuhakikisha kuwa suala la usawa wa kijinsia linaendelea kuwa moja ya vipaumbele vyangu vya juu wakati wote wa uongozi wangu.”

Ushiriki hai wa vijana ni kiini cha jamii thabiti na kuzuia vitisho vibaya zaidi dhidi ya  maendeleo endelevu, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi
ICAN/Lucero Oyarzun
Ushiriki hai wa vijana ni kiini cha jamii thabiti na kuzuia vitisho vibaya zaidi dhidi ya maendeleo endelevu, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi

Naimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa kuwekeza kwa vijana

Rais huyu mteule wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amezungumzia pia ushirikiano wa kimataifa akisema ndio njia pekee ya kusonge mbele akisema kuwa, “nataka kupatia fursa wanadiplomasia vijana kutoka nchi ambazo hazina uwakilishi wa kutosha na ndio maana nimezindua mpango wa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa mafunzo kwa vijana. Ni kuwapatia fursa ya kufanya kazi na ofisi yangu ili wapate uzoefu wa kile kinachofanyika hapa. Kuwekeza katika ushirikiano wa kimataifa ndio tunapaswa kufanya sasa. Na uwekezaji mzuri zaidi wa ushirikiano wa kimataifa ni kuwekeza kupitia kwa vijana.”

Mkutano wa UNGA76 ambao unaanza leo utamalizika mwezi Septemba mwaka 2022 ukijumuisha vikao mbalimbali ambapo wiki ijayo kutaanza mjadala wa wazi wa ngazi ya juu ukijumuisha hotuba za viongozi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa.