Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia bado inaweza kutatua changamoto ya mabadiliko ya tibianchi, kutimiza SDGs na kuishi vyema na mazingira:UN 

Bahari yenye afya ambapo vyai vinashamiri ni muhimu kwa uwepo wa sayari dunia.
NOAA
Bahari yenye afya ambapo vyai vinashamiri ni muhimu kwa uwepo wa sayari dunia.

Dunia bado inaweza kutatua changamoto ya mabadiliko ya tibianchi, kutimiza SDGs na kuishi vyema na mazingira:UN 

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP inatoa muongozo wa jinsi ya kushughulikia changamoto kubwa tatu za dharura zinazoikumba dunia ambazo ni mabadiliko ya tabianchi, kuishi vyema na mazingira na ufikiaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Ripoti hiyo “kuwa na amani na maliasili” iliyozindiliwa kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na mkurugenzi mtendaji wa UNEP Inger Anderson jijini Nairobi Kenya na New York Marekani, imeweka bayana ukubwa wa dharura hizo tatu kutokana na tathimini iliyofanywa kimataifa na wadau mbalimbali lakini pia kilichobainika kuhusu magonjwa ya kuambukiza yatokanayo na wanyama kama corona au COVID-19. 

Waandishi wa ripoti wametathimini uhusiano uliopo baina ya changamoto za mazingira na maendeleo na kuelezea jinsi gani maendeleo ya kisayansi na sera madhubuti vinaweza kufungua njia ya kuelekea utimizaji wa maelngo ya maendeleo endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030 na kuwa na dunia isiyozalisha hewa ukaa ifikapo mwaka 2050, huku vikibadili mwenendo wa upotevu wa bayoanuai na kushughulikia utoaji wa hewa chafuzi . 

Mbinu hizo ni pamoja na kukumbatia ubunifu na uwekezaji ambao utawalinda watu na mazingira imesisitiza ripoti, ikitaka mifumo ya maisha irejeshwe kwenye msitari, maisha yawe yenye afya na kukomesha mabadiliko ya tabianchi. 

“Kwa kuleta pamoja ushahidi wa kisayansi ukionyesha athari na vitisho vya dharura ya mabnadiliko ya tabianchi, mgogoro wa bayoanuai na uchafuzi wa hewa ambao unaua mamilioni ya watu kila mwaka, ripoti hii inaweka bayana kwamba vita vyetu na mazingira asilia vimeisambaratisha dunia, lakini pia inatuongoza katika mahali salama kwa kutupa mpango wa amani na wa ujenzi mpya baada ya vita”.  amesema Katibu Mkuu Antonio Guterres katika ripoti hiyo na kuongeza kuwa  “Kwa kubadilisha jinsi gani tunavyoyatazama mazingira yetu ya asili tunaweza kutambua thamani yake halisi. Kwa kuiweka thamani hiyo katika sera zetu , mipango na mifumo ya uchumi, tunaweza kuelekeza uwekezaji katika shughuli ambazo zinarejesha uasili wa mazingira yetu na tukapata faida. Kwa kutambua kwamba mazingira yetu ni mshirika wetu mkubwa basi tutayafanya kuwa endelevu, na kutufanya tuwe na afya njema na ustawi sambamba na mazingira yetu.” 

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba changamoto hizo tatu zinahusiana na zinaweza kushughulikiwa kwa pamoja. Inger Anderson mkuu wa UNEP kwa upande wake amesema ripoti inaonyesha umuhimu wa kubadili fikra, mtazamo na hulka na kisha kusaka suluhu za kisiasa na kiufundi ambazo zinaweza kumudu mgogoro wa mazingira unaoikabili dunia. 

“Na hii ni kuonyesha jinsi gani afya ya binadamu na mazingira asili vinavyoingiliana. Janga la COVID-19 limedhihirisha haja ya kubadili hatua za jinsi tunavyoyachukulia mazingira yetu ya asili na thamani yake. Kwa kuingiza fikra hizo kwenye ufanyaji maamuzi au katika machaguo binafsi, tunaweza kuleta mabadiliko kuelekea uendelevu kwa binadamu na mazingira”. Aeongeza bi Anderson. 

Ripoti hiyo iliyotolea kabla ya kuanza kwa Baraza Kuu la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEA,imesema hatua za haraka zinahitajika ili kuinusuru dunia na mazingira yake na kutaja hatua hizo kuwa ni “Mosi: Ni kuhakikisha kwamba malengo ya mabadiliko ya tabianchi na bayoanuai yanatimia, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kutimiza malengo ya SDGs yanajumuisha msukumo wa jamii nzima, pili:kubadili mtazamo wa dunia na kuyaweka mazingira ya asili katika kitovu cha kufanya maamuzi kwani ni muhimu katika kufikia mabadiliko ya kweli na tatu: mipango ya kujikwamua na janga la COVID-19 ni fursa nzuri ya kuwekeza katika mazingira na maliasili na kufikia kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo 2050.”