Dola milioni 10.5 zitaokoa viumbe walio hatarini kutoweka :UNEP

8 Disemba 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP, limepokea dola milioni 10.5 kutoka  serikali ya Luxemburg, ikiwa ni  mchango utakaosaidia kulinda aina za wanyamapori  waishio  mlimani ambao wako katika tisho la kutoweka.

Hahadi hiyoiliyotolewa leo kwenye mkutano wa mazingira mjini Nairobi Kenya,  imekuja wakati UNEP inajiandaa na  maadhimisho siku ya milima duniani hapo tarehe 11 mwezi huu. Shirika hilo limesema fedha hizo zitasaidia kulinda aina ya wanyama kama lengau, nyani  na aina ya sokwe ambao tafiti zinaonyesha kua miaka 50 ijao kusipokuwepo na jitihada za kimazingira za kuwalinda, basi watatoweka katika uso wa dunia.

Bwana  Erik Solheim mkurugenzi mtendaji wa  UNEP, amesema kadri mabadiliko ya tabia nchi yanavyozidi kuenea  ndivyo , aina za viumbe  nyeti  na pia maeneo ya  asili yanavyoathirika. Hata hivyo amesema  ufumbuzi wa mapema wa jinsi ya kukabiliana na tatizo la   mazingira unaweza kusaidia kuhifadhi wanyamapori kupitia misaada kama iliotolewa na serikali ya Luxemburg.

UNEP imesema mpango mpya unaongozwa kwa ushirikiano na  Luxemburg utazingatia kuboresha na kugawana maarifa na  mbinu za ubunifu za mazingira ya kukabiliana na hali ya hewa.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter