Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa ni nini na kwa nini ni muhimu?

Mkutano wa Sita wa Wazi wa Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (OECPR-6) huko Nairobi, Kenya.
UNEP / Eugene Kaiga
Mkutano wa Sita wa Wazi wa Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (OECPR-6) huko Nairobi, Kenya.

Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa ni nini na kwa nini ni muhimu?

Tabianchi na mazingira

Umewadia wakati ambapo nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zitapata fursa ya kuonesha kwamba vitendo vya mazingira vinaweza kuunganisha ulimwengu. Wakati huu ni Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira, au Unea, ambalo mkutano wake wa sita utafanyika kati ya Februari 26 na Machi 1, 2024 Nairobi, Kenya.

Limeundwa kuwa aina ya "baraza la mazingira duniani", ambalo linakutana kila baada ya miaka miwili ili kufafanua vipaumbele vya sera za mazingira na kuunda sheria za kimataifa kuhusu suala hilo. Hili ndilo tukio pekee kando na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo Nchi Wanachama wote hushiriki.

Wajumbe wakusanyika kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira mjini Nairobi, Kenya.
UNEP/Duncan Moore
Wajumbe wakusanyika kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira mjini Nairobi, Kenya.

Kwanini Unea ni muhimu?

Toleo hili linakutanisha wajumbe 6,000, wakiwemo wakuu wa nchi 7 na mawaziri na makamu 139, pamoja na wataalamu, wanaharakati, na wawakilishi wa sekta hiyo. 

Unea ilianzishwa mwaka wa 2012, katika Mkutano wa Rio+20, uliofanyika nchini Brazil. Tangu wakati huo, limeleta enzi mpya ya ushirikiano wa pande nyingi ambapo mazingira yanapewa kiwango sawa na masuala mengine ya kimataifa kama vile amani na afya.

Kwa miaka mingi, Unea imeidhinisha maazimio muhimu kuhusu mada kama vile kupambana na usafirishaji haramu wa wanyamapori, kulinda mazingira katika maeneo yenye migogoro ya silahauhamaji endelevu mijini, miongoni mwa mengine mengi.

Kama matokeo ya kikao cha mwisho cha Baraza hilo, mwaka 2022, mazungumzo yalianza juu ya chombo cha kwanza cha kisheria cha kimataifa kumaliza uchafuzi wa plastiki, ambacho kinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa 2024.

Plastiki inayotumika mara moja inaoelea karibu na mwamba wa matumbawe, Bali.
© Ocean Image Bank/Naja Bertolt
Plastiki inayotumika mara moja inaoelea karibu na mwamba wa matumbawe, Bali.

Ni nini kiko hatarini katika mkutano huu?

Mada kuu ya Unea-6 itakuwa makubaliano ya kimataifa ya mazingira na jinsi yanavyoweza kusaidia kushinda shida ya sayari tatu ya mabadiliko ya tabianchi, upotezaji wa bayoanuwai na uchafuzi wa mazingira.

Licha ya msukosuko unaosababishwa na janga hili na kuongezeka kwa mvutano wa kijiografia, miaka miwili iliyopita imekuwa na ushindi muhimu sana wa ushirikiano wa mazingira.

Mnamo mwaka 2022, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitambua haki ya binadamu ya ulimwengu kwa mazingira safi, yenye afya na endelevu, na kufungua nafasi ya mabadiliko ya kikatiba na kisheria kwa ajili ya mazingira na ubinadamu.

Katika mwaka huo huo, Mfumo wa kihistoria wa Biodiversity wa Kunming-Montreal uliidhinishwa, ukiwa na hatua za kulinda spishi milioni 1 za wanyama na mimea ambazo tayari ziko katika harakati za kutoweka.

Mnamo Juni 2023, nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilitia saini Mkataba wa Bahari Kuu, ili kuhifadhi bioanuwai ya baharini katika maeneo yaliyo nje ya mamlaka ya kitaifa.

Novemba mwaka jana, makubaliano yaliyosubiriwa kwa muda mrefu kuhusu ufadhili wa "Hasara na Uharibifu" kwa nchi zilizoathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi yalitangazwa kwenye Mkutano wa Wanachama wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP 28.

Unea itakuwa na siku maalum kwa mifano hii na mingine iliyofanikiwa kujadili jinsi serikali zinaweza kuchukua hatua pana na za umoja, ikiwa ni pamoja na ufadhili wa kutosha, ili kutekeleza mikataba ya kimataifa ambayo wametia saini.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen katika Kikao cha 31 cha Jopo la Kimataifa la Rasilimali mjini Nairobi.
UNEP
Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen katika Kikao cha 31 cha Jopo la Kimataifa la Rasilimali mjini Nairobi.

Mada za kipaumbele zitakuwa zipi?

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira -UNEP, Inger Andersen, aliangazia maeneo sita ya kipaumbele kwa Unea-6: Uhaba wa maji, uchimbaji madini unaowajibika, usimamizi wa madini, hasa fosforasi, teknolojia ya kubadilisha hali ya hewa, ufadhili wa hatua za mazingira na utekelezaji wa Mkataba wa Kunming -Montreal.

Bi. Andersen amesema, “tunachohitaji kufanya ni kukusanyika pamoja na kutoa suluhu hizi za kimataifa ambazo tumeahidiana ili tuweze kupata mustakabali wa wanadamu wote, wanaoishi kwenye sayari yenye afya na inayostawi.”

Mazungumzo kabla na wakati wa tukio yanalenga maazimio yaliyopendekezwa yaliyowasilishwa na Nchi Wanachama na tamko la mwisho la mawaziri. 

Maazimio yanabainisha na kutoa kipaumbele kwa changamoto za pamoja na masuluhisho yanayowezekana. Pia zinafafanua maeneo ya kipaumbele ya kazi kwa UNEP.

Katika Unea-6, maazimio 20 na maamuzi 2 yatajadiliwa, yakijumuisha mada kama vile urekebishaji wa mionzi ya jua, uchimbaji madini, kuenea kwa jangwa, mzunguko wa kilimo cha miwa, viuatilifu hatari sana, kuongeza ustahimilivu wa mifumo ikolojia na jamii kukabiliana na ukame, ushirikiano wa kikanda kwa ubora wa hewa, miongoni mwa wengine.

Mazungumzo yanafanyaje kazi?

Katika Baraza, maazimio yanatarajiwa kupitishwa kwa maridhiano. Kwa vitendo, hii inampa kila mtu aliyepo haki ya kura ya turufu. Kwa hivyo, wiki moja kabla ya mkutano ni muhimu kwa wajumbe kukagua maazimio na kushinda migongano. 

Mazungumzo mara nyingi yanaenea hadi wiki ya mkutano, na vikao vya milangoni ambavyo vinaendelea hadi usiku.

Kama chombo cha juu zaidi cha maamuzi duniani kuhusu mazingira, Unea inalenga kusaidia kurejesha uwiano kati ya ubinadamu na asili, kuboresha maisha ya watu walio hatarini zaidi duniani. 

Mkazo mwaka huu hautakuwa tu juu ya ahadi mpya, lakini katika kutimiza yale yote ambayo tayari yapo.

UNEP itanunua mikopo ya kaboni iliyoidhinishwa ili kukabiliana na uzalishaji wa usafiri kutoka kwa washiriki wanaofadhiliwa kama sehemu ya mchakato wake wa kila mwaka wa hesabu ya mazingira ili kukabiliana na uzalishaji wa gesi chafuzi, pamoja na hatua nyingine kadhaa za kupunguza athari za mazingira za mkutano huo.