Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2020 ulikuwa wa kifo na sasa 2021 ni wa matumaini, tushirikiane- Guterres

Mwanafunzi wa kike akiandika kwa makini akiwa darasani huku amevalia barakoa yake ya kushoneshwa nyumbani. Hapa ni katika shule ya msingi ya Mchoka wilaya ya Salima nchini Malawi, tarehe 13 Novemba mwaka 2020.
© NICEF/UN0372089/
Mwanafunzi wa kike akiandika kwa makini akiwa darasani huku amevalia barakoa yake ya kushoneshwa nyumbani. Hapa ni katika shule ya msingi ya Mchoka wilaya ya Salima nchini Malawi, tarehe 13 Novemba mwaka 2020.

Mwaka 2020 ulikuwa wa kifo na sasa 2021 ni wa matumaini, tushirikiane- Guterres

Masuala ya UM

Mwaka 2020 ulikuwa ni mwaka wa majanga lakini 2021 ni mwaka wa fursa na matumaini! Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa leo kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  jijini New York, Marekani akielezea vipaumbele vyake 10 kwa mwaka 2021. 

Vipaumbele hivyo ni kusongesha usawa katika chanjo dhidi ya COVID-19, kujikwamua kutoka COVID-19 kupitia mbinu endelevu na zisizoharibu mazingira, hatua kwa tabianchi, kukabili ukosefu wa usawa na umaskini, haki za binadamu, usawa wa jinsia, amani, usalama na sitisho la mapigano, kutoendeleza nyuklia, ukiritimba katika teknolojia za digitali na kupanga upya ajenda ya dunia kwa ustawi wa wote.

Guterres akianza hotuba yake kwa lugha ya kilatini, Annus Horribilis kwa 2020 na annus possibilitatis kwa mwaka 2021 amesema mwaka 2020 ulikuwa wa kifo, janga na kukata tamaa.

Tweet URL

“Tumepoteza watu milioni 2, wakiwemo wanafamilia ya Umoja wa Mataifa. Idadi ya vifo inaongezeka, gharama za kiuchumi halikadhalika. Ajira milioni 500 zimepotea. Umasikini wa kupindukia umerejea katika viwango havijawahi kushuhudia katika vizazi kadhaa. Pengo la ukosefu wa usawa linaongezeka. Njaa inaongezeka tena. Utete kwenye dunia umefichuka. Tumetangaza vita dhidi ya mazingira na mazingira yanajibu. Janga la tabianchi linasambaa,” amesema Katibu Mkuu.

Amesema kama hiyo haitoshi, mivutano baina ya mataifa inaendelea kudumaza jitihada za pamoja za kuleta amani duniani, mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka, watu wanalazimika kukimbia makwao na idadi ya mwaka jana ya wakimbizi imevunja rekodi.

“Wakati huo huo, hatari ya kuendelezwa kwa silaha za nyuklia na kemikali nayo inaongezeka, haki za binadamu zinabinywa, kauli za chuki zimeshamiri, uvunjifu wa sheria kupitia mitandao unaongezeka na kuweka jukwaa jipya la uhalifu, ghasia, taarifa potofu na mvurugano.” 

Bwana Guterres amesema pamoja na changamoto zote hizo, mwaka 2021 lazima uwe mwaka wa kubadilisha mbinu na kurejesha dunia kwenye mwelekeo sahihi kwa kuwa “ni lazima tuondokane na vifo tujenge afya, tuondokane na majanga tuweke ujenzi mpya, kutoka kukata tamaa hadi matumaini na kutoka kufanya mambo kikawaida na badala yake mabadiliko.”

Ni kwa mantiki hiyo ametaja vipaumbele vyake 10 atakavyozingatia kwa mwaka huu wa 2021 akianza na chanjo dhidi ya Corona au COVID-19.

Wanawake nchini Nigeria wakipokea mgao wa vocha za chakula kama sehemu ya programu ya kusaidia familia zinazohaha wakati huu wa COVID-19 na hatua za kudhiiti kusambaa kwa ugonjwa huo.
WFP/Damilola Onafuwa
Wanawake nchini Nigeria wakipokea mgao wa vocha za chakula kama sehemu ya programu ya kusaidia familia zinazohaha wakati huu wa COVID-19 na hatua za kudhiiti kusambaa kwa ugonjwa huo.

Chanjo ya COVID-19 ifikie kila mtu

Kipaumbele cha kwanza ni chanjo, akisema janga hilo  katu haliwezi kumalizwa na nchi moja pekee, “iwapo virusi hivyo vitaachiwa visambae kama moto wa nyika katika nchi za kusini, vitabadilika tabia zao na kuweza kusambaa kwa haraka zaidi, kusababisha vifo na kuwa sugu kwa chanjo na kisha kurejea katika nchi za kaskazini.”

Amesema cha kusikitisha zaidi chanjo zinafikia haraka nchi chache ilhali nchi masikini zaidi hazina kabisa chanjo hizo. “Sayansi inafanikiwa lakini mshikamano unashindikana.”

Bwana Guterres amesema katika mazingira kama hayo, mshindi pekee katika dunia ya walio nacho na wasio nacho ni virusi!

Tutajikwamua vipi iwapo uchumi uko mahututi?

Akielekea kwenye kipaumbele cha pili, Guterres amesema wakati  huu ambapo dunia inahaha kujikwamua kutoka janga la COVID-19, ni lazima mikakati ya kuhakikisha kukwamuka huko kunakuwa jumuishi na endelevu ni lazima ianze kuandaliwa sasa kwa kuwa dunia haiwezi kusubiri kuponyeka kutoka kwenye janga la Corona iwapo uchumi uko mahututi.

Ni kwa mantiki hiyo amesema kinachohitajika ni uwekezaji mkubwa katika mifumo ya afya kila pahali, huduma ya afya kwa kila mtu, au UHC, afya ya akili ipatiwe kipaumbele, hifadhi ya jamii kwa kila mtu, ajira zenye hadhi, watoto warejee shuleni salama na zaidi ya yote nchi tajiri ziangalie uwezekano wa kufuta madeni ya nchi maskini kwa kuwa hivi sasa shughuli za kiuchumi zimedumaa.

“Nchi tajiri zinatekeleza mipango ya kujikwamua kwa kutoa mipango yenye thamani ya matrilioni ya dola, ilhali nchi maskini zimeweza kutumia asilimia 2 tu za pato lao la ndani. Kujikwamua lazima kuwe jumuishi. Hakuna nchi ambayo italazimishwa kuchagua kati ya kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake au kulipa deni.”

Mafuriko nchini Uganda ambako nyumba zimezama.
UN News/ John Kibego
Mafuriko nchini Uganda ambako nyumba zimezama.

Hatua thabiti kulinda sayari dunia

Kipaumbele cha tatu ni hatua kwa tabianchi ambapo ametoa wito kwa kila jiji, kampuni au taasisi ya fedha kuridhia mikakati thabiti yenye lengo la kuondokana na utoaji wa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050. “Sekta muhimu kama vile usafirishaji kwa njia ya meli, anga, viwanda na kilimo nazo lazima zifanye vivyo hivyo.”

Amerejelea wito wake ya kwamba wakati umefika kuweka gharama katika hewa ya ukaa, na kuacha kujenga mitambo mipya ya nishati ya makaa yam awe na kuondokana na mitambo hiyo ifikapo mwaka 2040.

Tuondokane na janga la umaskini na ukosefu wa usawa

Ongezeko la ukosefu wa usawa katika umiliki wa mali umeathiri zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wa dunia wakati huu ambapo fursa za mtu kustawi kimaisha zinategemea jinsia, rangi, familia na kabila alilotoka, na iwapo wana ulemavu au la na vigezo vingine.

Ombeni Sanga, mvumbuzi kijana mtanzania ambaye ametengeneza kifaa chenye uwezo wa kusambaza elimu katika mazingira ambayo hakuna mwalimu.
UN Tanzania
Ombeni Sanga, mvumbuzi kijana mtanzania ambaye ametengeneza kifaa chenye uwezo wa kusambaza elimu katika mazingira ambayo hakuna mwalimu.

 

Janga la COVID-19 nalo limetumia fursa ya uwepo wa mapengo hayo na kujiimarisha.

Ni kwa kuzingatia hilo katika kipaumbele hiki cha nne Katibu Mkuu anatoa wito wa mkataba mpya wa kijamii ndani ya nchi, wa kuhakikisha kila mtu anakuwa na matumaini ya ustawi na ulinzi akisema, “elimu na teknolojia ya dijitali ni mambo makubwa mawili ya kuwzesha na kuleta usawa. Kufanyike marekebisho katika masoko ya ajira, na hatua za makusudi dhidi ya rushwa, utakatishaji wa fedha, usafirishaji haramu wa fedha na vitendo vya kusamehe ulipaji wa kodi.”

Katibu Mkuu amekumbusha pia umuhimu wa misaada rasmi ya maendeleo na marekebisho katika mfumo wa kujaliana katika dunia ya sasa ili kufanikisha ahadi ya kutomwacha nyuma mtu yeyote kwenye safari ya maendeleo endelevu.

Tusimame kidete kulinda haki za binadamu

Suala la haki za binadamu ni kipaumbele cha tano ambapo Guterres amekaribisha mwelekeo mpya wa dunia wa kukabiliana na haki dhidi ya ubaguzi wa rangi. Amesema ukosefu wa usawa kwa misingi ya rangi bado ni tatizo kwenye taasisi, mifumo ya kijamii na katika maisha ya kila siku, “sote tunapaswa kusimama kidete dhidi ya kuibuka kwa manazi mamboleo na wale wanaoona kuwa watu weupe ni bora zaidi kuliko wengine.”

Usawa wa Kijinsia

Kipaumbele cha sita kwa Guterres kwa mwaka 2021 ni kusongesha usawa wa jinsia akisema “COVID-19 imeangazia kile ambacho mara nyingi hakionekani. Wanawake ni wafanyakazi muhimu wanaowezesha jamii kuwa hai. Ni wakati wa kubadili mifumo na miundo kwenye jamii. Sekta rasmi ya uchumi inafanya kazi kwa sababu tu kazi ya malezi inayofanywa na wanawake hailipiwi ujira.”

Wakulima kutoka ushirika wa wanawake wakulima wa mbogamboga wa Koinadugu, Sierra Leone wakivuna kabichi kutoka katika shamba lao lao la jumuiya. Miradi kama hii ni moja ya miradi inayofadhiliwa na FAO kote duniani.
NOOR for FAO/Sebastian Liste
Wakulima kutoka ushirika wa wanawake wakulima wa mbogamboga wa Koinadugu, Sierra Leone wakivuna kabichi kutoka katika shamba lao lao la jumuiya. Miradi kama hii ni moja ya miradi inayofadhiliwa na FAO kote duniani.

Amani na Usalama: Hatuwezi kutatua shida zetu iwapo wenye nguvu hawaelewani

Ili kukabili changamoto ya amani na usalama, Guterres ametaja mambo hayo mawili kuwa kipaumbele cha saba akisema, “kushughulikia vitisho vya zama vya sasa vya amani na usalama, tunahitaji kuweka daraja katika utambuzi wa kiasilia. Tunahitaji kuepuka ufa mkuu ambao unaweza kugawanya dunia katika vipande viwili. Tufanye kazi tuhakikishe tuna ulimwengu mmoja na unaoheshimu sheria za kimataifa na kanuni zinazotambuliwa na wote. Ukosefu wa maelewano baina ya nchi zenye uthabiti zaidi duniani, ni upenyo unaoweza kutumiwa na wengine kuleta mvurugano. Hatuwezi kutatua matatizo yetu iwapo wenye nguvu hawana maelewano.”

Amerejelea wito wa sitisho la mapigano kuanzia Syria hadi Sudan Kusini, Yemen hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako amesema wito wake wa kusitisha mapigano mara kwa mara unakiukwa.

Bwana Guterres amesema ingawa mipango ya ulinzi wa amani inakuwepo bado kuna changamoto ulinzi wa amani uko kwenye maeneo yasiyo ya amani ya kulinda. “Tayari mwaka huu pekee, walinda amani 9 wameuawa. Tunapaswa kuhakiisha kila ujumbe wa kulinda amani na kila mlinda amani ana rasilimali na vifaa sahihi vya kumwezesha kutekeleza jukumu lake,” amesema Katibu Mkuu.

Guterres ametaja kipaumbele cha nane kuwa ni kubadili mwelekeo wa uendelezaji wa silaha za nyuklia akipongeza kuanza kutumika wiki iliyopita kwa mkataba wa kimataifa wa kuzuia silaha za nyuklia, TPNW akitaka nchi zote ziunge mkono lengo la mkataba huo.

Kipaumbele cha tisa ni kutumia fursa za teknolojia za kidijitali sambamba na kuweka mbinu za kuepusha matumizi mabaya za teknolojia hizo akisema, “wakati wa janga la Corona, teknolojia zimeendelea kuunganisha jamii lakini janga hilo hilo limeonesha pengo la ufikiaji na upataji wake kwa baadhi ya makundi na jinsia. Lazima tuzibe pengo la teknolojia za kidijitali.”

Tujipange upya kufanikisha karne ya 21

Kwa kutamatatisha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ili kukamilisha vipaumbele vyote ni lazima kupanga upya usimamizi wa dunia katika karne ya 21. Amesema hicho ndio kipaumbele chake cha kumi  kwa kuwa, “Changamoto zilizo mbele yetu zinataka ujumuishwaji zaidi na ushirikiano wa kimataifa. Nimetoa wito wa makubaliano mapya baina ya nchi yatakayohakikisha kuwa mamlaka, faida na fursa zinagawanywa kisawia na kwa mapana zaidi. Nchi zinazoendelea zinahitaji jukwaa la kupaza sauti zaidi kwenye maamuzi yoyote ya dunia.”

Bwana Guterres amesma “vijana wawepo kwenye meza za maamuzi kama wabunifu wa mustakabali wao na si wapokea maamuzi kutoka kwa watu wazima, ambao hebu tuwe wazi, tumewaangusha katika mambo ya msingi.”