Tunashukuru kwa usaidizi dhidi ya COVID-19, sasa maisha yamerejea hali ya kawaida- Tanzania

Tunashukuru kwa usaidizi dhidi ya COVID-19, sasa maisha yamerejea hali ya kawaida- Tanzania
Tanzania imezungumza kwenye mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuelezea msimamo wake katika masuala mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kimataifa, janga la ugonjwa wa Corona, COVID-19, amani na usalama maziwa makuu na mustakabali wa Umoja wa Mataifa wakati huu ambapo chombo hicho kinatimiza miaka 75 tangu kuanzishwa kwake.
Misimamo hiyo ya Tanzania imetolewa na Rais John Magufuli wa Tanzania kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo na Mwakilishi wa kudumu wa taifa hilo kwenye Umoja huo, Balozi Profesa Kennedy Gastorn.
Katika hotuba hiyo, Balozi Gastorn amesema , “nina heshima kubwa kuwasilisha hotuba hii kwa niaba ya Rais John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye hakuweza kuungana nanyi kwa njia ya mtandao kwa kuwa hivi sasa anashiriki kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini humo. Rais Magufuli anawania awamu ya pili ya uongozi kwenye uchaguzi utakaofanyika tarehe 28 mwezi ujao wa Oktoba.”

Ametumia sehemu ya mwanzo ya hotuba yake kusema kuwa Tanzania imesisitiza azma yake ya kwamba kampeni na uchaguzi vinafanyika kwa amani, huru, uhalali na kwa uwazi kama ambavyo imekuwa ikifanya tangu mwaka 1965.
Janga la COVID-19: Kwa Tanzania maisha yamerejea hali ya kawaida
Maudhui ya mjadala mkuu mwaka huu wa ushirikiano wa kimataifa ambao Tanzania umesema unaendana na kile ambacho kinapatiwa kipaumbele sasa cha kutomwacha mtu yeyote nyuma na hivyo inaunga mkono maudhui hayo.
Amesema ni katika muktadha huo huo, Tanzania inashukuru juhudi zote ndani ya Umoja wa Mataifa za kuhamasisha juhudi za kukabili janga hiloi ikiwemo “kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kupunguza kusambaa zaidi kwa janga hilo. "
Ushirikiano huo wa kimataifa ameupigia chepuo kwa jinsi dunia imeshirikiana kukabili COVID-19, akisema kuwa, “mlipuko na kuenea kwa COVID-19 duniani kumetukumbusha kuwa tunapaswa kuimarisha mshikamano ndani ya mfumo wetu wa ushirikiano ili kuweza kukabili changamoto kama janga la Corona ambalo pamoja na kusababisha vifo, limevuruga uchumi wa nchi na dunia nzima.”

Amesema ni katika muktadha huo huo, Tanzania inashukuru juhudi zote ndani ya Umoja wa Mataifa za kuhamasisha juhudi za kukabili janga hiloi ikiwemo “kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kupunguza kusambaa zaidi kwa janga hilo. Katika ngazi ya taifa, serikali imechukua hatua za kina za kupunguza kuenea kwa COVID-19 na hatua hizo zimefanikisha matokeo chanya ya kutokomeza janga hilo nchini kote. Leo hii shughuli zote za kiuchumi na kijamii zimerejea katika hali ya kawaida.”
Hata hivyo amesema kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, “hatuwezi kuyakana madhara ya janga hilo kwa nchi yetu na duniani kwa ujumla hasa kwa nchi maskini na zile zinazoendelea, tunashukuru wadau wetu wa maeneleo ikiwemo taasisi za fedha za kimataifa ambazo zimesaidia juhudi zetu za kutokomeza janga hilo kwa kutupatia unafuu kwenye ulipaji madeni, kuahirisha ulipaji madeni na hata kutupatia mikopo yenye riba nafuu.”
Pamoja na shukrani hizo, Tanzania imependekeza hatua zaidi ikiwemo msamaha wa madeni ili nchi maskini na zile zinazoendelea ziweze kujikwamua kiuchumi.

Tanzania na miaka 75 ya Umoja wa Mataifa
Kuhusu miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, Tanzania imesisitiza azma ya pamoja na mataifa mengine ya kuendelea kusimamia na kuzingatia misingi ya Umoja wa Mataifa ambayo ni amani na usalama, haki za binadamu na maendeleo.
Halikadhalika iko kidete na kamati ya Umoja wa Mataifa ya kutokomeza ukoloni hadi pale nchi zote duniani zitakapokuwa huru.
Akisisitizia mchango wa Tanzania na misingi ya Umoja wa Mataifa ametaja ulinzi wa amani ambako hadi sasa kuna walinda amani 2,300 kwenye mataifa 6 wanakohudumu walinda amani hao ikiwemo Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC na Lebanon.
Ushirikiano wa kimataifa
Akimulika ushirikiano wa kimataifa, amesema bila shaka ni mbinu muhimu ya kufanikisha ushirikiano baina ya mataifa. “Tunapoingia muongo wa utekelezaji kuelekea ukomo wa ajenda 2030 tunaendelea kuamini kuwa Umoja wa Mataifa ni jukwaa pekee la kujadili changamoto za dunia.”
Ametaja mafanikio ya Tanzania katika utekelezaji wa ajenda hiyo ikiwemo ukuaji wa uchumi wa asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.2 mwaka 2015.
Ukurasa kuhusu Virusi vya Corona & taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.Hata hivyo amekiri kuwa COVID-19 imesababisha makadirio ya ukuaji uchumi kushushwa hadi asilimia 5.5 kwa hiyo “tunahitaji msaada ili kusaidia kufikia makadirio bora zaidi ya ukuaji uchumi.”
Ameongeza kuwa serikali imechukua hatua kuunganisha maendeleo ya kiuchumi na yale ya wananchi wake kwa kuboresha miundombinu muhimu katika utoaji wa huduma za kijamii.
“Mathalani, katika miaka mitano iliyopita, maeneo ya utoaji wa huduma ya afya 1,769 yamejengwa nchini kote ikiwa ni kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za rufaa. Halikadhalika ujenzi wa na ukarabati wa miundombinu ya maji.”
Miaka 25 baada ya Beijing
Jukwaa la Beijing, au mkutano wa kimataifa wa wanawake uliofanyika Beijing, China, miaka 25 bado haujaweza kufuta kabisa pengo la usawa duniani ambapo Balozi Gastorn amesema, “ukosefu wa usawa bado upo duniani .Licha ya changamoto zilizopo, Tanzania imeweza kuweka mifumo mbalimbali ya kitaifa ya kuongoza utekelezaji wa usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana.”
Marekebisho ya Baraza la Usalama
Marekebisho ya uwakilishi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni muhimu ili chombo hicho kiwe na uwakilishi sawia na pia kiwe na uhalali. Amesema marekebisho hayo ni kwa mujibu wa makubaliano ya Ezulwini na azimio la Sirte.
Miongozo hiyo ya Afrika inataka Afrika iwe na viti viwili vya kudumu kwenye Baraza la Usalama.
Hotuba pia imemulika Zimbawe ambayo bado imegubikwa na vikwazo na Tanzania imetaka kuondolewa kwa vikwazo hivyo ili kutoa fursa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na hatimaye kusongesha taifa hilo.

Kwa upande wa Maziwa Makuu, Tanzania imesema kuwa kuapishwa kwa Rais Everiste Ndayishimiye, wa Burundi mwezi Juni mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu nchini humo, kumehitimisha kile kilichosubiriwa muda mrefu ambacho ni uchaguzi, “Tanzania inasihi jumuiya ya kimataifa kuunga mkono serikali mpya kwa kupatia nchi hiyo msaada unaohitajika wa kiuchumi na kijamii li kusongesha raia wake.”
Kwa upande wa DRC, amesema Tanzania inasisitiza msimamo wake wa kusaidia ustawi, utulivu na amani nchini humo na inasisitiza msimamo wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, wa kuhakikisha kuna ushirikishwaji katika kupanga upya kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB, cha MONUSCO ili kiweze kuendeleza uwezo wake wa ulinzi na operesheni.
Ametamatisha hotuba yake kwa kusisitiza msimamo wa Tanzania katika kutoa msaada wowote kwa Umoja wa Mataifa ili kufanikisha ajenda ya dunia ikiwemo kusongesha usawa, kujitawala, amani, usalama, haki za binadamu, maendeleo, ajenda 2030 na marekebisho ya Umoja wa Mataifa.