Ushirikiano wa kimataifa ndio dawa mujarabu ya changamoto za kimataifa:UN

8 Januari 2021

Hatimaye Umoja wa Mataifa hii leo umezindua ripoti yake ya mwisho ya maoni ya wakazi wa dunia kuhusu chombo hicho kinapotimiza miaka 75 tangu kuanzishwa kwake ambapo idadi kubwa kipaumbele chao cha muda mfupi ni huduma za msingi kama vile afya, elimu, maji na huduma za kujisafi, lakini pia matarajio yao na mawazo yao katika sula zima la ushirikiano wa kimataifa na kwa Umoja wa Mataifa kwa ujumla.

Watu zaidi ya milioni 1.5 kutoka mataifa 195 walishiriki katika kampeni hiyo ya kukusanya maoni kupitia utafiti na majadiliano.

Kuhusu kilichojitokeza katika kampeni hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema“Mchakato huo wa maoni ya UN75 umeonyesha kwamba asilimia 97 ya walioshiriki wanunga mkono ushirikiano wa kimataifa katika kushughulikia changamoto za kimataifa. Na hii inaonyesha dhamira muhimu katika ushirikiano wa kimataifa na kwa lengo la Umoja wa Mataifa. Na sasa ni juu yetu nchi wanachama na sekretariati ya Umoja wa Mataifa kukidhi matarajio ya watu tyunaowahudumia.”

Changamoto za muda mfupi na muda mrefu

Washiriki wengi hususan katika nchi za kipato cha chini na kati wametaka usaidizi zaidi kwa watu walio hatarini, jambo ambalo kwa watu wa kipato cha juu, suala hilo halikupatiwa kipaumbele. 

Tishio la mabadiliko ya tabianchi na mazingira lilionekana kubwa zaidi kwa asilimia 73 ya washiriki wa utafiti kutoka Amerika Kusini na Karibea ilhali ni asilimia 37 tu ya washiriki kutoka nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara walioona kuwa hoja hiyo ni tatizo, 

Hata hivyo suala lingine ambalo kwa ujumla linatakiwa kupatiwa kipaumbele ni fursa za ajira, haki za binadamu na mizozo. Maoni hayo  yanafuatia utafiti wa miezi 12 ulioanza mwezi Januari mwaka jana ambapo Umoja wa Mataifa ulihoji wakazi wa dunia kuhusu matarajio na hofu yao juu ya mustakabali wa dunia hususan chombo hicho kilichotimiza miaka 75. 

Licha ya changamoto hizo, asilimia 49 ya washiriki wanaamini kuwa maisha yatakuwa bora mwaka 2045. 

UN Barbados and the OECS
Mwanamke kutoka St. Kitts na Nevis visiwa vya Caribbea amekamilisha kutoa maoni yake kwenye utafiti wa UN kuhusu matumaini na hofu za mustakbali wa dunia

Umoja katika makundi na kanda

Akitangaza matokeo ya utafiti na ukusanyaji wa maoni hayo kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswis hii leo Fabrizio Hochschild, mshauri maalum wa Katibu Mkuu kuhusu maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa amesema njia mbalimbali zilitumika katika kukusanya maoni na kupata tathimini ikiwa ni pamoja na majadiliano, maoni, njia mbalimbali bunifu, akili bandia, vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii.

Ameongeza kuwa mbali ya mbinu hizo pia kulifanyika tafiti mbili huru zikitumia maswali hayohayo ili kupata ukweli hali halisi na matokeo yake yalikuwa ya kusisimua na mambo yaliyojitokeza ni pamoja na masuala ya“umoja, rika, makundi katika kipato kwenye kanda mbalimbali na viwango vya elimu. Lakini maoni yalikuwa sawa lilipokuja suala la matumaini ya watu na hofu zao kuhusu mustakbali wao, pia matarajio yao katika suala la ushirikianom wa kimataifa.”

UNDP Bangladesh/Fahad Kaize
Wafanyakazi wa kijamii wanaowezeshwa na Umoja wa Mataifa, wakihamasisha umma kuhusu mbinu za kujikinga na COVID-19 na kusambaza vifaa vya kujisafi miongoni mwa kaya maskini nchini Bangladesh.

Kuhusu COVID-19

Katika vipaumbele vya haraka baada ya COVID-19 dunia imeungana katika kutaka fursa bora zaidi za kupata huduma za msingi kama za afya, elimu bora, maji na usafi na pia wanataka mshikamano zaidi na maeneo na jamii zilizoathirika vibaya zaidi.

Ukusanyaji maoni hayo wa Umoja wa Mataifa limekuwa ni moja ya zoezi kubwa na lenye matamanio zaidi kufanywa na Umoja wa Mataifa ili kupata maoni ya umma kuhusu vipaumbele kwa ajili ya kujikwamua na janga la COVID-19.

UN photo/Jean Marc Ferré
Vijana wamuuliza maswali Katibu Mkuu Antonio Guterres wakati wa mkutano wa UN75 huko Geneva

Jukumu la Umoja wa Mataifa

Washiriki wengi pia wamezungumzia kuhusu Umoja wa Mastaifa kuongoza katika ushiriukiano wa kimataifa katika kushughulikia changamoto za kimataifan za muda mrefu na za muda mfupi.

Matokeo yanaonyesha kuwa wengi pia wanataka shirika la umoja wa Mataifa kuwa bunifu, kuwa jumuishi zaidi , kuwa shirikishi, lenye kuwajibika na lenye ufanisi zaidi.

Katika utafiti huo na majadiliano ya UN75 yaliyofanyika kote duniani , washiriki wametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuwa na uongozi wa kimaadili, wenye mabadiliko na Baraza la Usalama linalozingatia matakwa ya watu linaowahudumia, na kuwa na mfumo wa Umoja wa Mataifa ambao ni shirikishi na jumuishi.

Pia wametyaka kuwe na maboresho na uelewa wa kazi za Umoja wa Mataifa miongoni mwa raia wa Dunia na shirika ambalo linaonyesha kujali zaidi mahitaji ya watu.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud