Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta binafsi nusuruni dunia dhidi ya COVID-19 - Guterres

Mchuuzi wa mtaani akipita eneo la Han Zhen jie, moja ya maeneo yenye maduka mengi huko Wuhan nchini China
Chen Liang
Mchuuzi wa mtaani akipita eneo la Han Zhen jie, moja ya maeneo yenye maduka mengi huko Wuhan nchini China

Sekta binafsi nusuruni dunia dhidi ya COVID-19 - Guterres

Afya

Sekta binafsi ina dhima muhimu katika kunasua dunia kutoka katika janga la Corona au COVID-19 na janga la mabadiliko ya tabianchi, amesema Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa wakati akihutubia hii leo jukwaa la kimataifa la kiuchumi, WEF linalofanyika kwa njia ya mtandao badala ya ilivyozoeleka huko Davos, Uswisi kutokana na janga la Corona.
 

Akihutubia kwa njia ya mtandao kutoka New York, Marekani, Bwana Guterres amesema, “tunawahitaji sasa kuliko wakati wowote ule ili kutusaidia kubadili mwelekeo, kumaliza utete unaokumba dunia, kuepusha janga zaidi la tabianchi na kujenga mustakabali sawia na endelevu tunaoutaka.”

Katibu Mkuu amehudumia jukwaa hilo wakati ambapo Umoja wa Mataifa umetoa ripoti yake mpya ya uchumi ikionya juu ya ufinyu wa kukwamuka kwa uchumi wa dunia kutokana na janga la COVID-19..

Utu umekumbwa na changamoto

Katibu Mkuu Guterres amesema utu wa binadamu umekumbwa na mwaka wa majanga ambayo katu hakuna mtu anayetaka kuona yanajirudia na bado bado majaribu yanaendelea kukumba jamii.

“Kama kuna neno moja ambalo linaweza kuainisha dunia ya leo, basi ni utete,” amesema Guterres akiongeza kuwa sasa kunashuhudiwa madhara ya janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19. Zaidi ya watu milioni mbili wamekufa na kinachoshuhudiwa ni janga baya zaidi la kiuchumi kuwahi kushuhudiwa katika karne.

Amegusia ia utete wa dunia kuhusiana na mfumo wa kudhibiti kusambaa kwa silaha za nyuklia na ongezeko la tishio la kuendelezwa kwa nyuklia na silaha za kemikali kutokana na ukosefu wa mfumo wa pamoja wa wadau kuhakikisha kuna usimamizi sawia na salama wa masuala ya kimtandao.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kwenye skrini) akihutubia mkutano wa mwaka wa jukwaa la uchumi duniani, WEF, likiratibiwa kutoka Davos-Klosters Uswisi.
World Economic Forum/Pascal Bitz
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kwenye skrini) akihutubia mkutano wa mwaka wa jukwaa la uchumi duniani, WEF, likiratibiwa kutoka Davos-Klosters Uswisi.

Wakati ni huu

Guterres amesema sasa wakati umewadia na ni wakati wa kuchukua hatua akisema, “mwaka 2021 lazima tushughulikie huu utete na kurejesha dunia katika mwelekeo sahihi. Ni wakati wa kubadili mwelekeo na kufuata mwelekeo endelevu. Tunataka ushirikiano wa kimataifa uliohamasika, jumuishi na wenye mtandao thabiti.”

Kwa mujibu wa Guterres, mwelekeo wa pamoja unaainishwa na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na kwamba kufanikisha malengo hayo “natoa wito wa makubaliano mapya ya kijamii na makubaliano mapya duniani ya kuweka fursa sawa kwa wote na kuheshimu haki na uhuru wa kila mtu.”

Amesema mkataba mpya wa kijamii unahitajika ndani ya jamii ili kuwezesha watu kuishi kwa utu.
Guterres amesema mkataba huo mpya wa kijamii baina ya serikali, wananchi, mashirika ya kiraia, sekta ya biashara na makund mengine mengi ni lazima ujumuishe ajira, maendeleo endelevu, hifadhi ya jamii na msingi wake uwe haki sawa kwa wote na fursa sawa kwa wote.

Kwa upande mwingine, amesema makubaliano mapya ya dunia, ambao ni mfumo mpya wa usimamizi duniani, lazima yatoe hakikisho ya kwamba mamlaka, utajiri na fursa vinagawanywa kwa wote na kwa usawa katika ngazi ya kimataifa.

Hata hivyo amesema katika mwelekeo wa dunia baada ya janga, njia ya haraka ya kufungua upya uchumi wa dunia ni kuhakikisha kila mtu popote alipo pale anafikiwa na chanjo dhidi ya COVID-19.

“Chanjo zinafikia haraka nchi za kipato cha ju, ilhali wale maskini zaidi duniani hawana chochote. Iwapo nchi tajiri zinafikiri kuwa zitakuwa salama zitajipatia chanjo zenyewe na kupuuza nchi maskini, hilo ni kosa. Hivi sasa kuna hatari kubwa ya virusi kubadilika na kuvifanya kuwa hatari zaidi na rahisi kusambaa na hatimaye kuwa sugu kwa chanjo zilizopo,”  amesema Katibu Mkuu.

Ni kwa mantiki hiyo ametaka hatua za haraka zichukuliwe ikiwemo kuongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa chanjo na leseni za kufanikisha hatua hizo zipatikane.

“Chanjo zinapaswa kuonekana kuwa ni bidhaa ya umma yaani chanjo ya watu,” amesema Guterres.