Mfumo wa fedha duniani umefilisika kimaadili, asema Guterres akihutubia Baraza Kuu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaja mambo makuu matano anayoona yanapaswa kupatiwa kipaumbele ili dunia iweze kuwa na mwelekeo sahihi na mustakabali bora kwa kila mkazi wake.
Maeneo hayo ni janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, marekebisho ya mfumo wa ufadhili wa fedha duniani, hatua kwa tabianchi, ukosefu wa kanuni katika masuala ya mtandao pamoja na amani na usalama na ameyafafanua wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo kuhusu vipaumbele vyake.
Guterres akifafanua hali halisi ilivyo sasa na msingi wa maeneo hayo makuu matano amesema “tumeanza tena mwaka mwingine tukikabiliwa na janga la Dunia. COVID-19 inaendelea kuvuruga maisha, mipango na matumaini. Uhakika pekee ulioko unazidi kukosa uhakika. Wakati huo huo ukosefu wa usawa unaongezeka, halikadhalika mfumuko wa bei. Janga la tabianchi, na bayonuia inatoweka. Tunakabiliwa na mlolongo wa machafuko ya kisiasa na mizozo. Ukosefu wa kuaminiana miongoni mwa mataifa makubwa umefikia kiwango kikubwa. Mifumo ya intaneti ya kasi kubwa imesheheni chuki na uongo na hvyo kupatia uhai mambo mabaya zaidi kwa binadamu.”
Katibu Mkuu amesema hali hiyo ni inafahamika kwa kila mtu na kwamba “huu si wakati wa kuorodhesha na kulalamika kuhusu changamoto, ni wakati wa kuchukua hatua. Changamoto zote hizi zimetokana na kushindwa kwa utawala bora wa dunia. Kuanzia afya duniani hadi teknolojia ya kidijitali, mifumo mingi ya ushirikiano wa kimataifa hivi sasa imepitwa na wakati na haikidhi matakwa ya sasa.”
Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametaja eneo la kwanza kuwa ni kuingia katika udharura wa kukabiliana na COVID-19 akisema “Omnicron ni onyo lingine bado na aina nyingine au lahaja nyingine ya virusi inaweza kuwa mbaya zaidi. Kukomesha kusambaa kwa COVID-19 kokote kule lazima iwe ajenda ya juu kila pahali.”
Hata hivyo amesema virusi visitumike kukandamiza haki za binadamu na kubinya fursa ya raia sambamba na uhuru wao akitolea mfano baadhi ya nchi kuwa vizuizi vya safari vyenye misingi ya kibaguzi.
Amesisitiza kuwa uamuzi wowote lazima uwe wa misingi ya kisayansi kwa kuwa sayansi iko wazi, chanjo zinafanya kazi na chanjo zinaokoa maisha. Guterres amezungumzia uwiano katika mgao wa chanjo akisema kwa sasa kiwango cha utoaji chanjo ni kikubwa nchi za kipato cha juu mara 7 zaidi ikilinganishwa na Afrika, “kwa kasi ya sasa, Afrika itafikia asilimia 70 ya utoaji chanjo mwezi Agosti mwaka 2024.”
Ametaka uzalishaji wa chanjo uongezwe sambamba na usambazaji.
Eneo la pili ni marekebisho ya mfumo wa wa fedha duniani akisema wa sasa umefilisika kimaadili ukinufaisha matajiri na kuadhibu maskini.
“Moja ya majukumu makuu ya mfumo wa fedha duniani ni kuhakikisha kuna utulivu kwa kusaidia uchumi ambao unakabiliwa na changamoto. Lakini katika changamoto za sasa za janga la Corona, mfumo huo umeshindwa kufanya hilo.” Amesema Guterres.
Kasi ya ukuaji wa uchumi kwa nchi za kipato cha chini ni kidogo mno na nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara zinaweza kushuhudia kiwango cha ukuaji uchumi katika miaka mitano ijayo ambacho ni kidogo kwa asilimia 75 ikilinganishwa na maeneo mengine ya dunia.
Ametaka marekebisho hayo yaende sambamba na marekebisho ya mfumo wa utoaji na msamaha wa madeni.
Eneo la tatu ni hatua kwa tabianchi ambako Katibu Mkuu amesema kwa mwelekeo wa sasa dunia haitaweza kufikia lengo la kupunguza ongezeko la joto kwa nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi.
“Tayari dunia yetu imepata joto kwa nyuzi joto 1.2 na madhara yake ni dhahiri. Mwaka 2020 changamoto za tabianchi zimesababisha watu milioni 30 kukimbia makwao, idadi ikiwa ni mara tatu zaidi ya wale waliofurushwa makwao kutokana na vita na ghasia.” Amesema Guterres.
Katibu Mkuu amesema kinachohitajika kupunguza kwa asilimia 45 utoaji wa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2030 ili ifikapo mwaka 2050 kusiweko na uzalishaji kabisa wa hewa ya ukaa.
Akimulika eneo la nne, Katibu Mkuu amesema ni lile ambalo halina usimamizi kabisa wa kimataifa na hilo lazima ushughulikiaji wake uwe wa dharura. Eneo hilo ni teknolojia akisema, “teknolojia isitutumie bali sisi tuitumie.”
Amesema teknolojia iwapo itatumia vizuri, manufaa yake ni ya kupindukia iwapo “tunaweza kuhakikisha usalama na uunganishaji salama wa intaneti. Lakini kupanuka kwa teknolojia kunanufaisha zaidi nguvu haribifu na kunyima fursa watu wa kawaida.”
Amesema katika nchi ambako intaneti si nzuri, shule kuunganishwa kwenye mtandao kunaweza kuongeza pato la ndani la taifa kwa asilimia 20.
Guterres amesema wanawake ndio wako nyuma zaidi kwenye kupata huduma ya mtandao na ndio maana amesema “mkutano wa mwaka huu wa viongozi kuhusu marekebisho ya mfumo wa elimu duniani utakuwa ni fursa muhimu ya kusaidia kufunga pengo la kidijitali na kuhakikisha kuna huduma ya intaneti ambayo ni salama na inapatikana kwa kila mtu.”
Akitamatisha hotuba yake, Guterres ametaja kipaumbele cha tano kuwa ni kuchukua hatua za dharura kurejesha amani katika Dunia ambamo kwayo kwa sasa ni kidogo.
“Tunakabiliwa na mizozo mikubwa zaidi tangu mwaka 1945. Mapinduzi ya kijeshi yamerejea, hifadhi ya nyuklia sasa ni imezidi 13,000, kiwango cha juu zaidi katika miongo kadhaa. Haki za binadamu na utawala wa sheria vimeshambuliwa.” Amesema Guterres.
Ametaja mizozo kuanzia Afghanistan, Sudan, Colombia, hadi Ethiopia ambako amesema kutoa hakikisho la misaada ya kibinadamu na kumaliza chuki ndio jawabu mujarabu.
“Dunia ni ndogo sana kuweza kuwa na maeneo mengi yenye mizozo. Tunahitaji Baraza la Usalama lijikite kikamilifu kushughulikia. Mgawanyiko wa kijiografia lazima usimamiwe ili kuepusha vurugu duniani,” amesema Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu amesihi nchi wanachama akisema, “hebu kwa pamoja na tufanye mwaka 2022 uwe mwaka wa kujenga njia mpya, yenye matumiani na usawa.”