Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watu bilioni 2 wanategemea vituo vya afya visivyo na huduma ya WASH:UNICEF/WHO

Muhudumu wa afya katika kituo cha afya cha Bamrasnaradura Thailand
UN Women/Pathumporn Thongking
Muhudumu wa afya katika kituo cha afya cha Bamrasnaradura Thailand

Takriban watu bilioni 2 wanategemea vituo vya afya visivyo na huduma ya WASH:UNICEF/WHO

Afya

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto duniani UNICEF la afya WHO leo yameonya kwamba ukosefu wa maji katika vituo vya huduma za afya unawaweka wafanyakazi na wagonjwa katika hatari kubwa ya maambukizi ya corona au COVID-19.

Kwa mujibu waripoti ya pamoja ya mashirika hayo iliyotolewa mjini Geneva Uswis na New York Marekani, watu karibu bilioni 1.8 wako katika hatari hiyo ya coronavirus">COVID-19 na kupata magonjwa mengine ya kuambukiza kwa sasabu vituo vya afya vinavyowahudumia havina huduma za msingi za maji.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema“Kufanyakazi katika kituo cha afya ambacho hakina maji, usafi na huduma za kujisafi ni kama kupeleka wauguzi na madaktari kufanyakazi bila kuwa na vifaa vya kujikinga PPE. Huduma ya maji, usafi na kujisafi (WASH) katika vituo vya afya ni muhimu sana katika kukomesha maambukizi ya COVID-19. Lakini bado kuna mapengo makubwa ya kuyaziba hususan katika nchi zenye maendeleo duni.”

Mtoto wa miaka 12 akinawa mikono kwa sabuni kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Afghanistan
UNICEF/Ghafary
Mtoto wa miaka 12 akinawa mikono kwa sabuni kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Afghanistan

 

Hali halisi ilivyo

Ripoti hiyo“Hatua zilizopigwa kimataifa kuhusu huduma za WASH katika vituo vya afya:mambo ya msingi kwanza”imetolewa wakati COVID-19 ikitanabaisha mapengo ya msingi katika mifumo ya afya ikiwemo hatua hafifu za kuzuia na kudhibiti maambukizi.

Huduma za maji, usafi na kujisafi ni muhimu kwa usalama wa wahudumu wa afya na wagonjwa lakini bado huduma hizi hazipewi kipaumbele duniani kote imesema ripoti hiyo ikiainisha kwamba kituo 1 kati ya 4 havina huduma za maji, huku kituo 1 kati ya 3 hakina huduma za kunawa mikono zinazotolewa, kituo 1 kati ya 10 hakina huduma za usafi na kituo 1 kati ya 3 hakitenganishi kwa usalama maji taka.

Kwa upande wake mkurtugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema“Kuwapeleka wahudumu wa afya na watu wanaohitaji matibabu kwenye vituo visivyo na maji safi, vyoo salama ayu hata sabuni za kunawia mikono ni kuweka maisha yao hatarini.  Hii ilikuwa kweli kabla ya COVID-19 lakini mwaka huuu umefanya kuwa vigumu sana kuyapuuzia mapengo haya. Wakati tukifikiria na kukutafakari Maisha baada ya COVID-19 kuhakikisha kwamba tunawapeleka kina mama na Watoto kwenye vituo vya afya vyenye huduma za kutosha za maji , usafi na kujisafi sio tu kitu ambacho tunaweza na tunapaswa kufanya lakini ni kitu ambacho ni lazima tufanye.”

Chumba cha upasuaji katika hospitali ya Bulawayo Zimbabwe
UNDP/Karin Schermbrucker
Chumba cha upasuaji katika hospitali ya Bulawayo Zimbabwe

Masikini ndio waathirika zaidi

Ripoti hiyo ya mashirika ya Umoja wa Mataifa imesema hali ni mbaya zaidi katika nchi zpte 47 zenye maendeleo dunia (LDCs) kote duniani.

Huko kituo 1 kati ya 2 vya afya havina huduma za msingi za maji ya kunywa, kituo 1 kati ya 4 havina huduma za kujisafi na vituo 3 kati ya 5 vinakosa huduma za msingi za usafi.

Hata hivyo ripoti inasisitiza kwamba hali hii inaweza kurekebishwa na inakadiria kwamba itagharimu takriban dola moja kwa kila pato la mtu kuwezesha nchi zote 47 kuanzisha huduma za msingi za maji kati vituo vya afya. Kwa wastani ripoti inasema dola 0.20 kwa kila pato zinahitajika kila mwaka kuendesha na kuendfeleza huduma hizo.

Kwa mujibu wa ripoti uwekezaji mara moja wa huduma za WASH unamanufaa makubwa, kwani kuboresha usafi katika vituo vya afya ni muhimu katika kukabiliana na usugu wa vijiuavijasumu.

Pia inapunguza gharama za huduma za afya kwa sababu inapunguza maambukizi yanayotokana na kukosa huduma hizo ambayo ni gharama kuyatibu. 

Piakunaokoa muda kwani wahudumu wa afya hawatohitaji kusaka maji kwa ajili ya kunawa mikono.Usafi bora pia unaongeza ufanisi wa huduma na hivyo kuleta faida na dola 1.5 kwa kila dola iliyowekezwa.

Ripoti imeongeza kuwa huduma hizi ni muhimu sana hususan kwa watu walio hatarini na wasiojiweza wakiwemo wanawake wajawazito, Watoto wachanga na watoto wengine kwa ujumla.

Imesisitiza kuwa kuimarisha huduma za WASH katika vituo vya afya ni muhimu zaidi hususan wakati wa kujifungua ambapo kina mama wengi na Watoto huugua na kufariki dunia, ikiwemo kutokana na hali ambazozinaweza kuzuilika kama maambukizi. 

Hivyo huduma bora za WASH zinaweza kuokoa Maisha ya mamilioni ya kina mama wajawazito na Watoto wachanga na kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa wafu.

Mwanamke na watoto wakitumia mabomba ya maji liyowekwa na UNICEF kunawa mikono  huko Embratel, makazi yasiyokuwa rasmi ya mijini huko Boa Vista, kaskazini mwa Brazil.
© UNICEF/Yareidy Perdomo
Mwanamke na watoto wakitumia mabomba ya maji liyowekwa na UNICEF kunawa mikono huko Embratel, makazi yasiyokuwa rasmi ya mijini huko Boa Vista, kaskazini mwa Brazil.

Mapendekezo ya ripoti

Ripoti imetoa mapendekezo manne

  • Kutekeleza mipango ya kitaifa kwa ufadhili unaostahili
  • Kufuatilia na mara kwa mara kutathimini hatua za kuboresha huduma za WASH, tabia na kuhakikisha mazingira wezeshi.
  • Kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ili kuhakikisha huduma endelevu za WASH na kuchagiza hulka nzuri ya usafi.
  • Kujumuisha huduma za WASH katika mipango ya kawaida ya sekta ya afya, bajeti na program ikiwemo hatua za kukabiliana na COVID-19 na juhudi za kujikwamua na janga hilo ili kuweza kutoa huduma bora.

Mkakati wa kimataifa wa WASH na wadau wa afya ripoti inasema wameonyesha mshikamano wao kwa kutaka kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya WASH katika vituo vya afya.

Hadi kufikia mwaka huu 2020 zaidi ya washirika 130 wameahidi rasilimali ambapo nchi 34 zimeahidi msaada wa fedha ambazo ni jumla yad ola milioni 125. 

Wadau hao ni pamoja na Benki ya Dunia, mkurugenzi wake wa kimataifa wa masuala ya maji Jennifer Sara amesema “Kwa mamilioni ya wahudumu wa afya kote duniani maji ni PPE. 

Ni muhimu kwamba ufadhili ukaendelea kutolewa ili kufikisha huduma za maji na usafi kwa wale walio mstari wa mbele kupambana na COVID-19.Hivyo kufadhili huduma za WASSH katika vituo vya agfya ni moja ya uwekezaji wenye gharama nafuu ambao serikali zinaweza kuufanya.

Familia zilizotawanywa wanahitaji maji, vifaa vya kujisafi ili kuweza kuepukana na COVID-19.
UNICEF Lebanon
Familia zilizotawanywa wanahitaji maji, vifaa vya kujisafi ili kuweza kuepukana na COVID-19.

Takwimu za ripoti

UNICEF na WHO wamesema ripoti hii imejumuisha takwimu zilizokusanywa kutoka nchi 165 na utafiti huo umejumuisha vituo vya afya 760,000.

Mwaka huu takwimu nyingi zaidi zimekusanywa ikilinganishwa na mwaka jana ambapo nchi zilizoshiriki zilikuwa 125 na bvituo vya afya 560,000.

Na takwimu kuhusu maendeleo ya nchi katika kutekeleza azimio la baraza la afya duniani nchi 47 zimewakilishwa. Na hii ni mara ya kwanza takwimu hizi zimekusanywa na kutathiminiwa.