Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Choo sio tu kinaokoa maisha bali kinatengeneza maisha:UN

Sunaina alikopa pesa ili kujenga choo katika kijiji chake nchini Nepal baada ya kubaini umuhimu wa choo
©WSSCC/Charles Dickson
Sunaina alikopa pesa ili kujenga choo katika kijiji chake nchini Nepal baada ya kubaini umuhimu wa choo

Choo sio tu kinaokoa maisha bali kinatengeneza maisha:UN

Afya

Vyoo vinaokoa maisha kwa sababu kusambaa kwa kinyesi cha binadamu kunasababisha maradhi mengi yanayokatili maisha ya mamilioni ya watu kila mwaka umesema Umoja wa Mataifa hii leo katika siku ya choo duniani. 

Katika taafira yake kuhusu siku hii Umoja wa huo umesema siku ya choo ambayo kila mwaka huadhimishwa 19 Novemba ni ya kuchagiza hatua madhubuti kuchukuliwa ili kukabiliana na mgogoro wa masuala ya usafi kimataifa.

Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF zinasema  kwamba watu bilioni 4.2 wanaishi bila huduma stahiki za usafi ikiwa ni sawa na nusu ya watu wote duniani na watu milioni 673 wanaendelea kujisaidia haja kubwa katika maeneo ya wazi kwa kukosa vyoo. Kaulimbiu ya mwaka ni “Choo si choo tu bali ni mwwokozi wa maisha, mlinzi wa utu na mtengenezz fursa”.

Umoja wa Mataifa unasisitiza kwamba “Uwe nani, au uwe wapi usafi ni haki yako ya binadamu” , lakini bado mamilioni wanaishi bila huduma hiyo hii leo, na kuzua maswali  mengi je watu watawezaje kujikwamua na umasiki bila kuwa na huduma za usafi? “Ni lazima tupanue wigo wa huduma za usafi wa vyoo na kutomwacha yeyote nyuma,”. Kwa wasio na huduma ya choo kama mzee huyu toka Bangladesh ni dhiki kubwa , anasema

Huduma za vyoo ni muarobaini wa kutokomeza magonjwa yaenezwayo na wadudu kama vile nzi
Fardin Waezi/UNAMA
Huduma za vyoo ni muarobaini wa kutokomeza magonjwa yaenezwayo na wadudu kama vile nzi

“Wakati mwingine duniani tunavichukulia vitu vya msingi kwa mzaha, kwa watu masikini inaanza na kitu rahisi tu kama kuwa na fursa ya choo safi na maji salama nyumbani”

Kutokuwa na huduma za kutosha za usafi knakadiriwa kusababisha wagonjwa 432,000 wa kuhara kila mwaka na chanzo kikubwa cha magonjwa kama minyoo, vikope na kichocho.

Pia takwimu za UNICEF zinaonyesha kuwa watoto karibu laki tatu wa chini ya umri wa miaka mitano miaka mitano hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya kuhara kwa kunywa maji machafu, kutokuwa na huduma za usafi na kutonawa mikono, na watoto walikoko katika maeneo yenye mizozo wako katika hatari ya kifo mara 20 zaidi ya wengine. Na athari zote hizo huzigharimu nchi nyingi karibu asilimia 5 ya pato la taifa.