Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo kimoja cha afya kati ya vinne hakina huduma ya maji-UNICEF/WHO.

Mkunga Helen Danies anazungumza na mama  katika wodi ya kinamama hospitalini
UNICEF/UN0159224/Naftalin
Mkunga Helen Danies anazungumza na mama katika wodi ya kinamama hospitalini

Kituo kimoja cha afya kati ya vinne hakina huduma ya maji-UNICEF/WHO.

Afya

Kati ya vituo vinne vya afya duniani kote, kimoja kinakosa huduma za maji, hali inayowaathiri zaidi ya watu bilioni mbili. John kibego na taarifa kamili. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya pamoja iliyotolewa usiku wa kuamkia leo mjini Geneva Uswisi na New York Marekani na shirika la afya duniani WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Ripoti hiyo ambayo imepewa jina uwepo wa maji, huduma ya kujisafi na usafi katika vituo vya afya kifupi WASH ni ya kwanza ya ukubwa wa kiasi hiki duniani ikiangazia maji, huduma za kujisafi na usafi katika vituo vya afya.

Pia ripoti hiyo imegundua kuwa kituo kimoja kati ya vituo vitano vya afya hakina huduma ya kujisafi, mathalani kukosa vyoo au kuwa na vyoo visivyokidhi kiwango, hali ambayo inawaathiri watu bilioni 1.5 duniani. Ripoti hiyo inaendelea kusema kuwa vituo vingi vya afya havina vifaa vya kusafisha mikono, kuchambua taka na hata mahali salama pa kuhifadhi taka. 

Huduma hizo ni za muhimu katika kuzuia maambukizi, kupunguza kusambaa kwa usugu wa viuavijasumu na kutoa huduma bora hususani za kujifungua salama.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesejma, “maji, huduma ya kujisafi na huduma nyingine za usafi katika vituo vya afya ni mahitaji ya msingi ya kuzuia na kudhibiti maambukizi na pia kutoa huduma bora. Vitu hivyo ni vya msingi katika kuheshimu utu na haki za binadamu za kila mtu ambaye anatafuta huduma za afya na pia kwa wahudumu wa afya wenyewe. Ninatoa wito kwa watu kokote waliko kuunga mkono hatua hii ya WASH katika vituo vya afya. Hii ni muhimu kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs”

Ripoti hiyo ya WHO na UNICEF imegundua kuwa ni nusu tu yaani asilimia 55 ya vituo vya afya katika nchi zinazoendelea, LDCs, vyenye huduma ya msingi ya maji. Inakadiriwa kuwa mtoto 1 kati ya watoto 5 wanazaliwa katika nchi zinazoendelea, na kuwa kila mwaka, wanawake milioni 17 katika nchi hizi wanajifungua katika vituo vya afya vyenye uhaba wa maji, huduma za kujisafi na usafi.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Henrietta Fore ananukuliwa akisema, “wakati mtoto anapozaliwa katika kituo cha afya ambacho kina uahaba wa maji, uhaba wa huduma za kujisafi na uhaba wa usafi, hatari ya maambukizi na kifo kwa wote mama na mtoto inakuwa kubwa. Kila tukio la kujifungua linatakiwa kusaidiwa na mikono salama, iliyooshwa kwa sabuni na maji, kutumia vifaa vya kuua wadudu na mazingira masafi.”

Hospitali ya Ash Shifa mjini Gaza
OCHA
Hospitali ya Ash Shifa mjini Gaza

Katika Kijiji kidogo cha milima kiitwacho Daroot Korgon nchini Kyrgyzstan, video ya UNICEF inamwonesha daktari mmoja tu ambaye anahudumia idadi ya watu takribani 25,000 ameshuhudia jinsi ambavyo suluhu ndogo tu inavyookoa adogo tu yanavyookoa Maisha ya vichanga kila siku.

Dkt Baktygul Pakirova anaishukuru UNICEF ilivyoisaidia hospitali anayoifanyia kazi na vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa kasi sana,“Watoto 10 hadi 15 wanazaliwa hapa kila wiki. Kama ungekuja hapa miaka 7 iliyopita ungeshuhudia hali ya kutisha. Hakukuwa na maji ya kutiririka. Madirisha yalikuwa yametengenezwa kwa mbao na yalikuwa yanaruhusu upepo kuingia ndani. Hata akina mama walikuwa wanatetemeka kwa baridi wakati wa kujifungua”

Anaendelea kueleza kuwa watoto walikuwa wanakufa kutokana na joto la chini katika miili yao, tatizo linalosababishwa na baridi kali. Kisha anaishikuru UNICEF, “shukrani kwa UNICEF tumeboresha hali katika hospital hii. Walitupa mafunzo. Walianza kwa kuunganisha mabomba na kutuunganishia maji yanayotiririka. Walitupatia vifaa vya kutengeneza joto ili kupasha joto vyumba vyetu vya kujifungulia. Walibadilisha madirisha na kuweka ya kisasa. Hivi leo idadi ya vifo vya vichanga imeshuka sana.” 

Watafiti wa WHO na UNICEF wanaeleza kuwa Zaidi ya vifo milioni moja kila mwaka vinahusishwa na ukosefu wa usafi wakati wa kujifungua. Maambuki yanafikia asilimia 26 kwa vichanga na asilimia 11 ya wakati wa ujauzito.

Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO “fikiria kujifungua au kupeleka mtoto wako mgonjwa katika kituo cha afya ambacho hakina maji salama, vyoo au vifaa vya kujisafisha mikono.  Huo ndio uhalisia kwa mamilioni ya watu kila siku. Hakuna anayetakiwa kufanya hivyo na hakuna muhudumu wa afya anayetakiwa kutoa huduma katika mazingira hayo. Kuhakikisha vituo vyote vya vina huduma msingi za maji, huduma za kujisafi na usafi, ni muhimu katika kufikia dunia ya afya, salama nay a usawa.”

Kwa mujibu wa UNICEF, vichanga 7,000 walikufa kila siku kwa mwaka 2017, kutona na hali zinazozuilika au kutibika.

Katika mkutano mkuu wa afya wa dunia utakaofanyika mwezi ujao wa Mei, serikali zitajadili maamuzi kuhusu maji, huduma za kujisafi na usafi katika vituo vya afya.