Tunahitaji kuwekeza haraka kuziba pengo la wauguzi duniani:WHO

7 Aprili 2020

Mlipuko wa virusi vya Corona COVID-19 unadhidhirisa haja ya kuimarisha jopo la wahudumu wa afya kote duniani , kwa mujibu wa ripoti mpya ya “hali ya wauguzi duniani 2020.”

Ripoti hiyo iliyotolewa leo inatoa mtazamo wa kila kuhusu kundi kubwa la wafanyakazi wa huduma za afya.

Pia ripoti hiyo imebaini mapengo makubwa yaliyoko katika kundi hilo la wauguzi na maeneo ya kuyapa kipaumbele kama uwekezaji wa elimu kwa wauguzi, ajira na uongozi kuweza kuimarisha wauguzi kote duniani ili kuboresha afya kwa wote.

Waugunzi ni zaidi ya nusu ya wahudumu wote wa afya kwa mujibu wa ripoti hiyo na wanatoa huduma muhimu katika mfumo mzima wa afya.

“Kihistoria na hata ilivyo sasa wauguzi wako msitari wa mbele kupambana na milipuko ya magonjwa ambayo inatishia afya kote ulimwenguni. Duniani kote wanadhihirishahuruma yao, uhodari na ujasiri wakati wa napopambana na janga la COVID-19. Thamani yao hivi sasa haijawahi kuonyeshwa hapo kabla.”

Umuhimu na mchango wa wauguzi

Akisisitiza umuhimu wa kundi hili la wahudumu wa afya mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO, Dkt. Tedross Adhamon amesema”Wauguzi ni uti wa mgongo wa mfumo wowote wa afya. Leo wauguzi wengi wanajikuta wako msitari wa mbele katika mapambano dhidi ya COVID-19. Na ripoti hiini kumbusho la jukumu muhimu wanalolifanya na kusisitiza kuhakikisha kwamba wanapata msaada wanaouhitaji kuhakikisha dunia inakuwa na afya.”

 

Timu ya wauguzi wa kikosi cha Indonesia kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa UNFIL wakienda kutoa huduma kwenye moja ya nyumba katika Kijiji cha Rabb Tlettine, Kusini mwa Lebanon. (12 Oktoba 2012)
Picha na UNIFIL
Timu ya wauguzi wa kikosi cha Indonesia kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa UNFIL wakienda kutoa huduma kwenye moja ya nyumba katika Kijiji cha Rabb Tlettine, Kusini mwa Lebanon. (12 Oktoba 2012)

Ripoti hiyo iliyoandaliwa kwa pamoja na WHO kwa kushirikiana na baraza la kimataifa la wauguzi (ICN) na Nursing Now imeonyesha kwamba leo hii duniani kote kuna wauguzi takriban milioni 28.

Kati yam waka 2013 na 2018 idadi ya wauguzi iliongozeka kwa milioni 4.7 lakini bado idadi hiyo inaacha pengo la kimataifa la wauguzi milioni 5.9, huku pengo kubwa likishuhudiwa katika nchi za Afrika, Kusini Mashariki mwa Asia, kanda ya Mediterranea Mashariki na Amerika ya Kusini.

Pia ripoti imeonyesha kuwa Zaidi ya asilimia 80 ya wauguzi wote duniani wanafanyakazi katika maeneo yaliyo na nusu ya watu wote wa dunia.”Na imedhihirika kuwa muuguzi 1 kati ya 8 wanafanyakazi katika nchi ambazo hawakuzaliwa  au kupatiwa mafunzo.

Uzee pia imeelezwa kuwa ni moja ya changamoto inayotishia kazi za wauguzi kwani muuguzi 1 kati ya 6 kote duniani anatarajiwa kustaafu katika miaka 10 ijayo.

Muuguzi akimkagua mtoto katika kituo cha kujifungua kwenye hospitali ya Bilaspur India Aprili 2015
UNICEF/Nguyen Tanhoa
Muuguzi akimkagua mtoto katika kituo cha kujifungua kwenye hospitali ya Bilaspur India Aprili 2015

Nini kifanyike kuepuka mtihani huo

Ili kuepuka pengo la kimataifa la wauguzi ripoti inakadiria kwamba nchi zinazokabiliwa na uhaba wa wauguzi zinatakiwa kuongeza idadi ya wauguzi wanaohitimu kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka sambamba na kuimarisha uwezo wa kuajiriwa na kusalia kwenye mifumo ya afya. Hii ripoti inasema itagharimu karibu dola 10 kwa kila mtu kwa mwaka.

“Wanasiasa wanatambua gharama ya kuwasomesha wauguzi na kuhakikisha wanasalia kwenye tasnia hiyo, lakini sasa ndio wengi wanaanza kutambua thamani yao.” amesema Annete Kennedy rais wa ICN na kuongeza kuwa “Kila senti inayowekezwa kwa uuguzi inasaidia mustakbali wa wat una familia katika njia ambazo ziko bayana kwa kila mtu.Ripoti hii inaainisha mchango wa wauguzi na kuthibitisha kwamba uwekezaji katika tasnia ya wauguzi ni faida kwa jamii na si gharama. Dunia inahitaji mamilioni mengine ya wauguzi na tunatoa wito kwa serikali kufanya lililo bora , wekeza katika tasnia hii muhimu na angalia jinsi watu wako watakavyofaidika kutokana na kazi nzuri ambayo wauguzi pekee ndio wanaoweza kuifanya.”

Mwanamke nchini India akihudumiwa na muuguzi
© UNICEF/Ashima Narain
Mwanamke nchini India akihudumiwa na muuguzi

Asilimia kubwa ya wauguzi ni wanawake

 Kwa mujibu wa ripoti hii ya leo asilimia 90 ya wauguzi wote ni wanawake lakini bado ni asilimia ndogo sana ya wauguzi wanaoshika nafasi za juu za uongozi wa sekta za afya, kwani asilimia kubwa ya nafasi hizo zinashikiliwa na wanaume.

Lakini wakati nchi zinapowawezesha wauguzi kuchukua malaka ya uongozi kwa mfano kwa kuwa na mkuu wa wauguzi wa serikali au nafasi kama hiyo na program zinazohusu wauguzi basi mazingira ya wauguzi yanaimarika.

Naye mwenyekiti mwenza wa Nursing Now Lord Nigel Crip amesema “Ripoti hii inatoa takwimu zinazohitajika na Ushahidi  kwa ajili ya wito wa kuimarisha uongozi wa wauguzi, kuimarisha kazi zao na kusomesha kundi la wauguzi kwa ajili ya siku za usoni. Chaguo la sera ni hatua ambayo tunaamini nchi zinaweza kuchukua katika miaka 10 ijayo kuhakikisha kuna wauguzi wa kutosha katika nchi zote na kwamba wauguzi wanatumia elimu yao, mafunzo na ujuzi wao kuimarisha huduma za msingi za afya na kukabiliana na majanga ambayo ni dharura ya afya kama COVID-19. Hii inapaswa kuanza kwa mtazamo mpana na majadiliano ya sekta mbalimbali ambazo zinawaweka wauguzi katika mfumo mzima wa fya , ajira za afya na vipaumbele vya afya.”

Mapendekezo ya WHO na wadau

Ili kuweza kukidhi haja ya wauguzi wanaohitajika duniani WHO na wadau wamependekeza yafuatayo kwa nchi zote

 • Kuongeza fedha kwa ajili ya kuwaelimisha na kuajiri wauguzi Zaidi
 • Kuimarisha uwezo wa kukusanya, kutathimini na kuchukua hatua dhidi ya takwimu kuhusu wahudumu wa afya
 • Kufuatilia uhamaji wa wauguzi na kudhibiti kwa makini na kwa kuzingatia maadili
 • Kuwasomesha na kuwapa mafunzo wauguzi ya kisayansi, kiteknolojia na stadi za kijamii wanazohitaji kueta maendeleo katika huduma za msingi za afya.
 • Kuanzisha nafasi za uongozi ikiwemo muuguzi mkuu wa serikali na kusaidia maendeleo ya uongozi miongoni mwa wauguzi chipukizi
 • Hakikisha kwamba wauguzi katika timu za wahudumu wa afya wa msingi wanafanyakazi na kufikia uwezo wao wote kwa mfano katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
 • Kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo kupitia viwango salama vya wafanyakazi, mishahara ya kuridhisha na kuheshimu haki za kazi za afya na usalama.
 • Utekelezaji wa sera zinazozingatia masuala ya kijinsia katika sera za wauguzi
 • Boresha kanuni ziendane na wakati kwa kinua kiwango cha elimu na viwango vya kazi kwa kutumia mifumo ambayo inaweza kutambua kuendesha mchakato wa ujuzi wa wauguzi kote duniani.
 • Imarisha jukumu la wauguzi katika timu za kutoa huduma kwa kuzileta pamoja sekta zingine tofauti kama elimu, afya, uhamiaji, fedha na ajira pamoja na wadau wa uuguzi kwa ajili ya majadiliano ya sera na mipango ya wafanyakazi.
  Ujumbe wa ripoti hiyo uko bayana “serikali zinahitaji kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa kusomesha wauguzi , kuunda ajira za wauguzi na uongozi. Bila wauguzi, wakunga na wahudumu wengine wa afya nchi haziwezi kushinda vita dhidi ya magonjwa ya milipuko au kufikia huduma za afya kwa wote na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
   

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter