Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa mara ya kwanza hakuna kisa kipya cha Ebola DRC katika siku 7 zilizopita- WHO

Wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu wakijiandaa kwa mazishi salama ya mgonjwa wa Ebola. (Agosti 2019)
UN Photo/Martine Perret
Wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu wakijiandaa kwa mazishi salama ya mgonjwa wa Ebola. (Agosti 2019)

Kwa mara ya kwanza hakuna kisa kipya cha Ebola DRC katika siku 7 zilizopita- WHO

Afya

Huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hakuna kisa chochote cha Ebola kilichoripotiwa katika siku 7 zilizopita, na hii ni mara ya kwanza tangu mlipuko wa Ebola mwezi Agosti mwaka 2018 nchini humo.

Shirika la afya  ulimwenguni, WHO linasema kuwa “haya ni mafanikio makubwa kwa kuwa tangu tarehe 19 hadi 25 ya mwezi huu hakuna kisa kipya cha Ebola kilichothibitishwa. Kisa cha mwisho kabisa kiliripotiwa kwenye ukanda wa afya wa Beni jimboni Kivu Kaskazini tarehe 17 mwezi huu wa Februari.”

Hata hivyo WHO inasema kuwa licha  ya kutokuwepo kwa kisa kipya cha Ebola katika kipindi hicho cha siku 7 , mlipuko wa Ebola bado uko hai na hatari za visa vipya kupatikana ni kubwa.

WHO imesema pamoja na kuimarishwa kwa operesheni za ufuatiliaji katika maeneo hatari zaidi, maambukizi nje ya maeneo hayo hayawezi kuenguliwa.

WHO inasema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa katika tukio moja wakati wa mlipuko wa sasa, mgonjwa wa Ebola aliyepona alionyesha tena dalili za ugonjwa huo, alifuatiliwa na kuibua mnyororo mpya wa maambukizi ambao ulichukua miezi kadhaa kuibuka.

Kwa mantiki hiyo, shirika hilo limesema kuwa ili kupunguza uwezekano wa kuibuka tena kwa mlipuko, ni muhimu kuendeleza hatua za sasa za kubaini na kuchukua hatua haraka dhidi ya visa vipya na kupatia kipaumbele cha kusaidia manusura na kuwasaidia sambamba na vikundi vya wale waliopona ugonjwa huo.

Ukata ukibisha hodi, WHO imesema kuwa ili kuendeleza operesheni za sasa , fedha zaidi zinahitajika ambapo mahitaji ya fedha kwa operesheni hizo kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu n idola milioni 83.

Mchango wa wahisani umefanikisha kiasi cha fedha na kinachohitajika sasa ni dola milioni 40 ili kusongesha operesheni na kutokomeza kabisa ugonjwa huo na kujenga mifumo thabiti ya afya.

Tangu kuibuka kwa Ebola hadi tarehe 25 mwezi huu wa Februari, visa 3444 vya Ebola vimeripotiwa kati  ya hivyo vilivyothibitishwa ni 3310.

Wagonjwa waliofariki dunia ni 2264 sawa na asilimia 66.