Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjamzito aliyepona Ebola DRC ajifungua mtoto asiye na Ebola, madaktari wastaajabu!

Mhudumu wa afya anayehusika na ebola akimchunguza ugonjwa huo mtoto mchanga mwenye umri wa wiki moja kwenye hema maalum la kituo cha matibabu dhidi ya ebola huko Beni jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC Desemba 3, 2018
UNICEF/Guy Hubbard
Mhudumu wa afya anayehusika na ebola akimchunguza ugonjwa huo mtoto mchanga mwenye umri wa wiki moja kwenye hema maalum la kituo cha matibabu dhidi ya ebola huko Beni jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC Desemba 3, 2018

Mjamzito aliyepona Ebola DRC ajifungua mtoto asiye na Ebola, madaktari wastaajabu!

Afya

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC madaktari wamestaajabu baada ya mjamzito aliyepona ugonjwa wa ebola kujifungua salama mtoto wake ambaye hajaambukizwa ugonjwa virusi vya ugonjwa huo. Arnold Kayanda na ripoti kamili.

Mjini Beni, jimbo la Kivu Kaskazini, kitovu cha mlipuko wa ebola, tupo katika moja ya vituo vya kutibu wagonjwa. Anaonekana Josephine Ekoli akiwa amembeba mwanae mchanga, ana umri wa siku tano tu, amepatiwa jina Sylvana.

Josephine akiwa na tabasamu kwenye kituo hiki kinachosaidiwa na shirika la afya ulimwenguni, WHO,  tangu mwezi uliopita, anasema..

 “Unapaswa kuwa mwangalifu, nimejifungua salama, nashukuru Mungu kwa kuniwezesha. Hivi sasa ninapona na sina ugonjwa wowote na mwanangu alizaliwa na afya.  Nashukuru wahudumu wa afya. Akina mama hawapaswi kuwa na hofu ya kufa kwa magonjwa. Wahudumu wanafanya kazi nzuri katika hospitali na kliniki.”

Kiwango cha kupona kwa wajawazito wenye ebola pamoja na watoto wanaojifungua kwa  kawaida ni cha chini na kituo hiki kimekuwa kinawafuatilia kwa muda manusura wa ebola ambao wamebeba ujauzito, anasema Dkt. Susan McLellan anayehusika na usimamizi wa wagonjwa.

WHO inasema kwa kawaida watoto wanaozaliwa na mama wenye ebola mara nyingi huzaliwa tayari wameambukizwa ugonjwa huo na mara nyingi hufariki dunia.

Hata hivyo katika mlipuko huko Beni, kutokana na malezi kwa watoto wachanga, idadi kubwa wamepona na wanasema Sylvana ni mtoto wa kwanza kuzaliwa na manusura wa ebola bila kuwa ameambukizwa kirusi hicho. Dkt. Junior Ikomo kutoka taasisi ya ALIMA ambayo ndio inasimamia kituo hiki anasema…

“Tulichunguza damu ya mtoto, tukachukua sampuli kutoka kwa mama mzazi na pia tukapima majimaji ya mfuko wa uzazi, tukihofu pengine kuna virusi. Baada ya uchunguzi wa kina majibu yalionesha hakuna virusi. Hii ndio sababu hata sisi wenyewe tunastajabu na kushangaa kwa mtazamo wa kisayansi.”