Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kati ya Januari 1 na 7 kuna visa vipya 12 vya Ebola:WHO

Mhudumu wa afya wa Ebola akionesha ishara kuwa watu wa DRC hawapaswi kuwaogopa madaktari isipokuwa ugonjwa wenyewe wa Ebola (aGOSTI 2019)
UN Photo/Martine Perret
Mhudumu wa afya wa Ebola akionesha ishara kuwa watu wa DRC hawapaswi kuwaogopa madaktari isipokuwa ugonjwa wenyewe wa Ebola (aGOSTI 2019)

Kati ya Januari 1 na 7 kuna visa vipya 12 vya Ebola:WHO

Afya

Shirika la afya duniani WHO leo Ijumaa limethibitisha kwamba kuna visa vipya 12 vya Ebola vilivyoripotiwa kati ya Januari Mosi na Januari 7 mwaka huu katika mlipuko unaoendelea kwenye jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Visa hivyo vya juma hili vimeripotiwa katika vituo tisa vya afya katika kanda nne , na kisa kipya kilichoripotiwa mjini Beni kinahusishwa na mnyororo wa maambukizi ambayo yalianzia katika eneo la afya la Aloya  kwenye kanda ya afya ya Mabalako.

Kwa mujibu wa shirika la WHO hadi kufikia Januari 7 mwaka huu jumla ya visa vilivyoripotiwa ni 3392, ikiwemo visa 3274 vilivyothibitishwa, 118 vinavyoshukiwa na jumla ya vifo 2235.

Katika visa vyote vilivyothibitishwa na kushukiwa WHO inasema wanawake ni asilimia 56, watoto wa chini ya umri wa miaka 18 ni asilimia 28 na asilimia 5 ya visa vyote ni wahudumu na wafanyakazi wa afya.