Hatujasitisha huduma zetu DRC- WFP

20 Novemba 2018

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema linaendelea na mgao wa chakula na usambazaji wa vifaa kwenye maeneo yaliyokumbwa na mlipuko wa Ebola huko Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Msemaji wa WFP  huko Geneva, Uswisi, Herve Verhoosel amesema hay oleo akizungumza na waandishi wa habari kufuatia ripoti zilizokuwa zinadai kuwa shirika hilo limesitisha operesheni zake kufuatia shambulio la Ijumaa dhidi ya hoteli moja ambamo watendaji wa shirika hilo walikuwa wanaishi.

Hoteli hizo zilikuwa zinatoa huduma za malazi kwa watendaji wa WFP na watumishi wengine wa Umoja wa Mataifa na walinda amani na hakuna hata mmoja ambaye alijeruhiwa.

Bwana Verhoosel amesema, “hatuwezi kukatiza operesheni zetu za kuokoa Maisha. WFP inasaidia operesheni za matibabu kwa kuwapatia wahusika usafiri, usambazaji na uhifadhi wa vifaa vya matibabu, kujenga vyumba salama kwa ajili ya watoa huduma za misaada. Tunagawa pia chakula kwa watu waliosajiliwa wakati wa kampeni dhidi ya Ebola kama njia mojawapo ya kudhibiti mienendo ya watu na hivyo kuzuia kuenea kwa Ebola.”

Wakati huu ambapo WFP imesema inaendelea na mgao wa chakula kwa familia, mgao unaofanyika  nyumba kwa nyumba, pia imejipanga kuchukua hatua zozote za haraka iwapo kutakuwepo na mlipuko wowote wa Ebola nchini DRC, hususan maeneo ya mijini.

Bwana Verhoosel ametumia fursa ya mkutano wa leo na waandishi wa habari kulaani vikali ghasia yoyote kwenye eneo hilo, ghasia ambazo amesema zinaweza kukwamisha operesheni za misaada ya kibinadamu zinazolenga kudhibiti kuenea kwa virusi vya Ebola.

Halikadhalika ametaka pande husika kuheshimu sheria za kibinadamu za kimataifa.

Kwa mujibu wa WFP, takribani wafanyakazi wote 400 wa Umoja wa Mataifa walioko Beni kama sehemu ya operesheni dhidi ya Ebola, wanaendelea na kazi yao.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter