Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO imehimiza umuhimu wa serikali kudhibiti virusi vya corona.

Mfano wa virusi vya corona
Centers for Disease Control and Prevention
Mfano wa virusi vya corona

WHO imehimiza umuhimu wa serikali kudhibiti virusi vya corona.

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO leo Jumatatu limehimiza umuhimu wa serikali kuendelea kuweka kipaumblele katika kuzuia na kudhibiti virusi vya corona.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus baada ya kuelezea kuhusu maambukizi ya watu wasio na historia ya kusafiri China kwa mfano kisa cha Ufaransa na kile kilichoripotiwa Uingereza kama kiashiria cha changamoto kubwa zaidi, ama ameonnya licha ya kwamba kusambaa kwa ugonjwa kunaonekana kuwa na kasi ndogo, huenda hali ikabadilika.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, “ugunduzi wa visa vichache huenda ikawa cheche ambazo zitakuwa mtoto mkubwa lakini kwa sasa ni cheche tu. Lengo letu kwa sasa ni udhibiti na tunatoa wito kwa nchi kutumia fursa hii ili kuzuia moto mkubwa.

Kufikia saa kumi na mbili alfajiri saa za Geneva kulikuwa na visa 40,235 vilivyothibitishwa nchini China na vifo 909. Nje ya China, kuna visa 319 katika nchi 24 na kifo kimoja.

WHO imesema taswira ya maambukizi haijabadilika. Asilimia 99 ya visa vimeripotiwa nchini China na vingi sio vya dharura. Takriban asilimia 2 ya visa ni vya dharura, ambayo ni kubwa kwa mujibu wa WHO.

Kwa sasa timu ya awali ya wataalamu ya WHO imewasili China kwa ajili ya kufanya maandalizi kuwasili ya timu kubwa ya kimataifa.

Kama sehemu ya maandalizi, WHO inafanya juhudi kuimarisha uwezo wa maabara kufanya uchunguzi ambapo shiirka hilo limesema nchi hazina tarifa kuhusu upana wa tatizo na ni nani aliye na virusi vya corona au ugonjwa mwingine wenye dalili kama hizo.

WHO imesema imetambua maabara 168 kote ulimwenguni zilizo na teknolojia inayohitajika kufanya uchunguzi wa virusi vya corona na kwamba wametuma vifaa vya kufanyia uchunguzi virusi vya corona nchini Cameroon, Cote d’Ivoire, nchini Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo, DRC, Misri, Ethiopia, Gabon, Ghana, Iran, Kenya, Morocco, Nigeria, Tunisia, Uganda na Zambia. Nyingi ya nchi hizo tayari zimeanza kutumia vifaa hivyo.

Shehena nyingine ya vifaa 150,00 vya uchunguzi vinawekwa pamoja mjini Berlin na zinatarajiwa kutumwa kwa maabara 80 katika kanda zote. Wiki iliyopita kituo cha magonjwa yanayoambukiza barani Afrika walitoa mafunzo kwa nchini 12 nchini Senegal kwa kutumia vifaa vilivyotumwa na WHO ambapo mafunzo mengine yatatolewa Afrika Kusini wiki ijayo.

WHO itaendelea kufanya kazi na nchi zote kwa ajili ya kuzuia na kuchunguza kwa haraka visa vipya vya virusi vya corona wka ajili ya kuokoa maisha.