Vizuizi vya COVID-19 vikilegezwa, tujiandae kukabili changamoto – WHO

12 Mei 2020

Idadi ya watu waliougua ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 ikifikia zaidi ya milioni 4 duniani kote, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO limesema kuwa hatua za baadhi ya nchi kulegeza  masharti ya watu kubakia majumbani imeonesha baadhi ya changamoto zitakazokabili mataifa siku za usoni.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo mjini Geneva, Uswisi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika moja ya mikutano yake ya kutoa muhtasari wa hali ya COVID-19 duniani. Dkt. Ghebreyesus amesema kuwa,  “mwishoni mwa wiki tumeona dalili za changamoto zinazoweza kutukabili. Nchini Korea Kusini, baa na vilabu vya usiku vilifungwa tu baada ya mgonjwa wa Corona kusababisha watu aliokuwa amekutana nao wafuatiliwe. Huko Wuhan nchini China, wagonjwa wapya kubainika tangu kuondolewa kwa vizuizi walibainika. Ujerumani nako wameripoti ongezeko la wagonjwa tangu vizuizi kulegezwa. Bahati nzuri mataifa haya matatu yana mifumo ya kubaini na kushughulikia wagonjwa.”

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amezungumzia pia uamuzi wa baadhi ya nchi kutaka kufungua shule ili watoto warejee kwenye mafunzo ambapo amesema,“kuhusu watoto kwenda shule, waamuzi lazima waangalie idadi ya mambo kadhaa pindi wanapofikia uamuzi wa kufungua au kutofungua shule. Kwanza, uelewa wa dhati kuhusu maambukizi ya sasa ya COVID-19 na kiwango cha athari za virusi hivyo kwa watoto, pili mwenendo wa COVID-19 kule ambako shule inapatikana lazima ufahamike. Tatu, uwezo wa kudhibiti COVID-19 na mikakati ya kukinga watoto shuleni.”

Dkt, Tedros amepongeza nchi ambazo zimetumia kipindi cha watu kubakia majumbani kama njia ya kuimarisha mbinu za upimaji, ufuatiliaji, kuwatenga na kuhudumia wagojwa, njia ambazo amesema ni muhimu katika kukabili kasi ya virusi vya Corona na hivyo kupunguza mzigo kwa mfumo wa afya.

Amesema ni wazi kuwa vizuizi vimekuwa na athari katika njia za watu kujipatia kipato, hivyo ulegeaji wowote wa vizuizi hivyo ni lazima uende sambamba na kuwa macho ili kuhakikisha mbinu za kulinda kipato zinakwenda sambamba na mbinu za kutunza afya.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud