Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 86 waambukizwa Ebola nchini DRC kila wiki- WHO

Shirika la wasamaria wema lisilo la kiserikali likijenga kituo cha matibabu ya Ebola huko Ituri mashariki mwa DRC mwezi Januari 2019.
WHO/Lindsay Mackenzie
Shirika la wasamaria wema lisilo la kiserikali likijenga kituo cha matibabu ya Ebola huko Ituri mashariki mwa DRC mwezi Januari 2019.

Watu 86 waambukizwa Ebola nchini DRC kila wiki- WHO

Afya

Maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC yameendelea wiki hii katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri kwa wastani wa wagonjwa 86 kila wiki, ikiwa ni sawa na wiki zilizotangulia.

 

 

Shirika la afya ulimwenguni, WHO, kupitia taarifa yake ya wiki kwa wiki imesema hata hivyo hakuna kisa chochote kilichoripotiwa nje ya DRC.

WHO inasema katika siku 21 zilizopita yaani kuanzia tarehe 17 Julai hadi tarehe 6 mwezi huu wa Agosti wagonjwa wapya 257 waliripotiwa na kuthibitishwa kuwa na Ebola.

Kati yao yao 116 walitoka mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini, wakifuatiwa na 58 mjini Mandima jimbo la Ituri.

Hata hivyo hakuna mgonjwa aliyeripotiwa kutoka mji wa Goma, tangu ripoti ya awali ambapo kuliripotiwa wagonjwa wanne ambapo kati yao hao wawili walifariki dunia na wengine wawili wanapata matibabu kwenye kituo cha afya cha kutibu Ebola.

Shirika hilo la afya linasema kuwa watu wengine 232 ambao walikuwa na makaribiano na wagonjwa kwenye eneo la Nyiragongo, jimboni Kivu Kaskazini hivi sasa wanafuatiliwa kwa karibu.

Halikadhalika chanjo dhidi ya Ebola inaendelea kupatiwa  ikiwemo asilimia 98 ya wanaoshukiwa kuwa karibu na wagonjwa wameshachanjwa.

Hadi tarehe 6 mwezi huu wa Agosti, jumla ya visa 2781 vimeripotiwa tangu kulipuka kwa ugonjwa huo Kivu Kaskazini mwezi Agosti mwaka jana na kati ya visa hivyo wagonjwa 1866 waliothibitishwa wamefariki dunia.