Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndani ya siku 4 watu 27 wathibitika kuwa na Ebola DRC

Kituo cha matibabu ya Ebola katika Hospitali mjini Beni, jimboni Kivu ya kaskazini, DRC.
MONUSCO/Alain Coulibaly
Kituo cha matibabu ya Ebola katika Hospitali mjini Beni, jimboni Kivu ya kaskazini, DRC.

Ndani ya siku 4 watu 27 wathibitika kuwa na Ebola DRC

Afya

Shirika la afya duniani, WHO limesema katika siku nne zilizopita, watu wengine 27 wamethibitika kuwa na virusi vya Ebola huko jimbo la Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema wagonjwa 24 kati ya hao 27 wanatokea eneo la Beni na watatu wanatoka Butembo.

Miongoni mwa wagonjwa hao wapya, 17 wanafahamika kuwa na makaribiano na wagonjwa ambao awali walikuwa wamethibitishwa kuwa na Ebola.

Muhudumu mmoja wa afya kutoka katika kituo kimoja cha afya mjini Beni ni mmoja wa wagonjwa wapya na mpaka kufikia sasa ni wahudumu wa afya 21 ambao wameambukizwa, watatu kati yao wakiwa wameshapoteza maisha.

Hata hivyo WHO inasema matukio ya ukosefu wa usalama katika wiki za hivi karibuni  yaliyotokana na mapigano kati ya waasi na vikosi vya serikali vya DRC yakisababisha vifo vya wananchi na magari ya msaada kupigwa mawe, yamekuwa pia kikwazo kikubwa katika shughuli ya kupambana na Ebola.

Aidha taarifa hii imeendelea kueleza kuwa matukio haya yametokea katika kipindi ambacho kuna maambukizi makubwa ya virusi vya Ebola katika mji wa Beni lakini pia WHO inasema Wizara ya Afya ya DRC, WHO yenyewe pamoja wadau wanaongeza nguvu kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo na hasa WHO ikiwa na kikosi chake cha zaidi ya wafanyakazi 250.

WHO inasema hadi tarehe 23 mwezi huu wa Oktoba watu 124 wamefariki dunia kutokanana Ebola jimboni Kivu Kaskazini na Ituri.

Hatari ya mlipuko wa ugonjwa huo kusambaa katika maeneo mengine ya DRC na pia katika nchi zilizoko jirani bado ni kubwa kwa mujibu wa shirika la afya duniani.

Kutokana na mlipuko wa ugonjwa huu wa juma lililopita, tahadhari zimtolewa katika nchi za Mauritania, Sudan Kusini, Sudan, Uganda na Tanzania.