Ghasia Beni zasababisha WFP kusitisha kwa muda mgao wa msaada

29 Novemba 2019

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesitisha kwa muda usambazaji wa misaada ya kibinadamu huko Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kutokana na mashambulizi yaliyoripotiwa kwenye maeneo yenye mlipuko wa Ebola. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo, msemaji wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP Hervé Verhoosel, amesema kuwa wamechukua hatua hiyo kwa sababu wafanyakazi wa shirika hilo pamoja na wale wa wadau wao hawana uhakika wa usalama wao na kwamba kuna ugumu kufikia maeneo ambako misaada inapaswa kupelekwa.

Amesema kwamba kutokana na hali hiyo wana hofu kuwa hali ya kibinadamu itakuwa mbaya kutokana na watu wengi kuwa na uhitaji wa misaada.

Mvutano mjini Beni umekuwa ukiongezeka kila uchao tangu kuanza kwa operesheni iliyoongozwa na serikali ya DRC dhidi  ya kikundi cha waasi cha ADF tarehe 30 mwezi uliopita wa Oktoba.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR Charlie Yaxley amesema kuwa vikundi vilivyojihami vimekuwa vikilenga raia na wakimbizi wa ndani kwenye eneo hilo na kusababisha vifo vya watu kadhaa huku wengine wakinasa katiakti ya mapigano, “UNHCR na wadau wake wanatoa wito wa kurejeshwa haraka kwa usalama ili mashirika ya kibinadamu yaweze kufikia raia na kuwapatia misaada. Mamia ya watu  hivi sasa wanalala kwenye makanisha na shule.”

Kwa mujibu wa UNHCR, mji wa Beni ni makazi ya watu 500,000 na kwamba hivi sasa watu wapatao 250,000 wamekimbia makazi yao na  hali zao ni mbaya.

Takribani watu 100 wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi kwenye eneo hilo la Beni tangu tarehe 2 mwezi huu wa Novemba.

Kutokana na mashambulizi hayo kwenye maeneo yenye Ebola, shirika la afya  ulimwenguni, WHO linasema kuwa kiwango cha ufuatiliaji wa watu wenye Ebola kimepungua kutoka asilimia 86 hadi 59 tangu mwanzoni mwa wiki hii na kwamba theluthi moja ya wahudumu  wa Ebola huko Beni wamehamishiwa kwa muda mjini Goma.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud