Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yasindikiza watoa huduma dhidi ya Ebola, DRC

Timu ya kutoa chanjo dhidi ya Ebola iliyopiga kambi huko kijiji cha Iboko, wakiwa na pipa lenye chanjo wakielekea eneo la Bisolo. Hii ni tarehe 20 juni 2018
WHO/Lindsay Mackenzie
Timu ya kutoa chanjo dhidi ya Ebola iliyopiga kambi huko kijiji cha Iboko, wakiwa na pipa lenye chanjo wakielekea eneo la Bisolo. Hii ni tarehe 20 juni 2018

MONUSCO yasindikiza watoa huduma dhidi ya Ebola, DRC

Afya

Msafara wa wahudumu wa afya wanaokabiliana na ugonjwa wa Ebola huko jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wamelazimika kuambatana na msafara wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa ili kuweza kufikia mji wa Oicha ambako kisa kipya cha Ebola kimeripotiwa.

Mkurugenzi wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, anayehusika na masuala ya dharura, Dkt. Peter Salama amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi.

Dkt. Salama akafanua kisa hicho kilichoripotiwa Oicha, mji ulioko kilometa 30 kutoka Beni..

(Sauti ya Dkt. Peter Salama)

“Kisa hicho ambacho bado hakijathibitishwa kinaweza kuwa daktari kutoka Oicha ambaye alilazwa katika hospitali mjini Oicha na pengine alimuambukiza mke wake.”

Hivyo akasema ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO umesaidia..

(Sauti ya Dkt. Peter Salama)

“Timu yetu imechukua hatua wiki hii. Walilazimika kufika Oicha wakisindikizwa na MONUSCO. Walipofika Oicha waliweza kutembea bila ulinzi wowote kwa kuwa mji wenyewe ni salama. Tumeandikisha watu 90 ambao walikuwa na uhusiano na washukiwa wa Ebola na chanjo ilianza na inaendelea.”

Kuhusu chanjo, mkurugenzi huyo wa WHO amesema wanazo za kutosha.

Kwa mujibu wa Dkt. Salama, Oicha ni mji ambao umezingirwa na kikundi cha waasi cha IDF na kwamba kikundi hicho kinashikilia mateka wafanyakazi wa mashirika ya kiraia.

Hadi sasa kumeripotiwa visa 103 vinavyoshukiwa kuwa ni vya Ebola huko jimboni Kivu Kaskazini,ambapo kati ya wagonjwa hao 63 wamefariki dunia.

WHO inasema asilimia 80 ya wagonjwa wa Ebola na vifo ni katika mji wa Mangina ambao ndio kitovu cha mlipuko huo ulioanza mwezi uliopita.

 

TAGS: WHO, Dkt. Peter Salama, Ebola, Oicha, Kivu Kaskazini