Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa usawa India moja ya sababu za kiwango cha juu cha utapiamlo- Ripoti

Mtoto mchanga wa umri wa siku mbili akiwa amelala pembezoni mwa mama yake katika wodi ya wazazi huko Rajasthan India.
UNICEF/Prashanth Vishwanathan
Mtoto mchanga wa umri wa siku mbili akiwa amelala pembezoni mwa mama yake katika wodi ya wazazi huko Rajasthan India.

Ukosefu wa usawa India moja ya sababu za kiwango cha juu cha utapiamlo- Ripoti

Afya

Viwango vya utapiamlo nchini India ni vya juu kuliko kiwango kinachoweza kuvumilika, imesema ripoti mpya ya uchambuzi wa chakula na uhakika wa chakula iliyotolewa leo kufuatia utafiti wa pamoja kati ay serikali ya India na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP.

Ripoti hiyo inasema miongoni mwa watu wote bilioni 1.32 nchini India walio hatarini zaidi kutokana na viwango hivyo vya juu vya utapiamlo ni wanawake na watoto, ikielezwa kuwa wana uhaba wa vitamin  na madini ya joto au aidini.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo,Herve Verhoosel ambaye ni msemaji wa WFP mjini Geneva, Uswisi amesema kwa kuzingatia idadi ya watu wa India, hali hiyo ya ukosefu wa lishe bora itakuwa na athari kwenye mafanikio ya dunia ya kutekeleza lengo namba 2 la malengo endelevu kuhusu kutokomeza njaa.

Ametolea mfano suala la udumavu akisema nalo ni tatizo kwa kuwa kiwango cha kupungua kwa udumavu ni cha chini ikilinganishwa na mataifa mengine yanayoibuka kiuchumi.

“Kwa kiwango cha sasa cha udumavu cha zaidi ya asilimia 30 kwenye majimbo yote ya India isipokuwa Kerala ambalo tayari limefikia lengo, serikali ya India italazimika kuongeza maradufu kiwango cha kupunguza udumavu hadi asilimia 2 kwa mwaka ili kukidhi kiwango cha kitaifa cha asilimia 25 ifikapo mwaka 2022,” amesema Bwana Verhoosel.

Msemaji huyo wa WFP ameonya kuwa iwapo kiwango cha sasa cha kupunguza udumavu cha asilimia 1 kikiendelea, “hii ina maana kuwa tutakuwa na zaidi ya asilimia 31 ya watoto wadumavu ifikapo mwaka 2022.”

WFP inasema ingawa India imefikia kiwango cha kujitegemea katika kuzalisha mchele, ngano na nafaka nyingine, “bado ongezeko hilo halijaweza kumfikia mwananchi mmoja mmoja kutokana na ukosefu wa usawa, ongezeko la idadi ya watu, upotevu wa chakula kwenye mavuno na uuzaji nje nafaka hizo.”