Utapiamlo kwa watoto umefurutu ada Afghanistan:UNICEF/WFP 

Wasichana wakicheza kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani nje ya mji wa Herat Afghanistan
© UNICEF/Sayed Bidel
Wasichana wakicheza kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani nje ya mji wa Herat Afghanistan

Utapiamlo kwa watoto umefurutu ada Afghanistan:UNICEF/WFP 

Msaada wa Kibinadamu

Hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula na vita nchini Afghanistan vimeongeza mara dufu tatizo la utapiamlo kwa watoto na kuzusha wasiwasi mkubwa kwa hatama ya watoto hao na familia zao yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na la mpango wa chakula duniani WFP ambayo sasa yametoa wito wa mshikamano kunusurua taifa hilo.

Katika hospital kuu ya Herat nchini Afghanistan watoto wakiwa kwenye wodi maalum za utapiamlo. Hali ni mbayá na mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistan Hervé Ludovic De Lys, na mwakilishi wa WFP Mary-Ellen McGroarty ambao wamefanya ziara ya siku mbili kujionea hali halisi wanasema bila upatikanaji wa huduma za maji za kuaminika, chakula,huduma za msingi za afya na huduma za lishe watoto wa taifa hili na familia zao wanaweka rehani maisha yao.

Watu milioni 14 wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na uhakika wa chakula na watoto wanaokadiriwa kuwa milioni 3.2 wenye umri wa chini ya miaka 5 wanatarajiwa kupata unyafuzi ifikapo mwishoni wa mwaka huu, huku takribani watoto milioni moja wako katika hatari ya kufa na utapiamlo uliokithiri endapo hawatopata matibabu ya haraka.

Taarifa ya pamoja ya viongozi hao imeonya kwamba familia nyingi zinahaha kuweka mlo mezani, afya ya kina mama na watoto inaendelea kuzorota kila uchao, na milipuko ya magonjwa kama surua na kuhara vitaongeza madhila.

Maafisa wa UNICEF na WFP wakizuru maeneo ya kuchezea watoto kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani nje ya mji wa Herat Afghanistan
© UNICEF/Sayed Bidel
Maafisa wa UNICEF na WFP wakizuru maeneo ya kuchezea watoto kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani nje ya mji wa Herat Afghanistan

Utafiti wa WFP unaonyesha asilimia 95 ya kaya nchini Afghanistan watu wazima hawapati chakula cha kutosha na wnapunguza idadi ya milo ili kuwaachia watoto wao chakula hicho.

Sasa Umoja wa Mataifa na washirika wake wamechukua hatua, katika vituo vya kugawa chakula  vya WFP na mashirika mengine ya umoja wa Mataifa misururu ni mirefu ya kupokea mgao kwani familia nyingi zimeathirika pia na ukame na ukosefu wa ajira.

Pia msaada umepelekwa katika makazi ya wakimbizi wa ndani ambako mbali ya chakula wanapewa pia huduma za afya ya mama na mtoto kwa kutumia vituo vinavyohamahama.

UNICEF na WFP ambao tayari wana viituo nchini humo 168 wamepanga kuonmgeza vituo vingine 100 hasa wakati huu ambapo msimu wa baridi unajongea ili kuweza kufika hata kwenye maeneo yasiyofikika.