WFP yasitisha mgao wa mlo unaoshukiwa kusababisha vifo Afrika Mashariki, uchunguzi waendelea

3 Mei 2019

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesitisha kwa muda usambazaji katika nchi 25 wa nafaka iliyorutubishwa au Super Cereal wakati huu ambapo uchunguzi unaendelea kubaini iwapo chakula hicho kina uhusiano na mlipuko wa magonjwa Afrika Mashariki.

Mlo huo ni mahindi au ngano ambayo imechanganywa na maharage ya soya na kurutubishwa na vitamini, madini na husagishwa na kuwa unga unaofungashwa kwa kilo 25. Chakula hicho kinatumiwa na WFP na wadau wake kuzuia utapiamlo  hususan miongoni mwa wanawake na watoto.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Roma, Italia inasema kuwa hatua ya kusitisha mgao huo wa chakula hicho kutoka kwa msambazaji wake mmoja inafuatia ripoti ya kwamba mwezi Machi na Aprili mwaka  huu watu watatu walifariki dunia na wengine 293 walilazwa hospitali huko Karamoja, kaskazini mwa Uganda baada ya kula chakula hicho kilichosambazwa na WFP.

Uchunguzi wa awali umeshindwa kuthibitisha pasipo shaka ni kitu gani kimesababisha ugonjwa huo ambapo hadi sasa chunguzi zaidi ya 2,400 zimefanyika kwenye maabara kubaini iwapo watu hao walikula kemikali za kuua wadudu, vijiumbe maradhi au chuma  nzito.

WFP imesema kwa kuwa imekuwa na shaka juu ya nafaka hiyo iliyorutubishwa ndio maana imeamua kusitisha kwa muda mgao wake ambapo kampeni zimeanzishwa huko Karamoja kusihi watu ambao bado wana akiba ya mlo huo waurejeshe.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter