Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujerumani yatoa dola milioni 2.3 kusaidia wakimbizi Tanzania na Rwanda

Wakimbizi wa ndani nchini Rwanda. Picha: UNHCR

Ujerumani yatoa dola milioni 2.3 kusaidia wakimbizi Tanzania na Rwanda

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limepokea zaidi ya dola milioni 2.3 kutoka Ujerumani ili kusaidia upatikanaji wa chakula kwa takribani wakimbizi nusu milioni walioko Tanzania na Rwanda.

Taarifa ya WFP iliyotolewa huko Dar es salaam, Tanzania imesema fedha hizo pamoja na mambo mengine zitanunua unga wa mahindi, mafuta ya kupikia na vyakula vyenye virutubisho kwa ajili ya wanawake wajawazito na watoto.

Halikadhalika fedha hizo zitatumika kuongeza dawa za kutibu Kifua Kikuu na zile za kupunguza makali ya Ukimwi ambazo zinatumiwa na wagonjwa wanaotibiwa kambini.

Naye Detlef Wächter ambaye ni balozi wa Ujerumani nchini Tanzania amesema msaada huo unazingatia jinsi ambavyo wanatambua umuhimu wa shughuli za mashirika ya kibinadamu kama WFP katika kusaidia wakimbizi.

Kwa mujibu wa WFP mwaka 2015 zaidi ya wakimbizi 258,000 kutoka Burundi walikimbilia Tanzania hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi pekee yenye idadi kubwa ya zaidi ya wakimbizi kutoka Burundi.