Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde walio hatarini si wakazi wa Tuvalu pekee bali sayari nzima ya dunia- Guterres

Mtoto mwenye umri wa miaka 16 akiogelea kwenye kijiji cha Aberao huko Kiribati ambacho kimefurika. Kisiwa hiki ni miongoni wa visiwa vilivyoathiriwa zaidi na ongezeko la kina cha maji ya bahari.
UNICEF/Sokhin
Mtoto mwenye umri wa miaka 16 akiogelea kwenye kijiji cha Aberao huko Kiribati ambacho kimefurika. Kisiwa hiki ni miongoni wa visiwa vilivyoathiriwa zaidi na ongezeko la kina cha maji ya bahari.

Chonde chonde walio hatarini si wakazi wa Tuvalu pekee bali sayari nzima ya dunia- Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameendelea kupigia chepuo suala la kila mkazi wa dunia pamoja na serikali kuchukua hatua kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchi, akisema kutochukua hatua si mbadala.

 

Katika tahariri aliyoandika leo kuhusu ukanda wa Pasifiki, Guterres amesema, “ni lazima kubadili mwenendo wa kuendesha shughuli zetu, kuzalisha nishati, kujenga miji na kulisha wakazi wa dunia.”

Katibu Mkuu amesema iwapo dunia inataka kuhimili mabadiliko ya tabianchi ni lazima kusaka utashi wa kisiasa wa kuchukua hatua thabiti za mabadiliko.

Kwa mantiki hyo amekumbusha kuwa, “viongozi lazima wafike kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambao utafanyika makao makuu ya UN mwezi Septemba wakiwa na suluhu madhubuti na hotuba.”

Tuvalu ambalo ni taifa la kisiwa kwenye bahari ya Pasifiki liko ukanda wa chini na hatarini zaidi kuzama kutokana na ongezeko la kiwango cha maji ya bahari litokanalo na mabadiliko ya tabianchi.
UNDP Tuvalu/Aurélia Rusek
Tuvalu ambalo ni taifa la kisiwa kwenye bahari ya Pasifiki liko ukanda wa chini na hatarini zaidi kuzama kutokana na ongezeko la kiwango cha maji ya bahari litokanalo na mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huo unalenga kusaka ahadi makinifu za kutekeleza mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi ambao  unahusisha kupunguza utoaji wa hewa chafuzi, mikakati ya kukabili na kuhimili mabadiliko ya tabianchi sambamba na ufadhili wa miradi ya muktadha huo.

Amerejelea ziara yake huko ukanda wa Pasifiki, ambao ndio uko mstari wa mbele kukumbwa na mabadiliko ya tabianchi sambamba na kuchukua hatua kukabiliana nayo.

“Nilisikia vilio vya okoa Tuvalu, Okoa Dunia,” amesema Katibu Mkuu akigusia kisiwa cha Tuvalu ambacho kinahaha kukabiliana na ongezeko la kina cha bahari ambacho kinatishia kuzama kwa kisiwa hicho.

Amesema kuwa alikuwepo eneo hilo kuonyesha mshikamano na wale walio hatarini na kuonyesha mbinu bunifu zinazotumiwa kwenye ukanda huo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Guterres amesema ongezeko la kina cha bahari kwenye ukanda wa Pasifiki ni mara nne zaidi ya kiwango cha ongezeko la kina cha bahari duniani, akisema hii inatishia uwepo wa mataifa hayo ya visiwani.

“Bahari ziko kwenye hatari kubwa, kuanzia kubabuliwa kwa matumbawe hadi kupotea kwa bayonuai ya baharini kutokana na uchafuzi unaosababishwa na plastiki,” ameonya Katibu Mkuu akiongeza kuwa hali za kupindukia za hewa nazo zinaongezeka na kutishia uhai wa binadamu na mbinu zao za kujipatia kipato.

Kudhihirisha kile alichoshudia, Bwana Guterres amesimulia ziara yake kwenye familia moja kisiwani Tuvalu ambayo kila wakati iko katika hofu ya eneo lao kumezwa kwa kuwa makazi yao yapo umbali hatua chache kutoka baharini.

“Baya zaidi wako katika machungu  na hofu ya kumezwa wakati wao si wachafuzi wakuu wa hali ya hewa na kutokana na makosa ya wachafuzi wakubwa, wao sasa wanalipa gharama,” amesema Guterres.

Ujenzi wa ukuta wa bahari kando kando mwa ufukwe wa Tarawa nchini Kiribati ili kukinga dhidi ya mawimbi ya Tsunami
Lauren Day/World Bank
Ujenzi wa ukuta wa bahari kando kando mwa ufukwe wa Tarawa nchini Kiribati ili kukinga dhidi ya mawimbi ya Tsunami

Sayari nzima iko hatarini

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema si Tuvalu pekee iliyoko hatarini au visiwa vidogo tu katika ukanda wa Pasifiki, bali sayari nzima ya dunia.

 Amesema “kile kinachotokea kwenye mataifa haya ni ishara ya kile ambacho kinasubiria kutokea kwetu. Wakazi wote wa dunia ni lazima waanze kuhisi madhara ya dharura ya tabianchi na hali itazidi kuwa mbaya”

Je nini kifanyike kufikia malengo muhimu?

Guterres amesema malengo yaliyowekwa dhahiri na wanasayansi ya kutokuwepo na uchafuzi utokanao na hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2050 na kupunguza kiwango cha ongezeko la joto duniani kwa nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi ifikapo mwishoni mwa karne hii ni muhimu.

Wakati jamii ya kimataifa inalenga malengo hayo, Katibu Mkuu amerejelea wito wake wa serikali kuwa ziondokane na kutoza kodi mishahara na badala yake kodi ielekezwe kwa watoaji hewa ya ukka akisema “tunapaswa kutoza wachafuzi badala ya watu.”