Tuvalu nathamini jitihada zenu za mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:Guterres

17 Mei 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anathamini na kutiwa moyo na jitihada zinazofanywa na serikali ya kisiwa cha Tuvalu katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza hii leo na waandishi wa habari kwa pamoja na waziri mkuu wa Tuvalu Enele Sosene Sopoaga mjini Funafuti Guterres amekipongeza kisiwa hicho ambacho amesema kinakabiliwa na hali mbaya ya mabadiliko ya tabianchi kuliko sehemu nyingine yoyote duniani. “nina wasifu sana, kwa jinsi mlivyoamua kupambana nakutekeleza mipango ya kukabiliana na kujenga mnepo hatua ambazo ulimwengu unapaswa kuzipenda na kuziunga mkono. Lakini ni muhimu kwamba serikali ambazo bado zinasababisha matatizo ambayo yanaiathiri Tuvalu kuelewa kwamba wanahitaji kubadilika. Wanahitaji kubadilisha sera zao za nishati, sera zao za usafirishaji,  jinsi ya kusimamia miji yao, jinsi wanavyotumia mafuta ili matokeo ya mabadiliko ya tabianchi kwa Tuvalu yanaweze kukomeshwa. Mabadiliko ya tabianchi hayawezi kukomeshwa huko Tuvalu ni lazima yakomeshwe ulimwenguni kote.

Guterres amesisitiza kuwa watapambana ipasavyo wakati wa mkutano wa kimataifa utakaofanyika  jijini New York baadaye mwaka huu ili kuhakikisha kwamba kimataifa hewa ukaa inapunguzwa na pia kudhibiti ongezeko la joto duniani na kusalia nyuzi joto 1.5. 

Pia amesema wakati huohuo anapenda kuonyesha mshikamano wa Umoja wa Mastaifa kwa serikali na watu wa Tuvalu hasa kwa dhamira ya kulinda taifa lao, kimazingira na kitamaduni katika malengo ya kiuchumi na kijamii kama moja ya kiungo muhimu cha utajiri wa Pasifiki na jumuiya ya kimataifa.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter